Mzozo wa Tigray Ethiopia: Mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani yakemea 'ukiukaji wa haki za binadamu'

Umoja wa mataifa yenye nguvu ya kiuchumi ya G7 umesema "una wasiwasi mkubwa" na ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo lililokumbwa na mizozo nchni Ethiopia.

Kundi hilo, ambalo linajumuisha Uingereza, Marekani na EU, lilitaka vitendo vya jinai vilivyoripotiwa vichunguzwe na wale waliohusika wawajibishwe.

Walihimiza pia Eritrea kuondoa wanajeshi ambao wanapigana pamoja na Ethiopia dhidi ya vikosi vya Tigray.

Vikosi vya nchi zote mbili vimeshutumiwa kwa ukiukwaji wa haki nyingi.

Vitendo hivyo ni pamoja na mauaji ya raia , unyanyasaji wa kijinsia, uporaji na unyanyasaji wa wakimbizi. Uchunguzi wa BBC wa Africa Eye pia umebaini ushahidi unaonesha kuwa jeshi la Ethiopia lilifanya mauaji ambayo watu wasiopungua 15 walipoteza maisha.

Eritrea imepuuzilia mbali madai hayo, wakati waziri mkuu wa Ethiopia hapo awali alikanusha taarifa za kuuawa kwa raia.

Mzozo ulianza baada ya wapiganaji wa Tigray People's Liberation Front (TPLF) kuziteka ngome za kijeshi katika jimbo hilo.

TPLF kimekuwa ni chama tawala katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia, lakini kilikuwa na uhasama mkubwa na Bw Abiy kuhusu hali ya baadae ya mfumo wa shirikisho wenye misingi ya kikabila na jukumu lake katika serikali.

"Tunalaani mauaji ya raia, unyanyasaji wa kijinsia na kupigwa risasi kiholela na kuhamishwa kwa lazima kwa wakazi wa Tigray na wakimbizi wa Eritrea," kundi la G7 lilisema katika taarifa yao Ijumaa.

"Ni muhimu kwamba kuna uchunguzi huru, wa uwazi na usio na upendeleo katika uhalifu ulioripotiwa na kwamba wale waliohusika na ukiukwaji huu wa haki za binadamu wanawajibika," iliongeza.

Taarifa hiyo, ambayo ilitolewa na mawaziri wa mambo ya nje wa kikundi hicho na Mwakilishi Mkuu wa EU, pia ilionesha wasiwasi kuhusu "kuongezeka kwa ukosefu wa chakula" na ikataka "ufikiwaji wa kibinadamu wa haraka, bila kizuizi".

Lakini ilikaribisha tangazo la hivi karibuni kutoka kwa Bw Abiy kwamba Eritrea itaondoa wanajeshi wake kutoka Ethiopia. Hakutaja tarehe, hata hivyo, na Eritrea haijathibitisha kujitoa.

Kumekuwa na uhasama kwa muda mrefu kati ya Tigray na serikali huko Eritrea, ambayo inashiriki mpaka na eneo hilo.