Nchi za Afrika zina ufanisi kiasi gani katika mifumo ya kurekodi vifo?

Katika kipindi cha ugonjwa wa Ebola na sasa janga la Covid, kuwa na picha halisi ya nani anayepoteza maisha, kutokana na nini na wapi - ni muhimu linapokuja suala la matumizi ya rasilimali na fedha.

Wanasayansi wanasema bila kuwa na mifumo yenye ufanisi ya kurekodi data, wale wanaoathirika zaidi mara nyingi wanawake na watoto, kwasababu data zao hazifikii serikali ili kutatua changamoto zao kama kutoa huduma za afya ya uzazi na kuzuia magonjwa.

Uchunguzi wa BBC ukishirikiana na kituo cha takwimu katika Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi wa Afrika (UNECA) nchini Ethiopia , kukusanya na kutathimini takwimu za vifo kwa nchi 55.

Kati ya nchi 55 za Kiafrika , BBC imeangazia, nane pekee, Misri, Afrika Kusini na Tunisia, Algeria na visiwa vya Cape Verde, Sao Tome na Principe, Ushelisheli na Mauritius ambazo zilikuwa na mifumo ya usajili, wa raia ambao unarekodi vifo.

William Muhwava, mkuu wa takwimu za idadi ya watu na kijamii katika shirika UNECA lililo Addis Ababa, amesema kwamba "usajili wa raia ni haki ya kila mtu ya kutambuliwa".

Nchi zote ambazo tumechunguza zina usajili wa kifo wa aina fulani - mara nyingi kwenye karatasi na sio elektroniki. Inafanya kazi ndani - lakini haifai kuhesabu mwenendo wa vifo katika kiwango cha kitaifa.

Kuna watoto ambao huzaliwa na kuishi wakiwa hawajasajiliwana kutoka wakiwa hawajasajiliwa, bila kujulikana - kwa sababu ya ucheleweshaji wa kusajili vizazi na vifo "

Mifumo hii ya usajili ya CRVS, kwa kitaalamu Civil Registration and Vital Statistics systems hurekodi vizazi, ndoa na vifo.

Tathimini ya data ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa barani Ulaya, nchi zote isipokuwa mbili ( Albania na Monaco) wana mfumo wa usajili wa vifo kwa wote, na katika bara la Asia, zaidi ya nusu

"Tuna wasiwasi juu ya utimilifu na ubora wa usajili wa vifo [Afrika] kwa sababu watu wanaokosekana sio mfano wa idadi ya watu - wametengwa kwa sababu maalum ambazo mara nyingi zinahusiana na shida za kijamii, kiuchumi, na kiafya," Romesh Silva, mwandamizi mtaalam wa idadi ya watu katika Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) aliiambia BBC.

"Ili kusaidia walio hai, tunahitaji kuhesabu waliokufa… tunahitaji kufanya juhudi za kusajili vifo vya watu ambao hawaonekani sana na mifumo ya takwimu za kiafya."

Wanasayansi wanasema kwamba data hufanya usawa uonekane na kwamba katika nchi nyingi za Kiafrika, takwimu zinapendelea zaidi watu wenye kipato zaidi, wakazi wa miji, na wanaume.

"Mifumo ya CRVS katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara haiwezi kutoa takwimu muhimu zilizoainishwa kwa jinsia, umri na jiografia, ambayo ni muhimu kwa utengenezaji wa sera, "anasema Irina Dincu, kutoka Kituo cha Ubora cha Mifumo ya CRVS.

"Licha ya uwekezaji, mifumo ya CRVS bado haifanyi kazi, ikilazimisha serikali kutegemea tafiti ... ambazo wakati zinapochapishwa tayari zimepitwa na wakati."

Hii inamaanisha kuwa vikundi vilivyo katika mazingira magumu vinateseka zaidi kwa sababu, data zao hazipatiwi sera.

Tathimini ya athari za Covid-19

Imeripotiwa sana kuwa idadi ya vifo vya Afrika kutokana na Covid-19 iko chini sana kuliko sehemu nyingine za ulimwengu.

Wengi wanakubali kwamba Afrika imeshughulikia vyema janga hilo, lakini wanasayansi wanasema kuwa kuhesabu "idadi kubwa ya vifo" barani ni vigumu katika nchi nyingi kwa sababu ya ukosefu wa CRVS.

Vifo vya ziada ni hatua ambayo inalinganisha vifo halisi katika kipindi fulani na vifo vinavyotarajiwa, kulingana na kipindi hicho katika miaka iliyopita.

Njia hiyo inategemea kabisa mfumo kamili wa usajili wa vifo.

Athari zisizo za moja kwa moja kutokana na Covid zinaweza kuwa mbaya zaidi kuliko ugonjwa wenyewe

Kwa kutazama vifo vilivyoshuhudiwa kunatoa hisia ya upotezaji wa maisha uliosababishwa moja kwa moja na Covid-19, na pia vifo vilivyosababishwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja na janga hilo kwa sababu ya mifumo ya afya iliyozidiwa, hofu ya kuhudhuria hospitali na kuanguka kwa uchumi.

Utafiti wa Lancet katika nchi 118 za kipato cha chini na kipato cha kati unakadiria kuwa changamoto katika mifumoya afya kutokana Covid-19 inaweza kusababisha vifo vya watoto zaidi ya 1,157,000 na vifo vya akina mama 56,700.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa, kama ilivyo katika tathimini ya mlipuko wa Ebola wa 2014 huko Afrika Magharibi, athari zisizo za moja kwa moja za mlipuko zinaweza kuwa kali zaidi kuliko mlipuko wenyewe.

Afrika Kusini na Misri ni kati ya nchi nane ambazo zina sajili kamili za vifo, kwa hivyo kuhesabu vifo vya ziada katika nchi zote mbili kunawezekana, na matokeo yanaelezea.

Afrika Kusini kulikuwa na karibu vifo vya ziada vya 60,000 mwanzoni mwa mwezi Desemba - hiyo ni karibu mara tatu ya takwimu rasmi ya Covid.

Kwa hivyo inamaanisha watu 23,600 walipoteza maisha kutokana na Covid na kuna vyeti vya vifo kuthibitisha.

Hii inamaanisha kuwa wengine 37,300 hawakugunduliwa, au walikufa kama matokeo ya moja kwa moja ya janga kama vile kucheleweshwa kwa matibabu ya saratani au hofu ya kwenda hospitalini.

Takribani nchi 14 zinarekodi moja tu kati ya vifo 10 au chini ya hapo.

Zaidi ya nusu ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara huweka kumbukumbu za kifo zilizoandikwa kwa mkono tu.

Nchi nyingine, kama Eritrea na Burundi hazina sharti la kisheria la kusajili au kurekodi vifo Eritrea imerekodi kifo kimoja tu cha Covid-19 hadi sasa na Burundi, ni viwili tu, ingawa kuna uvumi kwamba Covid-19 ilikuwa sababu ya kuchangia kifo cha ghafla cha Rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurinziza mwaka jana.

Nigeria ilirekodi tu 10% ya vifo mnamo 2017. Janga hilo lilizidi "kupooza shughuli zote za usajili wa raia" nchini, ambazo hazikuonekana kuwa huduma muhimu. Hii inaweza kuelezea kwa nini idadi ya vifo vya Covid kwa kila watu milioni bado ni ndogo - saba kwa milioni, ikilinganishwa na 579 nchini Afrika Kusini na 81 nchini Misri. Wastani wa ulimwengu leo ​​ni vifo 252 kwa milioni.

Kitu gani kinafanyika?

Nchi nyingi zinafanya maendeleo katika kuziba pengo la data.

Pamoja na Senegal, Rwanda kwa sasa inafanya kazi ya kuweka data ya kihistoria ya vifo ambayo inaweza kulinganishwa na vifo wakati wa janga - kwa kutumia njia inayoitwa ufuatiliaji wa vifo vya haraka. Nchi nyingine tano - Togo, Burkina Faso, Sierra Leone, Liberia na Ghana.

Chad na Liberia zinawataka wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii kutoa taarifa kuhusu vifo vinavyotokea nyumbani mbali na hospitali kusaidia kuangazia kiwango cha vifo vya jamii. Wanatumia uchunguzi wa mwili - kuhoji jamaa wa karibu kuhusu aliyekufa - suluhisho la gharama nafuu kuelewa sababu kuu za vifo katika eneo fulani.

Nchi nyingine zinatumia teknolojia ya simu ya kiganjani kukusanya, kusimamia na kuhifadhi data za vifo. Nchini Rwanda na Msumbiji, watu wanaweza kutumia simu za mkononi kusajili vifo kwenye mfumo wa kielektroniki, ikiruhusu jamaa kuripoti vifo.

Nchini Uganda, Ofisi ya Usajili wa Kiraia imeanzisha Mfumo wa Kumbukumbu za Vital za rununu (MVRS) ambao hutoa taarifa mtandaoni.

Katika muongo mmoja ujao, wanasayansi wana matumaini aina hii ya uvumbuzi itasaidia nchi zaidi barani kufikia malengo yao ya usajili wa vifo kwa wote.