Shambulio la Katumba Wamala: Kwanini Uganda ina tatizo la mauaji ya watu mashuhuri?

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi Tanzania

Tukio la kushambuliwa kwa Waziri wa Ujenzi na Usafirishaji Uganda, Jenerali Katumba Wamala, wiki hii linaibua swali moja kubwa la kiusalama kuhusu watu waliowahi kuwa makamanda wa Jeshi la Uganda tangu lilipobadilishwa muundo kutoka kuwa Jeshi la Msituni (NRA) na kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).

Wamala alinusurika kuuawa Juni 2 mwaka huu baada ya gari alilokuwamo kushambuliwa na watu wasiojulikana katika tukio lililosababisha kifo cha binti yake, Brenda, na dereva wake.

Wamala ni Mkuu wa Majeshi (CDF) wa tatu wa Uganda; akitanguliwa na Jenerali James Kazini na Jenerali Aronda Nyakairima. Watangulizi wake wawili hao wote wamefariki katika mazingira yenye utata hadi leo.

Aronda alifia kwenye ndege wakati akiwa ametoka safarini ughaibuni akirejea Uganda

Kama Wamala angepoteza maisha yake jana - gari lake likiwa limepigwa risasi zaidi ya 50 kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo, Uganda ingekuwa haina CDF mstaafu zaidi ya wale waliokuwa Makamanda wa NRA - Elly Tumwine, Salim Salehe na Mugisha Muntu

Tukio la kushambuliwa kwa Wamala limeacha wengi midomo wazi nchini Uganda kwa sababu mhusika ni mtu mashuhuri na mwenye wadhifa mkubwa katika nyanja ya ulinzi na usalama - akiwa analindwa na mwenye uwezo wa kujilinda binafsi.

Jambo linaloshangaza wengi ni kwamba ndiyo staili hiyohiyo iliyotumika kuua Waganda wengine mashuhuri; wauaji wakiwa wanashambulia kwa kutumia usafiri wa bodaboda.

Akina nani wengine wameuawa Uganda kwa mtindo huo?

Waganda mashuhuri ambao wamewahi kupoteza maisha kutokana na mashmbuliaji ya aina hii ni Muhammad Kirumira aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Buyende aliyeuwa Septemba 8, 2018.

Mwingine ni aliyekuwa Msemaji wa Jeshi la Polisi la Uganda, Andrew Felix Kaweesi, aliyeuwa jijini Kampala kwa staili hiyo mnamo Machi 17 mwaka 2017 na kuacha maswali mengi kuhusu kifo hicho.

Mhanga mwingine wa mashambuliji ya aina hii alikuwa ni Joan Kagezi - mmoja wa maofisa wa ngazi za juu katika Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali ya Uganda (DPP), aliyekutwa na mauti Machi 30 mwaka 2015 na hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo hadi sasa.

Novemba 26, mwaka 2016, ilikuwa zamu ya Meja Muhammad Kigundu aliyeuwa pamoja na mlinzi wake, Steven Mukasa katika eneo la Masanafu na kuacha watu wengi katika mshtuko mkubwa.

Mbunge wa Jimbo la Arua, Ibrahim Abiriga, yeye alikutwa na mauti ya namna hiyo pamoja na kaka yake, Saidi Buga Kongo katika Mkoa wa Wakiso mnamo Juni 8, 2018 na hadi sasa hakuna aliyekamatwa.

Katika orodha hiyo, yapo pia majina ya viongozi wa dini ya Kiislamu kadhaa ambao wamekumbwa na mauaji hayo na kwa sababu orodha ni ndefu, itoshe tu kutaja wachache hao mashuhuri.

Tatizo ni nini?

Tatizo la kwanza la mauaji haya ni kwamba kuna kitu kimoja kinafanana - hakuna wahusika waliowahi kukamatwa baada ya kufanya matukio ya namna hii.

Kwa namna moja au nyingine, inaonekana vyombo vya ulinzi na usalama vya usalama vya Uganda vinakosa namna ya kusaka, kukamata na kushitaki wahusika wa mauaji ya namna hii na labda sasa wahalifu wameona pengine hiyo namna bora zaidi ya kufanya uhalifu huo.

Miaka michache nyuma, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, alitangaza mikakati 11 ya kiulinzi na kiusalama kwenye kukabili jambo hilo - ikiwamo kufunga kamera za usalama, kukataza waendesha pikipiki kufunika nyuso zao, kurekodi bunduki zote zilizopo Uganda, kuwa na namna mpya za vyombo vya usafiri zilizorekodiwa mtandaoni na mbinu nyingine lakini hadi sasa machache yamefanikishwa.

Kwa hali ilivyo sasa, inawezekana itakuwa vigumu pia kuwakamata waliojaribu kumuua Katumba kwa sababu kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uganda, kamera za usalama zimefungwa katika maeneo fulani tu na maeneo mengine hazipo.

Kwa sababu hiyo, kama wahalifu wameshajua kwamba ukifanya tukio fulani kwa namna fulani huwezi kukamatwa, huo ndiyo utakuwa utaratibu wa kudumu wa kufanya uhalifu.

Siasa za Uganda na askari

Tangu enzi za Milton Obote, askari (wanajeshi) wamekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Uganda. Idi Amin alikaa miaka saba madarakani na Museveni sasa amefikisha zaidi ya miongo mitatu madarakani. Wote hao wawili walikuwa askari waliofanya mapinduzi kuingia madarakani.

Watawala wa kiraia wa Uganda kama vile Obote, Yusuf Lule na Godfrey Binaisa walikaa madarakani kwa vipindi vifupi pengine kwa sababu siasa za Uganda - walau baada ya Uhuru wa taifa hilo, zinawapa heshima ndogo raia.

Kwa maana hiyo, askari yeyote mwenye heshima na umaarufu ndani ya Uganda, anaweza kuwa katika hatari ya maisha yake kutoka kwa wale wanaodhani anaweza kuja kuwa tishio kwa wengine wanaotaka madaraka makubwa.

Chukulia mfano wa Katumba Wamala. Ana historia ya kuwa Mkuu wa Majeshi na askari hodari aliyepata mafunzo katika vyuo mashuhuri kikiwamo kile cha Monduli kilichopo Tanzania, amesoma vizuri, anatoka katika kabila lenye watu wengi zaidi nchini kwake na katika taifa linalothamini askari.

Kwa siasa za Uganda, huyu ni mwanasiasa tishio kwa wengine wote - walio madarakani sasa na wengine wanaotaka madaraka mara baada ya muda wa Museveni kumalizika.

Siasa za Uganda kimataifa

Jeshi la Uganda ndilo linafanya kazi ya kulinda Amani nchini Somalia kupitia Umoja wa Afrika (AU). Mara kwa mara UPDF hupambana na magaidi wa Al Shabab ambao kwao Uganda ni kikwazo cha wao kutawala nchini humo.

Wamala siyo tu kwamba aliwahi kuwa CDF wa Uganda lakini pia aliwahi kuongoza vikosi vya AMISON vilivyoko Somalia. Kama Al Shabab wanataka kuitisha Uganda iondoke Somalia, tukio kama hili dhidi ya Katumba ni mojawapo ya njia za kuwatisha Waganda.

Katika tafiti na historia mbalimbali za vitendo vya kigaidi, inafahamika kwamba lengo kuu la mauaji ya kisiasa au ugaidi ni kusababisha hofu na woga mkubwa kwa yule ambaye anaonekana ana nguvu kuliko magaidi.

Tayari Rais Museveni amewataja waliothubutu kumshambulia Katumba kama "nguruwe" ambao ipo siku watakamatwa.

Hata hivyo, wengi wa Waganda wanaamini kwamba wakati wa kutoa maneno makali pekee umepita na sasa kinachosubiriwa ni vitendo vya kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wanaohusika na vitendo hivyo.

Hii ni kwa sababu, kama wameweza kuthubutu kutaka kumuua CDF mstaafu, nini kitawazuia sasa kumsaka mwingine yeyote wamtakaye?

Hili ni swali ambalo mamlaka za ulinzi na usalama za Uganda zinapaswa kulijibu.