Teknolojia ya intaneti inayowezeshwa kwa kutumia vibofu yaanza Kenya

Chanzo cha picha, Loon
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
Teknolojia ya intaneti inayowezeshwa kwa maputo kutoka kwa kampuni dada ya mawasiliano ya Google inayofahamika kama Loon imezinduliwa rasmi nchini Kenya na itawezesha upatikanaji wa mtandao katika maeneo ya vijijini.
Teknolojia hiyo itatoa huduma ya mawasiliano ya 4G ili watu waweze kupiga simu kwa njia ya kawaida ama video, kuingia kwenye mitandao ya kijamii, kutuma ujumbe mfupi na hata mawasiliano ya moja kwa moja.
Mradi huo ambao ulitangazwa miaka miwili iliopita sasa hivi ndio serikali ya Kenya imefanikiwa kupata idhini ya kuuanzisha.
Teknolojia hii inafanya vipi kazi?
Hii ni teknolojia mpya na ni mara ya kwanza kutumika duniani kote. Ni teknolojia inayotumia maputo yanayopepea angani kilomita 20 kutoka usawa wa bahari na ndani ya maputo hayo kuna vifaa ambavyo vina uwezo wa kuwasiliana na vifaa vya kampuni ya mawasiliano ya Telkom Kenya chini ya ardhi.
Teknolojia hii bado inafanyiwa maboresho lakini imefikia kiwango ambacho raia wa Kenya wanaweza kunufaika nayo.
Ili mtu aweze kutumia huduma hii ni lazima awe na simu na laini ya kampuni yenye huduma ya intaneti ya 4G au LTE.
''Maputo haya yanaendeshwa na nguvu ya jua, na ni kama maputo ya kawaida yaani kwanza ni lazima yapandishwe juu mfano wake ni kufurisha puto la kawaida'', amesema mkuu wa kampuni ya Telkom Kenya,Mugo Kibati .
Kwa maputo ambayo yapo Kenya sasa hivi tayari kutoa huduma ya intaneti, yalifurishwa na kupeperushwa kutoka Amerika ya Kati na yamechukua karibu wiki nne kufika nchini Kenya.
Maputo hayo yamepitia bahari ya Atlantic, bahari ya Hindi kule Mombasa mpaka yakafika eneo la Baringo.
Na kila baada ya siku 120, maputo mapya yatakuwa yanaingia nchini Kenya kwa kutumia mikondo ya upepo.
Teknolojia hii ya mawasiliano ya maputo inayotumia 4G imefanyiwa majaribio kwa watu 35,000 na kwa kuanza, huduma itapatikana katika eneo la kilomita 50,000 za mraba.
Je teknolojia hii inamaanisha nini?
Kipindi hiki cha virusi vya corona kote duniani kimebadilisha kabisa mawsiliano, mwenendo wa kufanya kazi na sasa njia kuu inayotumika katika kutekeleza shughuli za kila siku, kuanzia biashara hadi kwenye mashirika na kadhalika ni kupitia mtandao.
Lakini watu wengi hasa wa vijijini wanapitia changamoto kuendeleza shughuli kama kawaida. Huduma hii ya teknolojia ya maputo inafika katika sehemu ambazo hazina mfumo wa kawaida wa mawasiliano.
Kwa matumizi mteja hataona tofauti na huduma yoyote ile kwa maana kwamba huwezi kutambua kuwa huduma hii ni ya teknolojia ya maputo au ile ya mawasiliano ya chini ya ardhi au hata upande wa data.
Lakini mkuu wa Kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Telkom Kenya, Mugo Kibati anasema kampuni hiyo itajitahidi kuhakikisha gharama ya data haitofautiani na huduma ya awali.
Hatima ya baadae ya Teknolojia ya maputo
Wakati mazungumzo yanaanza kati ya Kenya na kampuni inayotoa huduma hii Loon, puto lilikuwa linakaa angani kwa siki 60 tu lakini miaka miwili baadae, kampuni hiyo imeimarisha huduma na sasa hivi puto lina uwezo wa kukaa angani kwa siku hadi 120.
Kuna matumaini ya kuimarisha huduma hii hata zaidi sio tu kwa teknolojia ya ndani ya puto lakini pia inayoendesha huduma nzima.

Chanzo cha picha, Getty Images
Moja ya maeneo yaliyokuwa yanafanyiwa majaribio yameonesha kwamba kasi ya kupakua video ilikuwa ni 18.9Mbps (megabaiti kwa sekunde) huku kasi ya kuweka kitu mtandaoni ikiwa ni 4.7Mbps.
Huduma hii bado haijaimarika kwasababu ni mpya lakini kuna matumanini kuwa itazidi kuimarika ila kwasasa hivi, huduma hii inafuatiliwa kusaidia mawasiliano katika kipindi hiki cha corona.
Aidha, Kenya ina mipango ya kuwezesha huduma kufika katika maeneo mengine ambayo yamekuwa na changamoto ya mawasiliano.
Mwaka 2018, kampuni ya Loon ilishirikiana na Telkom Kenya katika utoaji huduma ya kibiashara.
Mkuu wa kampuni wa Loon, Alastair Westgarth, amesema usambaaji wa virusi vya corona kuna maanisha kwamba washirika wote (kampuni ya Loon, Telkom Kenya na serikali) wanafanyiakazi kuhakikisha huduma ya intaneti inapatikana kwa kasi ya juu.
Aidha mkuu wa Telkom Kenya, Mugo Kibati amesema, '' hii ni hatua kubwa iliopigwa katika huduma ya intaneti Afrika''.
Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wanasema kwamba ingekuwa vizuri zaidi kama huduma hii ingekuwa inapatikana kwa nchi nyingine Afrika kwasababu Kenya tayari inakadiriwa kwamba watu milioni 39 kati ya milioni 48 wanapatikana mtandaoni.
Awali, maputo ya kampuni ya Loon yamewahi kutumika wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea Peru.












