Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mauaji ya Khashoggi: Je Marekani imemsamehe mwanamfalme wa Saudia?
Kabla ya kuwa rais, Joe Biden aliita Saudi Arabia "kama katili " kwa wajiu wakee katika mauaji ya kutisha ya mwandishi wa habari wa Saudi Jamal Khashoggi.
Kama rais, aliidhinisha kutolewa mnamo Februari kwa ripoti ya ujasusi ya Marekani iliyomtuhumu mwanamfalme wa Saudi Mohammed Bin Salman.
MBS, kama anavyojulikana , amekana kuhusika kwa vyovyote na mauaji hayo
Lakini sasa, chini ya miezi sita baada ya kuchukua ofisi, utawala wa Biden umetoa makaribisho ya kufana kwa kaka mdogo wa MBS, Naibu Waziri wa Ulinzi, Prince Khalid Bin Salman. Ni ziara ya ngazi ya juu kabisa ya Saudia tangu mauaji ya Khashoggi mnamo Oktoba 2018.
"Kumekuwa na juhudi za pamoja [ndani ya washirika wa MBS] kuimarisha picha ya MBS na Saudi Arabia kwa ujumla ," anasema Michael Stephens, kutoka taasisi ya Royal United Services Institute (Rusi).. "Ufalme umekuwa ukizingatia sana fursa za kiuchumi," anaongeza, "wakati usemi mkali wa mapema juu ya usalama wa kanda hiyo ukipunguzwa."
Kwa hivyo hii inamaanisha kuwa MBS amesamehewa na mataifa ya Magharibi?
Sio kweli, hapana, na hakika sio na mashirika ya haki za binadamu, pamoja na UN, ambayo yanaendelea kutaka uchunguzi kamili na huru dhidi ya mtu mwenye nguvu zaidi nchini Saudi Arabia, MBS.
Maafisa kumi na tano wa serikali ya Saudi walisafiri kutoka Riyadh mnamo 2018 kwa ndege mbili za serikali kwenda Istanbul ambapo walimngojea Khashoggi, mkosoaji mkuu wa mwanamfalme. Mara tu alipotia mguu ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia walimzidi nguvu, wakamnyonga hadi kufa na kuukatakata vipande mwili wake.
Ukweli mgumu
Prince Khalid Bin Salman, ambaye amekaribishwa tu huko Marekani, alikuwa balozi wa Saudi Arabia huko Washington wakati huo. Awali alipuuza madai kwamba Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudia kama "uwongo kabisa na hauna msingi".
Wakati Uturuki ilipofichua kwa ulimwengu kile kilichotokea kwa kurekodi kisiri matukio katika ubalozi mdogo wa Saudia uongozi wa Saudi ulilazimika kubadilisha usemi. Uliwalaumu "operesheni mbaya" na mwishowe iliwahukumu maafisa kadhaa wadogo baada ya kesi ya siri.
Shirika la ujasusi la Marekani (CIA) lilihitimisha "kwa kiwango cha juu cha uhakika " kwamba operesheni hiyo isingeweza kufanywa bila ufahamu wa MBS mwenyewe. Marekani iliidhinisha vikwazo dhidi ya zaidi ya maafisa 70 wa Saudia wanaohusishwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na tangu mauaji hayo MB ameonekana kutengwa hadharani na viongozi wa Magharibi.
Walakini Saudi Arabia bado inaonekana na serikali nyingi za Magharibi kama mshirika muhimu, Kinga dhidi ya upanuzi wa Iran, mshirika muhimu wa kibiashara, mteja mzuri wa silaha na kiungo kikubwa cha kuleta udhabiti kwenye soko la mafuta. Kwa hivyo hapa ndipo siasa halisi zinapoingilia
Vyanzo vinavyomjua vizuri MBS vinasema kuna pengo kati ya msimamo rasmi wa serikali za Magharibi, kujitenga hadharani kutoka kwa MBS, na ukweli mgumu wa uhusiano wao wa nchi mbili na ufalme.
Ndio sababu kwa kujiamini na bila hata uwoga jamaa wa karibu zaidi wa MBS aliweza kukanyaga ndani ya ofisi za juu huko Washington wiki iliyopita.
'Suala la muda tu'
Katika kipindi cha siku mbili Prince Khalid Bin Salman alifanya mikutano na waziri wa mashauri ya kigeni , Anthony Blinken; Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa rais, Jake Sullivan; Katibu wa Ulinzi, Lloyd Austin; na Mwenyekiti wa Wakuu wa jeshi , Jenerali Mark Milley. Orodha hiyo pekee inatoa taswira ya umuhimu ambao Marekani inaichukulia mshirika wake Saudia hata ikiwa, kwa kushangaza, hakukuwa na tangazo la hapo awali la ziara ya Prince Khalid.
Mambo mengi yalijadiliwa, pamoja na vita huko Yemen, ambavyo Saudi Arabia inajaribu kujiondoa baada ya kushindwa kuwaangamiza wahouthi wanaoungwa mkono na Iran, ambao walichukua madaraka kinyume cha sheria mnamo 2014.
Nishati, soko la mafuta, usalama katika upeembe wa Afrika na kuanza tena kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran yote yalikuwa mambo yaliyojadiliwa. Vivyo hivyo, iliripotiwa, suala la Afghanistan, ambako vikosi vya Marekani sasa vimejiondoa na ambapo kuna hofu Taliban itarejea mamlakani na kuipa Al-Qaeda nguvu pia ilijadiliwa .
Wanadiplomasia wanaojua Saudi Arabia wanakubali kwamba inaweza kuwa, wakati mwingine, nchi ngumu kuhusiana nayo. Mashaka huko Magharibi juu ya Mohammed Bin Salman labda yatadumu urefu wa maisha yake.
"Bado njia sio shwari kwa MBS," anasema Michael Stephens wa Rusi. "Wakati zaidi utahitajika kabla nchi za Magharibi kuwa tayari kushirikiana naye. Lakini mambo yanaboreka kwake na labda itakuwa suala la muda tu kabla ya kuweza tena kutembelea miji mikuu ya Magharibi."