Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Pep Guardiola amsifu Haaaland, je mshambuliaji huyo atairarua Man City leo?
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amempongeza mshambuliaji wa Borussia Dortmund Erling Braut Haaland kuwa ni mchezaji bora kwa sasa.
Hii leo, City inaikaribisha Dortmund katika dima la Eithad katika mchezo wa kwanza wa robo fainali wa kombe la Klabu Bingwa Ulaya (Champions League).
Guardiola amekuwa akimnyemelea mshambuliaji huyo kwa muda sasa akitaka kumsajili japo City hawapo tayari kutumia zaidi ya pauni milioni 100 kumsajili, hatua ambayo kocha huyo anaitetea.
"Kufikia sasa klabu hii imeamua kutotumia karibu pauni milioni 100 kwa mchezaji mmoja," Guardiola amesema.
"Soka ni mchezo unaojumuisha timu, kila mmoja anachangia. Na wala sio tu mchezaji mmoja."
Haaland, 20, amefunga magoli 39 kwa klabu yake na taifa lake msimu huu, ikiwemo magoli 10 katika mechi alizoshiriki kwenye Champions League.
Huku vinara hao wa ligi ya primia wakithibitisha Jumatatu kuwa mshambuliaji Sergio Aguero, 32, ataondoka mkataba wake utakapokamilika mwisho wa msimu, Haaland amesemekana kuwa mlengwa mkuu kama mbadala wa Muarjentina huyo.
Hata hivyo, Guardiola anahisi kima kinachohitajika kwa mchezaji huyo ni cha juu sana.
Inasemekana kuwa Dortmund inataka karibu euro milioni 150 sawa na (pauni milioni 128) ili kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa raia wa Norway, ambaye wakala wake Mino Raiola amekutana na Barcelona na Real Madrid kuhusu uwezekano wa uhamisho wake.
"Ukweli ni kwamba hatujawahi kutumia dau la juu kabisa kwa mchezaji mmoja, pesa nyingi hasa, inakuongezea mtazamo chanya kwako," Guardiola ameongeza.
"Kile ninachoweza kusema pekee ni kuwa kwa kuzingatia umri wake, Haaland ni mshambuliaji wa kipekee.
"Pengine siku za usoni [matumizi ya zaidi ya pauni milioni 100 kwa mchezaji mmoja] yanaweza kutokea ikiwa wataamua ni muhimu kuimarisha timu katika kipindi cha miaka mitano ijayo, miaka 10 ijayo, kwasababu nyingi tu. Lakini hadi kufikia sasa, klabu, shirika, Mkurugenzi Mtendaji, mkurugezi wa michezo wameamua kutofanya hivyo na hiyo ndio sababu."
Manchester City ilimsajili Rodri kutoka Atletico Madrid aliyeweka rekodi katika klabu hiyo ya pauni milioni 62.8 mnamo mwezi Julai 2019.