Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Walioambukizwa corona waoongezeka Madagascar licha ya kuwa na 'dawa'
Idadi ya wagonjwa wa corona inaendelea kuongezeka Madagascar licha ya nchi hiyo kudai kuwa imepata ''dawa'' ya mitishamba ya kukabiliana na kuponywa maradhi hayo.
Kufukia sasa nchi hiyo ina jumla ya watu 195 waliambukizwa virusi vya corona baada wagonjwa wengine wapya 35 kuripotiwa siku ya Alhamisi.
Mwezi uliopita, rais Andry Rajoelina alizindua dawa ya kienyeji inayofahamika kama Covid-Organics ambayo alisema inaweza kuzuia na kuponya ugonjwa wa corona.
Kabla ya uzinduzi wa dawa hiyo Taasisi ya taifa ya tiba nchini Madagascar (Anamem) ilimeonyesha wasiwasi wake juu ya ufanisi wa dawa hiyo inayoelezewa na rais Andry Rajoelina kama yenye uwezo wa kuzuwia na kuponya corona.
Taasisi hiyo ilisema kuwa mitishamba inaweza kudhuru afya ya mtu kwani "hakuna ushahidi wa ufanisi wake kisayansi".
Shirika la habari la AFP lilimnukuu Dkt Charles Andrianjara, Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti ya Imra, akisema kuwa Covid-Organics inapaswa kutumiwa kama kinga.
Lakini alijihadhari zaidi kuzungumzia zaidi juu ya matumizi ya dawa hiyo kama tiba.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa hakuna ushahidi wa tiba ya Covid-19 baada ya Bwana Rajoelina kutangaza dawa yake.
Likizungungumzia dawa ya Covid-Organics, WHO liliambia BBC kwamba shirika hilo la dunia halishauri "matibabu ya kibinafsi ya dawa zozote... kama njia ya kinga au tiba ya Covid-19."
Lilirejelea kauli za Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kwamba "hakuna njia za mkato" za kutafuta dawa ya kupambana na virusi vya corona.
Majaribio ya kimataifa yanaendelea kupata tiba yenye ufanisi, WHO iliongeza.
Siku ya Jumatano Jumuia ya Kiuchumi, ya mataifa ya Afrika Magharibi (Ecowas) ilipinga ripoti kuwa iliagiza ''dawa'' ya corona kutoka Madagascar.
Ecowas ilisema kuwa "inafahamu kumekuwa na madai tofauti tiba ya corona ambayo imetolewa kutoka maeneo tofauti duniani, lakini inaweza tu kuidhinisha dawa ambayo ubora wake umeidhinishwa kupitia utafiti wa kisayansi".
Tanzania kutuma ndege Madagascar
Mnamo Mei 3, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli alisema kuwa atatuma ndege Madagascar kwenda kufuata dawa ya hiyo mitishamba.
Wakati huo Bw. Magufuli alisema kuwa amewasiliana na Madagascar baada ya kupokea barua rasmi kutoka nchi hiyo iliyoeleza kuwa wamegundua dawa ya corona.
Shirika la Afya Duniani limesema ni muhimu dawa zinazosemekana kuwa na uwezo wa kutibu kufanyiwa majaribio kwanza na kuonya kuwa huenda watu wakaona wamepata tiba na kujihisi kuwa salama ikiwa watakuwa na imani na dawa ambazo hazijafanyiwa majaribio.