Jovenel Moïse: Haiti yaomba vikosi vya kigeni baada ya rais wake kuuawa

Maelezo ya video, Polisi wamewatoa kwa umma washukiwa wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya rais wa Haiti pamoja na silaha na paspoti zao

Haiti imeomba vikosi vya kigeni kupelekwa nchini humo kulinda miundo mbinu muhimu baada ya kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse.

Ombi hilo lilitumwa kwa serikali ya Marekani na Umoja wa Mataifa (UN), lakini Marekani imesema haina mpango wakutoa msaada wa kijeshi "wakati huu".

Awali polisi wa Haiti walisema kundi la mamluki 28 wa kigeni walihusika na mauaji ya rais siku ya Jumatano.

Baada ya makabiliano makali ya bunduki katika mji mkuu wa Port-au-Prince, 17 kati yao walikamatwa.

Baadhi ya wanachama wa kundi hilo ambalo Haiti inasema ni pamoja na wanajeshi wastaafu wa Colombia, walizuiliwa katika nyumba waliokuwa wakitumia, baada ya wengine kuingia makazi ya kidiplomasia ya Taiwan, polisi walisema.

Haitian solder with a skull face mask

Chanzo cha picha, Getty Images

Washukiwa watatu waliuawa na polisi, wengine wanane wanatafutwa.

Ijapokuwa Markani haitatoa msaada wa kijeshi, ilisema siku ya Ijumaa kwamba itawapeleka maafisa shirika la upepelelezi la FBI na wale wa usalma wa kitaifa nchini Haiti kusaidia kwa kuchunguza.

Baraza la Usala la Umoja wa Mataifa linastahili kuidhinisha mpango wa kupelekwa kwa vikosi vya kimataifa nchini Haiti chini ya udhamini wa UN.

Mauaji hayo yamesababisha maandamano ya umma Haiti, taifa masikini zaidi Amerika. Hali ya hatari imeendelea kudumishwa kote nchini humo na kwa sasa haijulikani ni nani anaongoza serikali.

Silaha na pesa zanaswa

Washukiwa waliokuwa wamelowa damu, waliioneshwa kwa ummma kupitia kwa vyombo vya habari siku ya Alhamisi pamoja na silaha walizokuwa nazo.

Bado haijabainika ni nani aliyepanda shambulio hilo na lengo lake.

Shambulio dhidi ya makazi ya rais lilifanyika usiku wa Julai 7, wakati wanaume waliojihami kuvamia makazi yake, kumpiga risasi na kumuua na pia kumjeruhi mke. Bw. Moïse, 53, alipatikana amelala chini akiwa na majeraha 12 ya risasi, kulingana mamlaka.

Martine Moïse, 47, ambaye alijeruhiwa vibaya anaendelea kupata nafuu baada ya kusafirishwa Florida kwa matibabu.

Washukiwa walipatikana na silaha na dola za Marekani, kitabu cha rais cha kuandika hundi na mtambo wa uliokuwa na kanda ya video kutoka kwa camera za ulinzi nyumbani kwake, gazeti la Le Nouvelliste liliripoti.

Taiwan imethibitisha 11 kati ya washukiwa hao walikamatwa baada ya kuingia katika makazi yake ya kidiplomasia.

Raia waliokuwa na hasira waliungana na polisi kuwatafuta watu hao walio, na kusaidia polisi kuwapata baadhi yao waliokuwa wakijificha msituni. Raia walichoma moto magari matatu yaliyoshukiwa kuwa ya majambazi hao hatua ambayo huenda imevuruga uchunguzi.

Mashoka, vifaa vya kukata waya, hati za dhamana za dola ya Marekani na pasipoti za Colombia zimepatikana

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mashoka, vifaa vya kukata waya, hati za dhamana za dola ya Marekani na pasipoti za Colombia zimepatikana

Mkuu wa polisi Léon Charles ametoa wito wa utulivu, na kuomba raia kutochukua sheria mikononi mwao.

Msaada wa Colombia

Katika mkutano na vyombo vya habari siku ya Alhamisi, polisi waliwaonesha waandishi wa habari pasipoti za Colombia.

"Raia wa kigeni waliingia nchini kumuua rais wetu," Bw. Charles alisema, washukiwa waliokuwa wamevishwa pingu wakiwa wamekaa chini sakafuni nyuma yake.

Serikali ya Colombia pia imeahidi kusaidia Haiti katika juhudi za uchunguzi.

Mkurugezi wa polisi wa Colombia, Jenerali Jorge Luis Vargas, alisema 17 kati ya washukiwa hao ni wanajeshi wa zamani wa nchi hiyo.

Huku hayo yakijiri, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ilisema haiwezi kuthibitisha ikiwa raia yeyote wa nchi hiyo amezuiliwa.

Hata hivyo vyombo vya habari vya Marekani na Canada, vinaripoti kuwa mmoja wa washukiwa aliyekuwa na uraia pacha aliyekamatwa, James Solages, 35, anatokea Florida na alikuwa mlinzi wa ubalozi wa Canada nchini Haiti.

Short presentational grey line

Nani anayeongoza nchi?

Mauaji hayo yameleta mkanganyiko juu ya nani aongoze Haiti, angalau hadi uchaguzi ufanyike.

Kanuni katika katiba zimvurugwa wakati huu ambapo hakuna Bunge - mizozo ilimaanisha uchaguzi mnamo Oktoba 2019 haukufanyika - kwa hivyo haiwezi kuchagua rais mwingine.

Marekebisho ya katiba, ambayo hayakubaliwi na kila mtu, yanaonyesha kwamba waziri mkuu anapaswa kuongoza, lakini uhalali wa Bw Joseph unapingwa.

One of a number of cars set on fire during anger over the killing

Chanzo cha picha, EPA

Mwanasiasa mwingine, Ariel Henry, alikuwa ameteuliwa kama Waziri Mkuu mpya muda mfupi kabla ya mauaji, lakini alikuwa bado hajaapishwa.

UN inasema Bw Joseph anapaswa kuendelea kuwa kiongozi mpaka uchaguzi utakapofanyika baadaye mwaka huu.

Amesema hatogombea urais. "Siko hapa kukaa muda mrefu. Tunahitaji kufanya uchaguzi. Sina ajenda ya kibinafsi," aliiambia BBC.

Haiti imekuwa ikikumbwa na machafuko ya kisiasa na kiuchumi, na hivi karibuni na ongezeko la vita vya magenge.

Kulikuwa na maandamano yaliyoenea yakitaka kujiuzulu kwa Bw Moïse, ambaye alikuwa akitawala kwa amri tangu uchaguzi ucheleweshwe.