Mzozo wa Ethiopia: Hati ya kuwakamata maofisa wa kijeshi yatolewa,mapigano yaendelea Tigray

Ethiopia imetoa hati ya kukamatwa kwanza maafisa 76 wa kijeshi wanaotuhumiwa kushirikiana na chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).

Vikosi vitiifu kwa chama hicho vinapigana na serikali katika jimbo la Tigray .

Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema majeshi yake yanaelekea mji mkuu, Mekelle.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa na maelfu wengine kutoroka eneo hilo baada ya wiki mbili za makabiliano.

Kuthibitisha hali ilivyo katika Jimbo la Tigray ni vigumu kwasababu huduma za mawasiliano zimekatizwa.

Mzozo huo umetokana na taharuki ya muda mrefu kati ya chama kikuu cha siasa katika eneo hilo,Tigray People's Liberation Front (TPLF) na serikali kuu ya Ethiopia.

Wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipohirisha uchaguzi kutokana na janga la corona, hali ya taharuki ilipanda kati ya pande hizo mbili. TPLF inachukulia serikali kuu ni batili ikadai kuwa Bwana Abiy hana mamlaka ya kuendelea kuongoza nchi.

Serikali inalaumu TPLF kwa kushambulia kambi ya majeshi kwa lengo la kuiba silaha, madai ambayo TPLF imepinga. Bwana Abiy alijibu madai hayo akisema kitendo hicho ni uhaini.

Ni yapi yanayojiri kwa sasa?

Siku ya Jumatano mamlaka za polisi katika serikali kuu zilitoa hati ya kukamatwa kwa maafisa 76 wa kijeshi, baadhi yao wanadaiwa kustaafu. Wanatuhumiwa kushirikiana na TPLF "kutekeleza uhaini", kwa mujibu wa shirika la AFP .

Akizungumza na BBC, Billene Seyoum - msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed - alipinga madai kwamba watu kutoka jamii yaTigrinya katika maeneo mengine nchini wanakamatwa kwa misingi ya kikabila.

Lakini amekiri kuwa watu kadhaa wanazuiliwa kwa kuwa wanachama wa kile alichokiita mtandao wa uhalifu.

Taarifa hizo zinakuja baada ya vikosi vya serikali kuteka miji ya Shire na Axum baada ya makataa ya siku tatu iliyotolewa na Waziri Mkuu Abiy kwa vikosi vya Tigray kujisalimisha kuisha siku ya Jumanne.

Kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael, ambaye ni mzaliwa wa Shire, amethibitisha katika televisheni moja jimboni humo kwamba wanajeshi wake wamepoteza udhibiti wa miji ya Kusini na Magharibi mwa Tigray. Hatahivyo alitaja ushindi Abiy.

Sudan inasema watu 36,000 wameingia nchini humo kupitia mpaka wa Tigray wakati mapigano yakiendelea.

Umoja wa Mataifa umeonya kutokea kwa "mzozo kamili wa kibinadamu".

"Huenda kukawa na watu wengi waliokimbia makazi yao ndani ya Tigray hali ambayo inastahili kuangaziwa wakati tunapojiandaa kuwasaidia kadiri ya uwezo wetu," Jens Lark msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulia masuala ya kibinadamu (OCHA), amesema.

Umoja wa Mataifa unahofia idadi ya watu wanaotoroka mapigano Ethiopia huenda ni sehemu kidogo ya watu waliolazimika kutoroka makwao kutokana na ghasia, lakini kwa sasa mashirika ya kutoa misaada hayawezi kufika jimbo la Tigray.

Nchi zilizo na ushawishi wa kikanda kama vile Kenya na Uganda zimetoa wito wa majadiliano ya amani kusuluhisha mzozo huo. Serikali ya Ethiopia imefutilia mbali uwezekano wa kufanya mazungumzo na TPLF.

Mambo matano kuhusu Tigray:

1. Ufalme wa Aksum uko katika eneo hilo. Ilielezewa kama moja ya ustaarabu mkubwa wa ulimwengu wa zamani, wakati mmoja ilikuwa serikali yenye nguvu kati ya milki za Kirumi na Uajemi.

2. Magofu ya mii wa Aksum yametambuliwa na Umoja wa Mataifa kama eneo la turathi za kale duniani. Eneo hilo ambalo limekuwepo kati ya karne ya kwanza hadi ya tatu AD, linajumuisha , makasri, makaburi ya wafalme na kanisa linaloaminiwa na baadhi ya watu kuwa sanduku la agano (Ark of the Covenant).

3. Watu wengi katika eneo la Tigray ni Wakristo wa dhehebu la Orthodox Ethiopia. Mzizi wa Dini ya Kikristo ulianza kuchipuka miaka 1,600 iliyopita.

4. Lugha kuu katika eneo hilo ni Tigrinya, lahaja ya Kisemeti ina wasemaji wasiopungua milioni saba ulimwenguni.

5. Ufuta ni zao kuu la biashara, unasafirishwa Marekani, China na nchi nyingine.