George Floyd: Wachezaji mbalimbali duniani walivyozungumzia kifo cha Floyd

Muda wa kusoma: Dakika 3

Wachezaji wa Liverpool walipiga goti katikati ya uwanja wa Anfield kufikisha ujumbe wa kupinga mauaji ya raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika George Floyd mjini Minneapolis.

Picha iliyokuwa na wachezaji 29, ilichapishwa ikiwa na ujumbe ''Umoja ni nguvu. # BlackLivesMatter'' Wachezaji hao waliripotiwa kuomba kupiga picha hiyo walipokuwa mazoezini siku ya Jumatatu.

Wachezaji wa Manchester United, Paul Pogba na Marcus Rashford walipaza sauti zao kupinga vitendo vya ubaguzi.

Maandamano yamekuwa yakifanyika nchini Marekani, baada ya kifo cha mtu huyo ambaye hakuwa amejihami kwa silaha kilichotokea tarehe 25 mwezi Machi baada ya kushikiliwa na maafisa wa polisi miongoni mwao akiwa Derek Chauvin, ambaye alimkaba shingo chini kwa kutumia goti lake,kwa takribani dakika tisa.

Afisa huyo anakabiliwa na mashtaka ya mauaji na amekwishakufukuzwa kazi.

Kiungo huyo wa Manchester United Paul Pogba ameeleza kwa masikitiko makubwa katika ukurasa wake wa Instagram kuwa alikuwa akihisi ''hasira, huzuni, chuki, maumivu na masikitiko ''.

''Huruma kwa George na jamii ya watu weusi wanaokumbwa na vitendo vya kibaguzi KILA SIKU ! iwe kwenye mchezo wa mpira wa miguu, kazini , shuleni POPOTE! Hali hii inapaswa kukoma kabisa. Si kesho au siku nyingine, ikome LEO! Vitendo vya unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi hauwezi kuvumilika tena. Siwezi kuvumilia, sitavumilia, HATUTAVUMILIA''

''Ubaguzi ni ujinga, UPENDO ni werevu, VUNJA ukimya , ZUIA ubaguzi wa rangi.''

Mchezaji mwenzake Rashford alisema amekuwa ''akijaribu kufikiri kinakchoendelea duniani''.

Mshambuliaji wa England alieleza ''wakati mwingine nimekuwa nikiwaambia watu kuwa pamoja, kufanya kazi pamoja na kuungana, tunaonekana kugawanyika zaidi kuliko wakati mwingine wowote''.

''Watu wameumia na watu wanataka majibu. Maisha ya mweusi yana maana. Utamaduni wa mtu mweusi una maana. Jamii ya watu weusi ina maana. Tuna maana.''

Wachezaji mbalimbali wa Liverpool walichapisha picha zao wenyewe wakiwa wamepiga goti katika uwanja wa Anfield, wakiwemo wachezaji wa nafasi ya ulinzi Virgil van Dijk, Joe Gomez, Andrew Robertson na Trent Alexander-Anorld na viungo Georginio Wijnaldum na James Milner.

Nchini Ujerumani wachezaji Jadon Sancho na Achraf Hakimi wa Borussia Dortmund, Weston McKennie wa Schalke na Marcus Thuram wa Borussia Monchengladbach walifanya maandamano uwanjani mwishoni mwa juma lililopita.

Wachezaji wanne wanachunguzwa na Shirikisho la soka nchini Ujerumani (DFB) kwa kuvunja sheria kwa kutoa matamshi ya kisiasa kwenye uwanja wa michezo.

Lakini rais wa shirikisho hilo Fritz Keller amesema ''anaheshimu na kuwaelewa'' wachezaji hao.

Alisema: '' Ninaheshimu sana wachezaji wenye sifa ya kuonesha umoja. Ninatamani kuwepo na wachezaji wengi wa namna hii na ninajivunia.

''Kilichotokea nchini Marekani kinaweza kumuudhi mtu yeyote, watu wanapobaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi zao ni jambo lisilovumilika, nimeshtushwa sana.Waathirika wa vitendo hivi wanahitaji umoja kutoka kwetu sote.''

Unaweza pia kusoma:

'Imetosha'

Mshambuliaji wa kikosi cha Liverpool Rhian Brewster na nyota wa mchezo wa tenis Serena Williams, Coco Gauf na Naomi Osaka ni miongoni mwa wanamichezo waliozungumzia kifo cha Floyd pia .

lejendari wa mchezo wa kikapu Michael Jordan alisema ''amesikitishwa sana, ameumia kweli na ameghadhabishwa''.

''Ninawaunga mkono wanaopinga ubaguzi na unyanyasaji kwa watu kwa misingi ya rangi zao nchini mwetu. ''imetosha.''

Mjane wa Mcheza kikapu mashuhuri marehemu Kobe Bryant alichapisha picha yake na mumewe akiwa wamevalia T-Shirt iliyoandikwa ''Siwezi kupumua''

Aliandika ''Mume wangu alivaa nguo hii miaka mingi iliyopita na sasa bado tuko kwenye hali hii tena,''

''Maisha ni mafupi , maisha hayatabiriki , maisha ni rahisi kuharibika.'' Aliandika Vanessa.

Unaweza pia kutazama: