Al-Qaeda: Pompeo anasema Iran ni 'kambi mpya' ya mtandao wa magaidi

Muda wa kusoma: Dakika 3

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ameilaumu hadharani serikali ya Iran kwa kuruhusu mtandao wa kijihadi wa al-Qaeda kubuni "makao mapya makuu " nchini humo.

"Tofauti na Afghanistan, ambako al-Qaeda ilikuwa inajificha milimani, leo hii kundi la al-Qaeda linafanya kazi chini ya ulinzi wa utawala wa Iran," aliambia shirika la wanahabari la National Press Club.

Bw. Pompeo hakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alitaja madai hayo kuwa "uwongo wa kuchochea vita".

Mwezi Novemba mwaka jana, Iran ilipinga ripoti kwamba naibu wa kamanda wa al-Qaeda Abdullah Ahmed Abdullah, anayefahamika pia kwa jina la Abu Muhammad al-Masri, alipigwa risasi na kuuawa mjini Tehran na maajenti wa Israeli, kufuatia ombi la Marekani.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington siku ya Jumanne, Bw. Pompeo alisema anaweza kuthibitisha kwa mara ya kwanza kwamba Masri alifariki Agosti 7, japo hakutoa maelezo zaidi.

Alisisiza kwamba ni makosa kuamini uongozi wa madhehebu ya Waislamu wa Kishia (Iran) na Kikundi cha Sunni ambacho kinachukulia Washia kuwa wazushi na maadui wakubwa.

"Uwepo wa Masri ndani ya Iran unaashiria sababu ya kwanini tuko hapa leo. Al-Qaeda imepata makao mapya : Ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

"Kutokana na hilo, kundi baya lililobuniwa na [Osama] Bin Laden linaelekea kupata nguvu na uwezo."

Tangu mwaka 2015, Bw. Pompeo amekuwa akidai kwamba, Tehran imeruhusu viongozi wa al-Qaeda nchini humo kuwa huru kuwasiliana na wanachama wengine na kutekeleza majukumu mengine ambayo yalikuwa yakiendeshwa kutoka Afghanistan na Pakistan, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha mashambulio, propaganda, na kuchangisha fedha.

"Uwepo wa al-Qaeda ndani ya Iran unatishia usalama wa mataifa na hata ndani Marekani kwenyewe," aliongeza.

Waziri huyo wa Mambo ya nje pia alisema Marekani ilikusudia kutoa hadhi ya Magaidi Maalum Walioteuliwa Ulimwenguni kwa viongozi wawili wa al-Qaeda ambao iliamini kuwa walikuwa nchini Iran: Mohammed Abbatay, ambaye pia anafahamika kama Abdul Rahman al-Maghrebi, na Sultan Youssef Hassan al-Arif.

Marekani pia itatoa zawadi ya hadi dola milioni saba sawa na (£5.1m) kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kufahamu mahali alipo Maghrebi au kumtambua.

Zawadi pia tayari imetolewa kuwata viongozi wawili wa ngazi ya juu wa al-Qaeda wanaodai kuwa nchini Iran - Saif al-Adel na Yasin al-Suri.

Wanamgambo kadhaa wa al-Qaeda na familia ya Osama Bin Laden walikimbilia Iran baada ya Marekani kuvamia kijeshi Afghanistan mwaka 2001. Maafisa wa Iran walidai kwamba waliovuka mpaka walikamatwa na kurudishwa makwao.

Baada ya taarifa za kuuawa kwa Masri kuibuka mwaka uliopita Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisisitiza kwamba hakuna "magaidi" wa al-Qaeda katika ardhi yake.

Na siku ya Jumanne, msemaji wake aliambia kituo cha habari cha kitaifa: "Iran imekuwa mhasiriwa wa ugaidi wa serikali ya Marekani na washirika wake kwa miaka mingi na imekuwa na rekodi ya wazi katika vita dhidi ya al Qaeda na Islamic State."

Shirika la habari la Reuters limemnukuu afisa wa zamani wa Marekani wa masuala ya intelijensia akisema mamlaka nchini Iran haikuwa na uhusiano na al-Qaeda kabla au baada ya shambulio la kigaidi la 9/11, na kwamba "madai yoyote ya ushirikiano wa asa unatiliwa shaka".

Wachambuzi pia wamehoji muda ambao Bw. Pompeo ametoa tangazo lake, wakisema anaonekana kana kwamba anajaribu kufanya iwe vigumu kwa Rais Mteule Joe Biden kushauriana tena na Iran na kuishawishi ijiunge tena na mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.