Vita vya Yemen: Joe Biden asitisha msaada wa operesheni za kivita baada ya kubadilisha sera ya kigeni

Marekani itasitisha kuunga mkono operesheni za uvamizi zinazotekelezwa na washirika wake nchini Yemen ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na vita vya miaka sita huku watu zaidi ya 110,000 wakiaminika kuwa wameuawa.

"Vita vya Yemen lazima vifike mwisho," Rais Joe Biden amesema katika hotuba yake ya kwanza yenye mabadiliko makubwa ya sera za kigeni. .

Chini ya watangulizi wawili wa Bwana Biden, Marekani iliunga mkono muungano ulioongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen.

Mapigano hayo yamesababisha mamilioni ya raia wa yemen kukumbwa na baa la njaa.

Mapigano nchini humo yalianza mwaka 2014 kati ya serikali ya Yemen na vuguvugu la waasi wa Houthi.

Mwaka mmoja baadaye, vita hivyo viliendelea pale Saudi Arabia na mataifa manane ya kiarabu - yaliokuwa yanaungwa mkono na Marekani, Uingereza na Ufaransa - yalipoanza kutekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya Wahouthi.

Bwana Biden alitangaza mabadiliko mengine katika sera ya Marekani ya masuala ya nchi za nje, kama vile kuongezeka kwa idadi kubwa tu ya wakimbizi watakaokubaliwa kuingia Marekani, na kubatilishwa kwa uamuzi wa kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani ambako wamekuwa tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.

Hotuba yake inakinzana pakubwa na sera za mtangulizi wake Rais Donald Trump, ambaye muhula wake ulikamilika mwezi jana.

Tangazo la Yemen linamaanisha nini?

Marekani imekuwa ikiunga mkono serikali ya Yemen na washirika wa Saudi Arabia katika vita vyao dhidi ya Wahouthi.

Matokeo ya tangazo la Alhamisi, wanajeshi wa Marekani wataacha kuunga mkono operesheni za kivamizi ikiwemo uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Hili halitaathiri operesheni dhidi ya kundi la al-Qaeda katika rasi ya Arabia.

Utawala wa Biden tayari umesitisha kwa muda uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia na UAE.

Bwana Biden anatarajiwa kumtaja Tim Lenderking, kama mjumbe wake mpya nchini Yemen, mwanadiplomasia mwenye tajriba na mtaalamu wa Mashariki ya Kati.

Haya ni mabadiliko ikilinganishwa na utawala wa Trump ambao uliongeza kiwango cha kuunga mkono muungano wa Saudia.

Mwezi uliopita, waziri wa mambo ya nje chini ya utawala wa Trump, Mike Pompeo, alitangaza kwamba waasi wa Kihouthi wanatambuliwa kama kundi la kigaidi.

Alisema kuwa lengo lilikuwa ni kuwajibisha kundi la Houthi kwa mashambulizi yake mpakani na utekelezaji wake wa vitendo vibaya wakiwa wanaungwa mkono na Iran.

Mashirika ya kutoa msaada yalikosoa hatua hiyo, na kuonya kwamba kunaweza kuwazuia kutekeleza shughuli zao katika eneo hilo ambapo mamilioni ya raia wanahitaji msaada wa chakula kwa dharura.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa Yemen ni nchi iliyo katika mgogoro mbaya wa kibinadamu duniani huku asilimia 80 ya idadi ya watu wakihitaji msaada au ulinzi.

Biden alisema nini tena?

Marekani itaongeza idadi ya wakimbizi inayokubali kutoka 15,000 hadi 125,000 katika kipindi cha mwaka mmoja wa fedha.

Hatua ya kuondoa wanajeshi nchini Ujerumani itasitishwa na wanajeshi hao watasalia nchini humo kwa idadi yao ya sasa ambayo ni taktiban 36,000.

Chini ya utawala wa Trump, Marekani ilikuwa itapunguza uwepo wa wanajeshi wake nchini humo kwa 12,000 huku wanajeshi karibu 5,600 wakitarajiwa kupelekwa kwengineko Ulaya.

Pia, Bwana Biden ametoa wito kwa watawala wa kijeshi nchini Myanmar kumuachia huru kiongozi wa nchi hiyo Aung Suu Kyi na kurejesha demokrasia.

Na aliahidi kujadili suala la Urusi kwa njia ya diplomasia lakini atakuwa na msimamo mkali kwa Urusi kuliko Bwana Trump akisema kuwa Marekani haitayumba.