Alex Navalny: Hana fahamu baada ya 'kuwekewa sumu' kwenye chai

Alexei Navalny ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa Rais Vladimir Putin

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwanasiasa wa upinzani Alexei Navalny hana fahamu akiwa hospitalini kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa ameathirika na sumu, msemaji wake ameeleza.

Mpiga kampeni dhidi ya vitendo vya rushwa alianza kujisikia mgonjwa alipokuwa safarini kwenye ndege, hali iliyofanya ndege aliyokuwa akisafiri nayo kutua kwa dharura mjini Omsk, ambapo madaktari walisema kuwa alikuwa hana fahamu na walikuwa wakijaribu kuokoa maisha yake.

Timu yake inashuku kuwa kuna kitu kiliwekwa kwenye chai katika mgahawa wa uwanja wa ndege .

Ikulu ya Urusi imesema inamtakia ''afya njema na ya haraka bwana Navalny''

Bwana Navalny, 44, kwa miaka mingi amekuwa mmoja kati ya wakosoaji wakubwa wa Vladimir Putin.

Mwezi Juni alieleza kuwa kura ya mabadiliko ya katiba ni ''mapinduzi'' na ''ukiukaji wa katiba''. Mabadiliko yanampa fursa Putin kuongoza tena mihula miwili, baada ya minne aliyokuwa nayo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Dominic Raab amesema kuwa ''amesikitishwa sana'' na ripoti kuwa alikuwa amepewa sumu, na kutuma salamu za pole kwake na familia yake.

Taasisi ya German Peace ina matumaini ya kutuma ndege ya kusafirisha wagonjwa ili kumchukua Navalny kuelekea Berlin kwa ajili ya matibabu.

Hospitali ya Charite mjini Berlin iko tayari kumtibu, Jaka Bizilj , Mkurugenzi wa mfuko huo ameeleza.

''Tuko kwenye mazungumzo na mamlaka na kuna matumaini kuwa vibali vyote vya usafiri na ripoti za kitabibu zitapatikana usiku huu.'' aliongeza.

Mkutano wa watu walioonesha kumuunga mkono Bwana Navalny ambaye amepoteza fahamu

Chanzo cha picha, Getty Images

Msemaji wake amesema nini?

Kira Yarmysh, afisa habari wa mfuko wa kupambana na rushwa, ambao ulianzishwa na Bwana Navalny mwaka 2011, aliandika katika ukurasa wa Twitter kuwa:

''Asubuhi hii Navalny alikuwa akirejea mjini Moscow akitokea Tosmk.

''Wakati akiwa safarini alijihisi mgonjwa. Ndege ililazimika kutua kwa dharura mjini Osmk. Alexei amepewa sumu.''

Aliongeza: ''Tunashuku kuwa Alexei ameathirika na kitu ambacho kilichanganywa kwenye chai yake. Ndicho kitu pekee alichokunywa tangu asubuhi.

''Madaktari wanasema kuwa sumu hiyo inayeyuka haraka sana kwenye kimiminika cha moto. Na sasa Alexei hana fahamu.''

Bi Yarmysh amesema kuwa baadae Bwana Navalny aliwekwa kwenye mashine ya msaada wa kupumua huku akiwa hana fahamu, na kwamba maafisa wa polisi wako kwenye hospitali hiyo.

Vitu vyake vyote vimezuiliwa, aliongeza.

Picha ya video ikimuonesha Navalny akiingizwa kwenye gari la kubeba wagonjwa

Chanzo cha picha, EPA

Alisema pia madaktari awali walikuwa tayari kutoa taarifa yoyote lakini baadae walidai kuwa vipimo vimechelewa na hivyo ''Ni wazi walikuwa hawasemi kile wanachokijua''.

Uchunguzi utakuwa ''jioni nzima'', aliambiwa.

Mke wa Navalny, Yulia Navalnaya, na daktari, Anastasia Vasilyva, wamewasili hospitalini.

Mke wake awali alikataliwa kuingia ili kumuona Navalny kwasababu mamlaka zilisema kuwa mgonjwa hakukubali kutembelewa, alisema Bi Yarmysh, ingawa baadae aliruhusiwa kuingia wodini.

Dkt Vasilyeva alisema kuwa walikuwa wakitafuta uhamisho wa mgonjwa kwenda kwenye kituo maalumu cha tiba dhidi ya sumu barani Ulaya, lakini madaktari wa hospitali hiyo walikuwa wakikataa kutoa rekodi kuhusu afya yake.

Ripoti nyingine kutoka eneo la tukio

Shirika la habari nchini humo Tass lilinukuu chanzo kimoja katika hospitalli ya Omsk akisema: '' Alexei Anatolyevich aliyezaliwa 1976. Ana sumu yuko chumba cha wagonjwa mahututi.''

Hatahivyo, mganga mkuu wa hospitali hiyo baadae aliviambia vyombo vya habari kuwa hakuna uhakika kuwa Bwana Navalny alipewa sumu, ingawa moja ya vipimo vimeonesha ni sumu.

Anatoly Kalinichenko amesema kuwa ''madaktari walikuwa kweli wakijaribu kuokoa maisha ya Navalny''.

Msemaji wa ikulu Dmitry Peskov baadae alisema kuwa wanamtakia afya njema-na kuwa mamlaka itaangalia suala la kuidhinisha matibabu nje ya nchi ikiwa itaombwa kufanya hivyo.

Picha ya video kwenye mitandao ya kijamii imemuonesha navalny akiwa kwenye kiti cha magurudumu akipelekwa kwenye gari ya kubeba wagonjwa aliposhuka kwenye ndege.

Video nyingine ilionesha namna alivyokuwa akiugulia maumivu alipokuwa kwenye ndege

Abiria mmoja Pavel Lebedev alisema kuwa ; ''safari ilipoanza alikwenda msalani na hakurejea. Alianza kujisikia kuumwa sana.Walihangaika kumrudisha na alikuwa akipiga kelele kwa maumivu.''

Picha nyingine kwenye mtandao wa kijamii imemuonesha Bwana Navalny akinywa chai katika mgahawa wa uwanja wa ndege Tomsk.

Imeelezwa kuwa wamiliki wa mgahawa wanaangalia picha za CCTV ili kuona kama zinaweza kutoa ushahidi wowote.

Mke wa Navalny, Yulia Navalnaya yuko hospitalini, lakini awali alizuiwa kumuona mumewe

Chanzo cha picha, EPA

Alexei Navalny ni nani?

Alijipatia jina kwa kufichua vitendo vya rushwa akikita chama cha bwana Putin cha United Russia kuwa ''chama cha wezi na wahalifu'', na alitumikia vifungo kadhaa gerezani.

Mwaka 2011 alikamatwa na kufungwa kwa siku 15 baada ya maandamano yaliyodai kuwepo kwa vitendo vya wizi wa kura vilivyodaiwa kufanywa na chama tawala katika kura za ubunge.

Bwana Navalny alitumikia kifungo mwezi Julai mwaka 2013 kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha lakini alisema kuwa hukumu hiyo ilichochewa kisiasa.

Alijaribu kusimama kuwania nafasi ya urais mwaka 2018 lakini alizuiwa kwa kuwa alikuwa tayari amehukumiwa kifungo .

Bwana Navalny alifungwa siku 30 gerezani mwezi Julai mwaka 2019 kwa kosa la kuitisha maandamano ambayo yalikuwa batili.

Navalny alikamatwa mara kadhaa miaka ya hivi karibuni wakati wa maandamano yaliyopigwa marufuku

Chanzo cha picha, AFP

Mashambulio dhidi ya wakosoaji

Ikiwa itathibitishwa kuwa alipewa sumu, atakuwa mmoja kati ya wanasiasa maarufu wakosoaji wa Rais Putin ambao wamekutwa na mashambulizi.

Miongoni mwao mwanasiasa Boris Nemtsov na mwanahabari Anna Politkovskaya, ambao walipigwa risasi hadi umauti, na afisa wa intelijensia Alexander Litvinenko, aliyeuawa kwa sumu nchini Uingereza.

Mwanahabari na mwanaharakati Vladimir Kara- Murza bado yuko hai, lakini alidai kuwa alipata mashambulizi ya sumu mara mbili na vikosi vya usalama vya Urusi.

Karibu apoteze maisha baada ya figo kushindwa kufanya kazi mwaka 2015 na kisha hakuwa na fahamu miaka miwili baadae.

Mkosoaji mwingine, Pyotr Verzilov, alivishutumu vikosi vya usalama vya Urusi kwa kumuwekea sumu mwaka 2018, wakati alipoanza kuumwa baada ya kusikilizwa kwa kesi, alipoteza uwezo wa kuona na kuzungumza.

Mwaka huohuo, afisa wa zamani Sergei Skripal na binti yake walipewa sumu nchini Uingereza.

Uingereza inaamini kuwa maafisa wa Urusi wamehusika na shambulio hilo, lakini Ikulu ya Urusi mara zote imekuwa ikikana kuhusika.