Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Tanzania 2020: Polisi wapiga marufuku mikusanyiko ya kumpokea Lissu
Jeshi la polisi nchini Tanzania limetoa tamko la kuzuia mikusanyiko wa watu siku ya Jumatatu ya Julai 27, hatua hiyo inakuja baada ya viongozi mbalimbali wa chama cha siasa cha Chadema kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenda kumpokea mwanasiasa wa chama hicho Tundu Lissu.
Jeshi la polisi limesema sasa taifa lipo katika kipindi cha maombolezo ya kitaifa hivyo vyombo vya dola vinapaswa kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inakuepo katika kipindi chote cha maombolezo.
Kupitia ukurasa wa Chadema wa mtandao wa Twitter wameandika ujumbe wa kwenda kumpokea Lissu, "Tunakwenda kumpokea @TunduALissu
kwa sababu ni Kiongozi wetu, hakwenda Ubelgiji kutalii, kwa sisi tuliyemuona usingeweza kuamini kama angeendelea kuwa hai saa mbili mbele, mwili haukuwa umetobolewa tu, ulikuwa umefumuliwa, mimi ni kati ya watu wachache waliomuona" Benson Kigaila.
Jeshi la Polisi liliongeza kusema kuwa kurejea kwa kiongozi huyo ni haki yake kama ilivyo kwa watanzania wengine ,kwa sababu nchi hiyo ni salama kwa watanzania na wageni pia.
Aidha Jeshi hilo limesema litafuatilia kuona kama kuna kibali chochote kilitolewa ili kuruhusu mikusanyiko ya watu kisheria.
Lissu alizungumza na Watanzania kwa njia ya mtandao akiwa ughaibuni, kuhusu safari yake ya Tanzania hivi karibuni na akieleza wasiwasi alionao kuhusu usalama wake.
''Wale waliokuja kuniua hiyo siku ya tarehe saba Septemba miaka mitatu iliyopita na waliowatuma au waliowalipa au waliowaelekeza bado wanaitwa watu wasiojulikana, maana yake ni kwamba hao watu bado wapo na kwa sababu bado wapo na hawajasema kama lengo lao la kuniua wameliacha, bado kuna hatari juu ya maisha yangu.''
''Kwa hiyo ninarudi nchini kwangu katika mazingira ambayo hatari dhidi yangu haijaondoka bado. Lakini ninarudi tu, ni nyumbani kwetu, inabidi nirudi," amesema.
Kwa mujibu wa Lissu, katika miezi sita iliyopita, uongozi Mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe aliandika barua mbili kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, ili kuomba apatiwe ulinzi atakaporudi.
Amesema hadi sasa wanasubiri majibu ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao ndio wenye jukumu la kuhakikisha kuwa yuko salama atakaporejea nchini humo.
Hata hivyo, Lissu amedai kuwa: ''Hata kutujibu barua tu kusema kuwa tumepokea barua yenu tunaifikiria, hawajafanya hivyo."
"Naomba niseme hili kwa ajili ya kumbukumbu, mimi sina na siwezi kuwa na jeshi binafsi la kunilinda, sina na siwezi kuwa na rafiki au taasisi au nchi
itakayotoa jeshi la kunilinda mimi nitakapokuwa nyumbani, wajibu wa kunilinda mimi kwa mujibu wa katiba na sheria za Tanzania ni wajibu wa jeshi la polisi la Tanzania.''
Toka aliposhambuliwa kwa risasi jijini Dodoma mwaka 2017, Lissu amekuwa akiituhumu serikali ya Tanzania juu ya tukio hilo japo serikali imekanusha vikali madai hayo.
Lissu anatarajiwa kurejea Julai 28 akiwa mmoja wa wanaoomba kuteuliwa na chama chake cha CHADEMA, kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema nini kuhusu kesi zinazomkabili?
Kuhusu kesi mbalimbali zinazomkabili katika mahakama ya hakimu mkazi ya kisutu, Lissu amesema '' nimeulizwa ulizwa sana na nimetishwa tishwa sana kwamba nikirudi nitakamatwa aidha kwa kesi ambazo zipo au pengine nitafunguliwa kesi nyingine.''
Lissu amesema kuwa ana kesi za jinai sita katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kesi zote hizo Lissu amedai zinahusu ''maneno au kauli ambazo amezitoa ambazo zinakosoa au kuipinga au kutokukubaliana na sera, matendo au mipango ya serikali ya Tanzania''.
''Yote ambayo nimeyasema na ambayo nashtakiwa kwayo si makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania''.
Amesema katika kesi hizo zote sita zilizoko mahakamani, alikuwa nje kwa dhamana ya mahakama na hajawahi kukimbia au kuruka dhamana hiyo.
Lissu amesema Mahakama inafahamu sababu na mazingira yaliyomfanya aondolewe nchini na ambayo yamemfanya abaki nje ya nchi hadi sasa.
''Na ndio maana katika kipindi chote hiki,katika kesi zote hizo sita, mahakama haijafuta dhamana katika kesi hata moja, kati ya hizo sita kwa sababu inaelewa sababu na mazingira ya kuondoka kwangu na kubaki kwangu nje ya nchi''.
''Kwahiyo ninarudi si kama mfungwa aliyekimbia dhamana, ninarudi sio kama muhalifu aliyefutiwa dhamana, ninarudi kama raia huru ambaye kwa mujibu wa sheria na katiba za Tanzania anahesabika kuwa huru na kuwa hana hatia hadi hapo mahakama itakapoamua vinginevyo''.
''Ninarudi kama raia huru wa Tanzania asiyekuwa na kosa lolote au jinai yoyote," amesema Lissu.