Kwanini Marekani imeziwekea vikwazo kampuni za kompyuta China?

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imeorodhesha kampuni saba za China ikidai kutengeneza kompyuta maalum ya kusaida majeshi yake.
Ni hatua ya kwanza iliyochukuliwa na utawala wa Biden kufanya iwe vigumu kwa china kupata teknolojia ya Marekani.
Siku ya Alhamisi, kampuni tatu na matawi manne ya kituo cha kitaifa cha kompyuta nchini China ziliongezwa katika orodha hiyo.
Hatua hiyo inazuia kampuni za Marekani kusafirisha nje teknolojia kwa kampuni hizo bila ya kibali rasmi.
Idara ya Biashara ya Marekani imesema kampuni hizo zilihusika katika utengenezaji wa komputa maalum ambayo inatumiwa na ''washirika wa majeshi'' ya China kuwawezesha kutengeneza programu ya kuunda silaha za maangamizi.
Kampuni zilizoorodheshwa zinaongoza katika utengenezaji wa komputa China na ni viungo muhimu katika mpango wa Beijing wa kujitosheleza kiteknolojia.
Waziri wa biashara wa Marekani Gina Raimondo amesema utawala wa Biden utatumia ''mamlaka yake kuzuia China kufikia teknolojia ya Marekani kudhoofisha juhudi zakisasa za kijeshi".

Utawala wa Trump pia ulilenga kampuni kadhaa za China zilizoshukiwa kutumia teknolojia ya Marekani kwa shughuli za kijeshi, ikiwemo kampuni ya kutengeneza simu ya Huawei.
Hatua ya Bw. Biden ya siku ya Alhamisi inazitaka kampuni saba za China kupata leseni ya kuzifikia teknolojia za Marekani, ikiwemo miundombinu ya chip na Itel na watengenezaji wengine wa chip za Marekani.
Huku marufuku hiyo ikizizuia makampuni yaliyo na makao yao Marekani kutoa huduma na kuuza bidhaa kwa makampuni ya China, haijumuishi zile zinazotengenezwa katika vituo vingine nje ya Marekani.
Moja ya kampuni hizo ni TSMC, iliyo na makao yake Taiwan.
Supercomputer ni nini?
Supercomputer ni aina ya kompyuta ambayo utendakazi wake ni wa hali ya juu ikilinganishwa na kompyuta ya kawaida na ina uwezo wa kufanya mabilioni ya hesabu ndani ya sekunde moja.
Kompyuta za aina hii inatengenezwa kutokana na maelfu ya mifumo iliyounganishwa na inatekeleza majukumu kama ya kutabiri hali ya hewa na mienendo ya tibia nchi, kuiga majaribio ya nyuklia a utafiti wa dawa
Pia ni muhimu katika utengenezaji wa silaha za hali ya juu kama makombora yasafirio kwa kasi.
'Hawasubiri'
Marekani inahofia China inaweza kufikia teknolojia ambayo inasaidia majeshi yake kuwa na uwezo wa kukaribia majeshi ya Marekani.
Utawala wa Biden kwa sasa unachunguza hatua kadhaa zinazohusiana China-ambazo zilichukuliwa na Donald Trump, ikiwa ni pamoja na kuizuia Marekani kuwekeza katika kampuni za China zinazoaminiwa kuwa na mafungamano na jeshi.
"Unadhani China inachelea kuwekeza katika miundo mbinu yao ya kidijitali au utafiti na maindeleoo? Nakuahidi, hawatasubiri," Bw. Biden alisema katika hotuba yake siku ya Jumatano.
Bw. Biden alisema China na ulimwengu mzima "wameanza mbele yetu kuwekeza katika mipango ya siku zijazo".












