Maandamano ya wakulima: Fahamu kwanini ujumbe wa Twitter wa Rihanna ulizua hisia kali India

Muda wa kusoma: Dakika 4

Saa chache baada ya ujumbe wa Rihanna katika mtandao wa twitter kuzua hisia kali duniani baada ya kuwaunga mkono wakulima waliokuwa wakiandamana , serikali ya India ilimshutumu sana mwimbaji huyo wa Marekani.

Wizara ya masuala ya kigeni ilitoa taarifa rasmi ikiwakosoa watu maarufu na wengine kwa matamshi yao yasio sawa huku mawaziri na watu maarufu nchini humo nao wakalazimika kuchapisha jumbe dhidi ya propaganda ambayo inatishia umoja wa India.

Baadhi ya vyombo vya habari viliangazia sana taarifa hiyo ya serikali: Mmoja ya waigizaji wa kike wa Boollywood ambaye amekuwa akiunga mkono serikali alimuita Rihanna 'nyota wa ngono' na baadhi ya watu wakimuunga mkono mpenzi wake wa zamani Chris Brown kwa kumshambulia 2009.

Ujumbe wa Rihanna siku ya Jumanne unaohusishwa na habari moja kuhusu kuzimwa kwa mtandao katika eneo ambalo wakulima hao walikuwa wakiandamana na mara moja ukasambaa kwa haraka , ukipata likes 700,000.

Kwanini hatuzungumzi kuhusu hili? aliandika msanii huyo ambaye ana wafuasi milioni 100 duniani katika mtandao huo wa kijamii.

Hatua ya serikali kukabiliana na ujumbe huo ilikuwa ya haraka sana , ikiongozwa na waziri wa masuala ya ndani Amit Shah aliyetuma ujumbe wa twitter siku ya Jumatano usiku na neno #IndiaAgainstPropaganda and #IndiaTogether. "hakuna Propaganda zinazoweza kutishia Umoja wa India!

''Propaganda haziwezi kuamua hatma ya India .....ni maenedeleo pekee. India itaendelea kuwa na mshikamano na kwa pamoja itaafikia maendeleo'', aliandika.

Muda mfupi baadaye , mawaziri na nyota wa Bollywood na wachezaji kriketi pia walianza kutuma ujumbe katika twitter , wakitumia maeneo yaliotumiwa na bwana Shah.

Uhuru wa India hauwezi kuigiliwa. Nguvu za kutoka nje zinaweza kutazama lakini haziwezi kushiriki. India inawatambua Wahindi na wanapaswa kuiamulia India. Tusalie watu wamoja kama taifa , aliandika nyota wa Kriketi Sachin Tendulkar.

Maandamano hayo yamekuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi.

Makumi ya maelfu ya wakulima wamekuwa wakiandamana katika mipaka ya Delhi kupinga sheria tatu mpya za mashamba kwa zaidi ya miezi miwili.

Waandamanaji hao, wakiwemo wanaume wanawake, wazee na watoto , wamekataa katakata kusitisha maandamano hayo hata wakati wa majira ya baridi, wakipiga kambi katika maeneo yalio wazi, ambapo wamekuwa wakiishi na kulala barabarani. Wengi wao wakifariki.

Serikali imejitolea kusimamisha sheria hizo kwa miezi 18, lakini wakulima wanasema lazima zifutwe.

Wiki iliyopita, maandamano hayo yaligonga vichwa vya habari ulimwenguni wakati maandamano ya matingatinga ya wakulima yalipomalizika kwa mapigano makali, na kusababisha mwandamanaji mmoja kupoteza maisha yake huku mamia ya polisi na waandamanaji wakijeruhiwa.

Waandamanaji wengine walivamia jumba la kumbukumbu la Red Fort mjini Delhi na kusalia hapo hadi polisi walipowafukuza.

Huku Ujumbe wa Rihanna ukisambaa na kuvutia maelfu ya majibu , wengi walimpongeza kwa kuliangazia suala hilo muhimu. Lakini wengi pia walimkosoa kwa kuingilia maandamano ambayo ni kinyume na sheria ambayo imetetewa na serikali na wafuasi wake.

Vituo vingine vya habari vinavyounga mkono serikali vilikuwa na vichwa vya habari ambavyo vilimuelezea Rihanna kama "mgeni asiye na habari" ambaye alikuwa sehemu ya "njama ya kugawanya India" na kuapa kwamba "propaganda hazitashinda".

Mtangazaji mmoja wa habari - kwa kile kilichoonekana kama maoni ya Waislamu - aliuliza ikiwa mwimbaji huyo wa Barbadia aliitwa Rihanna au Rehana?

Waliokuwa wakimpinga walitoa picha za zamani za shambulio dhidi ya mwimbaji huyo na mpenzi wake wa zamani, wakimzidishia unyanyasaji dhidi yake.

Wengine walionyesha jinsi ambavyo wanaume wa India huamua kuwanyanyasa na kuwazima wanawake walio na maoni huru

Lakini moja ya pingamizi ya kushangaza dhidi ya mwimbaji huyo ilitoka kwa mwigizaji wa Kangana Ranaut, ambaye amekuwa akiunga mkono chama cha BJP.

Katika msururu wa jumbe zake za twitter, alikosoa kazi ya Rihanna, muziki wake, muonekano wake na hata rangi yake ya ngozi.

Alichapisha picha za nyota huyo wa pop akiwa amevalia vazi la bikini, na kumwita "nyota wa ponografia" na "mwimbaji wa ponografia", na akasisitiza kwamba alikuwa amelipwa kuandika ujumbe huo.

Lakini ujumbe wa Rihanna, ambao uliwaongezea sauti wakulima wanaoandamana, haungeweza kufikia serikali wakati mwafaka zaidi ya huo.

Wakulima hao wametangaza mipango ya kufunga barabara kuu zinazoingia mji mkuu Jumamosi na serikali inapeleka rasilimali nyingi kuwazuia.

Misumari ya chuma, fimbo, waya zenye miba, mawe na kuta za muda zimewekwa na mitaro kuchimbwa kwenye mipaka ya Delhi - huku wakulima na wakosoaji wakiishutumu serikali kwa kufanya maandalizi "kuwa vita" dhidi ya raia wake.

Mamlaka pia inajaribu kupigana vita dhidi ya muonekani wa India ughaibuni kuhusu jinsia inavyokabliana na wakulima wake.