Rais Samia Hassan azidi kueneza diplomasia na nchi jirani-Botswana ni ya hivi punde

Tanzania na Botswana zimekubaliana kufufua tume ya pamoja ya ushirikiano iliyoanzishwa mwaka 2002 na kufanya mkutano wake wa mwisho mwaka 2009.

Hayo yamesemwa leo na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi aliye nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

''Tumewataka mawaziri wetu wa mambo ya nje kuitisha mara moja mkutano huu, tutaangalia njia rahisi na njema kwa nchi zetu mbili kufanya mkutano huu, lakini ni muhimu mkutano huu ukafanyika kwa haraka ili kuangalia maeneo ya ushirikiano ya kiuchumi na kijamii kwa undani zaidi.''

Rais Samia amesema ''ziara hii inatupa fursa kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu''

Waliyoyazungumza viongozi hao

Masisi alijikita zaidi katika kutafuta namna ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili hususani katika nyanja za kiuchumi na katika hilo wameangazia eneo la biashara na uwekezaji.

"Tumewaagiza mawaziri wetu wa mambo ya nje kufungua tume ya ushirikiano na waanze kukutana ndani ya miezi mitatu na kuanza kuyafanyia kazi yale ambayo tumejadiliana katika sekta mbalimbali za kiuchumi, ulinzi na usalama pamoja na janga la corona," Alisema Rais Masisi.

Wameona kuwa biashara kati ya mataifa hayo mawili imeongezeka kutoka shilingi za kitanzania milioni 731 mwaka 2005 mpaka bilioni 3.5 mwaka wa 2020.

Botswana imewekeza nchini Tanzania miradi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 231 na kutoa ajira zipatazo 2128 kwa Watanzania.

Na miongoni mwa miradi mikubwa iliyowekeza Tanzania ni ule mradi wa Mlimani City walioingia mkataba na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Rais Samia amemhakikishia Rais Masisi kuwa wataulinda mradi huo ili uweze kuendelea kwa muda mrefu kwasababu mradi ule pia mbali na biashara umekuwa kivutio kwa Watanzania wengi.

Pamoja na kuongezeka kwa biashara na uwekezaji marais hao wameona kuwa kiwango hicho ni kidogo sana ukilinganisha na uhusiano uliiopo baina ya nchi hizo na fursa zilizopo kwenye mataifa hayo mawili.

Hivyo basi wamekubaliana kuwahamasisha wafanyabiashara wa mataifa hayo mawili kuchangamkia fursa zilizopo.

Kubadilishana uzoefu

Pia wamekubaliana kutanua maeneo ya ushirikiano na kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali.

''Kama mjuavyo Botswana inasifika kwa kupiga hatua kubwa kiuchumi barani Afrika na sekta za uchumi wa Botswana ni madini, yaani Almasi ambayo inaongoza kwa kuuza madini hayo duniani.

lakini haiongozi kwa bahati mbaya, bali ni kwa kupanga na kujiwekea mikakati mizuri kushikilia zao lao na kuweza kuuza duniani.

''Tumejifunza nasi mengi kutoka kwao na tumekubaliana timu yetu ya wataalamu waende Botswana kujifunza mikakati ya kuendeleza madini yetu nchini kwa ajili ya biashara duniani''.Alisema Rais Samia.

Pia Botswana ni wauzaji wazuri wa nyama duniani, hivyo wamekubaliana kushirikiana kwenye maeneo hayo.

Marais hao wamejadiliana kuhusu masuala ya kikanda, kibara na kidunia na hasa kuhusu maendeleo ya usalama ambapo wamekubaliana kuendeleza ushirikiano hususani kupitia taasisi ambazo nchi hizo mbili ni wanachama, kama vile SADC, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Uhusiano wa Tanzania na Botswana

Botswana ilitumika kama njia ya wapigania uhuru waliotoroka nchi zao kwenda Tanzania na Zambia kupanga mikakati ya ukombozi.

Miongoni mwa wapigania uhuru waliopokelewa kupitia Botswana ni mzee Nelson ambaye alifika Tazania kwa ajili ya mikakakati hiyo.

Tanzania na Botswana ni miongoni mwa nchi zilizounda jumuia ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADCC ya zamani ya mwaka 1980, huu ni uthibitisho kuwa Tanzania na Botswana ni nchi zilizo na uhusiano wa muda mrefu.

Nchi hizi mbili zinajivunia kuwa na uhusiano mzuri wa kidugu wa muda mrefu, msingi wa uhusiano uliopo umechangiwa na harakati za kupigania uhuru chini ya mwamvuli wa nchi hizo kuwa mstari wa mbele, ambapo zilichangia sana harakati za uhuru wa nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe.