Waathirika wa operesheni ya virutubisho vya matiti kufidiwa

Zaidi ya wanawake 2,500 ambao ni waathirika wa sakata ya upandikizaji matiti wanastahili kupokea fidia, mahakama ya rufaa nchini Ufaransa imesema.

Pia mahakama hiyo imeunga mkono uamuzi wa awali ulioipata kampuni moja ya Ujerumani ya TUV Rheinland, iliyokuwa imepewa cheti cha usalama, kwamba ina makosa katika upandikizaji huo uliokuwa na dosari, ikiwemo uzembe.

Kesi hiyo huko mjini Paris inajumuisha wanawake 540 wa Uingereza, ambao walipata madhara ya muda mrefu ya kiafya baada ya kufanyiwa upandikizaji wa matiti.

Matokeo ya kesi hiyo, huenda yakachangia pakubwa kesi zingine za waathirika wengine.

Jan Spivey ni mmoja kati ya wanawake walioathirika katika kesi hii. Alipewa virutubisha vya matiti baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa matiti kwasababu ya ugonjwa wa saratani.

Alianza kutokwa na vidonda na kupata maumivu makali kwenye viungo vya mwili, kifuani na mgongoni, uchovu, kuumwa na kichwa na kupata wasiwasi. Na kubaini kuwa upasuaji aliofanyiwa wa upandikizaji matiti umekuwa ukivuja silikoni ndani ya mwili wake.

Anasema upandikizaji huo umekuwa na athari kubwa sana katika afya yake ya akili.

"Upasuaji wa kurutubisha matiti niliofanyiwa miaka 20 iliyopita, bado unaniathiri maishani mwangu hadi hii leo, afya yangu na ustawi wangu."

"Nimekuwa na hasira sana kila siku ya kipindi chote hicho cha miaka 20. Na kuna uwezekano mkubwa kati ya yale ninayotarajia, ni kuondokana na hisia ya hasira na majonzi."

Chipu ya Silikoni

Kati ya mwaka 2001 na 2010, vipandikizi hivyo vya kiwango duni vilitengenezwa na kampuni moja ya Ufaransa.

Kampuni hiyo ilifilisika mwaka 2010 na mwasisi wake baadaye akafungwa jela baada kubainika kuwa vipandikizi vilivyokuwa vinatumika vilikuwa vimejazwa vipande vya silikoni duni ambavyo havikuwa vimeidhinishwa kwa matumizi ya binadamu.

Inakadiriwa kuwa hadi wanawake 400,000 kote duniani walikuwa wamepata matibabu ya upandikizaji huo duni ambao ulikuwa kinyume na sheria.

Amerika Kusini ndio iliyoathirika zaidi, hasa Colombia ambapo inakadiriwa kuwa wanawake 60,000 ni waathirika huku nchini Uingereza ikisemekana kuwa wanawake 47,000 wameathirika.

Olivier Aumaître, mwanasheria anayemwakilisha Jan Spivey na wengine karibu 2,700 katika kesi iayoendelea sasa hivi, anatarajia kuwa baada ya miaka 10 ya kupigania haki ya wanawake hao mahakamani, Alhamisi, itakuwa siku muhimu kwao.

"Tunatarajia kufika kipindi ambacho kitakuwa mapinduzi. Uamuzi chanya pengine utakuwa ndio unatamatisha kipindi kirefu cha maswali mengi ambacho wamekipitia. Na pia kiasi cha fidia yenyewe kitakuwa mwanzo mpya kwa waathirika."

Kesi hiyo ambayo inafahamika kama TUV1, ilikuwa ya kwanza kuwasilishwa mahakama miaka kumi iliyopita dhidi ya kampuni ya Ujerumani ambayo ilitoa cheti kinachohakikisha usalama cha Ulaya kwa vipandikizi vilivyokuwa vinatumiwa.

Mahakama ya rufaa huko Paris itaamua ikiwa kampuni hiyo ya Ujerumani ilifanya uzembe na ikiwa ni hivyo, ikiwa wanawake walioathirika wanastahili kufidiwa.

Uamuzi wa mahakama unatarajiwa kuwa na athari kubwa zaidi kwa karibu wanawake 20,000, nusu yao wakiwa ni raia wa Uingereza, ambao nao pia wamewasilisha kesi yao mahakamani huko Ufaransa.

Alifie Jones yuko nyumbani na kijana wake ambako amekuwa akiendelea kupata afueni baada ya kuondolewa vipandikizi vya matiti alivyokuwa amewekewa mwezi uliopita.

Na hatimaye, akashawishiwa na rafiki yake kuondoa vipandikizi alivyowekewa baada ya kupitia machungu memgi kwa miaka mingi mno.

Anasema kibaya zaidi, alikuwa anajiuliza mbona kila wakati anaumwa: "Bila kujua chanzo cha matatizo, magojwa ya ajabu ajabu na hata kushindwa kufanya mazoezi. Kushindwa kuwa mchangamfu, kutoishi maisha yangu ninavyotaka yaani nilikosa furaha kila wakati."

Daktari wa upasaji alishutuka alichokiona baada ya kufanya upasuaji na kuondoa moja ya vipandikizi. Kilikuwa kimevunjika vunjika vipande vipande mwilini mwake - na mwili wake ukawa unaingia jeli ya silikoni inayotumika viwandani.

"Siamini vipande vile ndio nilikuwa nimepandikizwa. Sijui viliidhinishwa vipi na mamlaka, sijui.

"Nilihisi vibaya kwa kuukosea mwili wangu na kwanini niliwekwa. Lakini nina hasira zaidi kuwa mwanadamu anaweza kumtendea binadamu mwingine kitendo kama hicho."

Hata hivyo, kampuni ya TUV Rheinland ilikanusha madai hayo ingawa ikakataa kusema lolote.