Hong Kong: China yawakamata watu 10 baada ya kulizuia boti lililokuwa likitoroka Hong Kong

kamishna wa polisi mjini Hong Kong Hong

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, kamishna wa polisi mjini Hong Kong Hong

Mamlaka nchini China imewakamata takriban watu 10 baada ya kuzuia boti inayoaminika ilikuwa inaelekea Taiwan kutoka Hong Kong kulingana na ripoti.

Walinzi wa pwani ya China wamesema kuwa ukamataji huo ulifanyika siku ya Jumapili alfajiri katika mkoa wa kusini wa Guangdong, karibu na Hong Kong.

Vyombo vya habari mjini Hong Kong vilisema kwamba wale waliokuwa wakiabiri chombo hicho walikuwa wakijaribu kuingia Taiwan ili kuchukua hifadhi ya kisiasa.

Ripoti hiyo imesema kwamba mwanaharakati wa Hong Kong Andy Li alikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa .

Bwana Li , ambaye alikamatwa mapema mwezi huu kwa madai ya kujihusisha na viongozi wa mataifa ya kigeni na utapeli wa fedha , alikamatwa kwa tuhuma za kuvuka mpaka bila kufuata sheria kulingana na gazeti la kusini mwa China la Morning Post likinukuu vyanzo tofauti.

Haijulikani waliokamatwa watafunguliwa mashtaka gani.

Majaribio ya watu Hong Kong kutoroka eneo hilo kwa kutumia boti sio ya kawaida.

Hong Kong imeripoti wimbi la ukamataji wa wanaharakati katika majuma ya hivi karibuni kwa madai ya kukiuka sheria yenye utata iliowekwa mwezi Juni nchini China.

Sheria hiyo ya usalama inayopingwa na wengi Hong Kong , inaadhibu kile ambacho Beijing inakitaja kuwa ubatili, kujitenga, ugaidi na kutumika na viongozi wa mataifa ya kigeni.

Ripoti hiyo imesema kwamba mwanaharakati wa Hong Kong Andy Li alikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa
Maelezo ya picha, Ripoti hiyo imesema kwamba mwanaharakati wa Hong Kong Andy Li alikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa

Idadi ya watu waliokamatwa imezua hofu kwamba China itatumia sheria yake ya usalama kufanya msako mkubwa dhidi ya wanaharakati wa Hongkong na wanahabari.

HongKong ilikabidhiwa kwa China na Uingereza iliokuwa ikiidhibiti 1997.

Lakini chini ya makubaliano yasio ya kawaida ni taifa moja lenye mifumo miwili inayolipatia jimbo hilo uhuru usioonekana nchini China.

Lakini wakosoaji wameishutumu China kwa kufuta uhuru huo, hali inayosababisha maandamano mjini Hong Kong na wasiwasi wa kisiasa kati ya Beijing na jamii ya kimataifa .

Je tunajua nini kuhusu kamata kamata inayoendelea?

Chapisho moja la mtandao wa kijamii lililowekwa na walinzi wa pwani wa Guandong siku ya Jumatano lilisema kwamba wale waliokamatwa walikuwa wanazuiliwa kwa tuhuma za kuvuka mpaka.

Limesema kwamba uchunguzi unaendelea , lakini likatoa maelezo machache. Ni wawili kati ya wale wanaozuiliwa walitambulika kwa majina yao Li na Tang.

Gazeti la China la Morning post limesema kwamba vyanzo vya polisi mjini Hong Kong na China vilithibitisha kwamba Andy Li ndie Li aliyekuwa akitajwa.

Mtu zaidi aliyekuwa ameabiri chombo hicho alikuwa amekamatwa na mashtaka yanayohusiana na maandamano dhidi ya serikali yaliofanyika mwaka jana , gazeti hilo lilisema.

Kamishna wa polisi wa Hong Kong Chris Tang alisema siku ya Alhamisi kwamba alikuwa anafahamu kuhusu kuzuiliwa kwa boti hilo , lakini akaongezea: Kwa sasa hatuna habari kutoka kwa mamlaka husika .

Je jukumu la Taiwan ni lipi katika kisa hiki?

Taiwan, kisiwa kinachojitawala kilichopo kusini mashariki mwa pwani ya China kimejaribu kuwasaidia raia wa Hong Kong walio na hofu ya msako wa kisiasa unaofanywa na Beijing.

Mwezi Julaii, Taiwan ilifungua ofisi ili kuwawezesha watu wa Hong Kong kuhamia kisiwani humo. Ofisi hiyo ilipokea zaidi ya maombi 1,000 katika kipindi cha mwezi mmoja pekee .

Taiwan imekuwa uhuru tangu 1950 lakini China inakichukulia kisiwa hicho kuwa jimbo lililojitenga na kwamba linapaswa kujiunga na China bara kwa lazima iwepo italazimika.

Hatua hiyo imesababisha mgogoro wa kisiasa huku rais wa Taiwan Tsai Ing-wen akilaumu China kwa kujaribu kukilazimisha kisiwa hicho kuwa chini ya himaya yake.