Virusi vya Corona: Mazishi ya usiku na hofu ya corona Tanzania

    • Author, Athuman Mtulya na Basillioh Mutahi
    • Nafasi, BBC News, Nairobi na Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Picha za video za mazishi ya usiku zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Tanzania na kusababisha baadhi ya watu kuibuka na maswali juu ya namna serikali inavyolishughulikia janga la virusi vya corona.

Video hizo zinaonesha mazishi yakifanyika chini ya ulinzi huku watu waliovalia mavazi maalumu ya kujikinga dhidi ya maambukizi huku waombolezaji wachache wakiruhusiwa kuhudhuria.

Wanasiasa wa upinzani na wahanarakati wanaamini huo unaweza kuwa sehemu ya mpango wa mamlaka kuficha hali halisi ya mambo.

Mamlaka nchini Tanzania pia zimekuwa zikilaumiwa kwa kutotoa takwimu za kila siku juu ya ugunjwa huo.

Tofauti na nchi nyingi, Tanzania haijachukua hatua kali za kupiga marufuku watu kutoka nje ijapokuwa mikusanyiko mikubwa ya watu kama misiba na harusi imepigwa marufuku.

Lakini usiri wa mazishi yaliyopigwa picha unachochea hisia kuwa ukubwa haswa wa maambukizo nchini humo unafichwa.

Jana Jumapili, Wizara ya Afya Tanzania katika tarifa yake kwa uma imesema kuwa hakuna sababu ya maiti kuzikwa usiku ama gizani.

"Katika kipindi hiki, tunaelekeza maafisa afya na waganga wakuu wa wilaya na mikoa kuhakikisha familia zinashirikishwa kikamilifu na bila hofu au haraka katika kuandaa na kufanya mazishi kwa heshima zote za utu," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi.

"Sitaki kuhisi kuna kitu kinafichwa. Nataka Serikali itimize wajibu wake... Hivi sasa tuna shuhudia misiba mingi, mazishi ya watu usiku usiku na hata miili ya watu mitaani," kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe ameiambia BBC.

"Bila kuwa wawazi wananchi watapata hofu kubwa na kusababisha maafa zaidi...Bila uwazi tutakuwa na Covid 19 kwa muda mrefu sana hapa Tanzania."

Hata hivyo viongozi wa serikali kuanzia Rais Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wamekuwa wakionya juu ya upotoshaji wa takwimu na taarifa mitandaoni na kuwa si kila anayekufa basi ni corona.

Kufikia sasa taifa hilo limethibitisha wagonjwa 480 wa Covid-19 na vifo 16.

'Salamu ya Wuhan'

Kipaumbele kikuu cha serikali ni kutoumiza uchumi wa nchi huku rais Magufuli akipinga kulifunga jiji la kibiashara la Dar es Salaam.

Magufuli alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa mwanzo duniani kuacha kusalimiana kwa kupeana mikono mwezi Machi mwaka huu - na alipigwa picha akisalimiana na viongozi wa upinzani ikulu kwa kugongesha miguu - maamkizi hayo yamepewa jina la 'salamu ya Wuhan'.

Siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, alisema ataendelea kupeana mikono na wat umara tu baada ya kutembelea hospitali moja - baadae, aliambukizwa corona na kufikia hatua ya kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi na kuhitajia usaidizi wa kifaa ya kupumulia.

Hata hivyo baadhi ya misimamo ya kiongozi huyo wa Tanzania juu ya hatari ya corona imezua utata - japo wale wanaofahamu aina yake ya uongozi inaendana na aina yake ya uongozi wanaweza wasistaajabie sana - na jina lake la utani, "Tingatinga ", linaashiria pia sifa yake ya umwamba.

'Nendeni kwenye nyumba za ibada kwa uponyaji'

Magufuli amesisitiza kuwa watu waendelee kuhudhuria katika nyumba za ibada ili kupata "uponyaji wa kweli " - ijapokuwa nyumba hizo zimeonekana katika sehemu mbalimbali duniani kuwa na hatari ya kusambaza maambukizi.

Katika mwezi huu mtukufu wa Waislamu wa Ramadhani, misikiti ingali wazi kwa waumini kusali japo mlo wa futari ambao umekuwa ukitolewa kwa wasionacho misikini unatakiwa kufungwa na watu wasikusanyuke kula kwa pamoja.

Akihudhuria ibada kanisani wiki chache zilizopita, Magufuli mwenye shahada ya uzamivu (PhD) katika kemia, aliviita virusi vya corona kuwa ni "shetani".

"Haviwezi kuishi kwenye mwili wa Kristo. Vitateketea mara moja," amesema.

Rais amekuwa mara kwa mara akiwanasihi wananchi wake kujibidiisha katika sala huku serikali ikitenga siku maalumu za maombi dhidi ya ugonjwa huo.

Je barakoa ni salama?

Magufuli pia amezuia kupulizwa dawa katika maeneo ya wazi, na kusema kuwa upulizaji wa klorini unaweza kuwa hata ulichochea kasi ya maambukizi jijini Dar es Salaam.

"Hakuna fumigation inayoua corona. Kile kilichofanyika Dar es Salaam ni upuuzi ... Klorini inaua mbu, viroboto na mende.

"Na je, vipi kama [hiyo dawa] ilikuwa na corona ndani yake."

Kuna mjadala juu ya ufanisi wa kupuliza dawa nje kama sehemu ya kuua virusi vya corona, kitu ambacho miji mbalimbali duniani imefanya, kwa kuwa baadhi ya dawa huvunjwa makali yake na miale ya jua - hata hivyo hakuna maana kuwa, kufanya hivyo kunasambaza virusi.

Rais pia ameonesha kutilia mashaka usalama wa baadhi ya nyenzo: "Hata vifaa vya kupimia, barakoa ambazo tunaziagiza, lazima tujiulize je zipo salama kwa watu wetu?"

Amepigia chapuo njia mbadala ambazo ni za kiasili pia akiitaka wizara ya afya kushauri juu ya kujifukiza kwa kutumia mitishamba.

Jana Jumapili, amesema kuwa anapanga kutuma ndege Madagascar kufata kinywaji cha mitishamba ambacho rais wa nchi hiyo Andry Rajoelina anakipigia chapuo kuwa ni tiba ya corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa hakuna dawa ya kutibu Covid-19 na linaonya watu Magufuli pia ametilia mashaka ubora na ufanisi wa maabara kuu ya taifa hilo ambapo sampuli hupimwa, akisema kuwa alipeleka sampuli kwa siri za Wanyama na matunda ambapo papai, kwale na mbuzi walikutwa na virusi.

"Lazima kuna watu wameambiwa positive lakini si wagonjwa wa corona, na inawezekana wengine wakafa kwa hofu. Papai lile lipo halijafa linaiva tu. Mbuzi yule yupo tu hajafa, fenesi lile lipo tu labda lije kuoza…

"…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa," amesema Magufuli.

Kinjeketile Ngwale

Hatua zinazochukuliwa na Magufuli zimefananishwa na baadhi ya watu mitandaoni na shujaa wa vita ya Maji Maji nchini Tanzania dhidi ya Wakoloni wa Kijerumani mwanzoni mwa karne ya 20.

Kinjekatile aliwaaminisha wapiganaji wa Kiafrika kuwa dawa yake ingeliweza kugeuza risasi za Wajerumani kuwa maji na kufanya hamasa kubwa kwa wapiganaji hao lakini hatimaye walishindwa.

WHO meridhishwa na baadhi ya hatua ambazo Tanzania imechukua kama kufunga shule na vyuo japo inaamini kuna mengi zaidi ambayo yangefanyika toka siku za awali kuzuia kasi ya maambukizi.

"Kwa hakika tumeona kuwa watu kuacha kutangamana, pamoja na kupiga marufuku kwa mikusanyiko ya watu wengi kumechukua muda mrefu kufanyika na tunaamini kuwa hayo yanaweza kuwa ni moja ya mambo yaliyosababisha ongezeko la kasi la wagonjwa wa corona," amesema Mkurugenzi wa WHO wa kanda ya Afrika.

Na ijapokuwa michezo na matamasha ya burudani yamepigwa marufuku kwa sasa, kwa biashara nyingi zilizobaki hali inaendelea kama kawaida.

Migahawa mikubwa nchini humo inatekeleza amri ya kuuza chakula kikiwa kimefungwa lakini hali ni tofauti katika migahawa midogo ifahamikayo kama mama ntilie ambapo watu wanakula kama kawaida.

Usafiri wa umma unaendelea, japo magari hayo hayatakiwi kusimamisha watu, bado kukaribiana kwa abiria limekuwa ni jambo gumu kuhakikisha halitokei.

'Watu wanaogopa'

Katika soko kuu la samaki la Kivukoni jijini Dar es Salaam kuna matanki ya maji ya kunawa mikono na sabuni katika lango la kuingilia lakini hatua za kutokaribiana haitekelezwi na sio kila mtu anavaa barakoa.

Mchuuzi wa samaki Juma Issa anafuraha kwamba katika mji huo bado hakujawekwa marufuku ya kutokutoka nje kwasababu analazimika kufanyakazi kila siku ili kukimu mahitaji ya familia yake, lakini tayari ana hofu kwamba baadhi ya wateja wanajitenga kwa hiari yao.

"Najua kwamba hili ni janga baya na ninafanyakazi hapa katika soko la samaki ambako kunaweza kuwa hatari zaidi kwasababu watu wengi hutembelea soko hili. Ninaamini kwamba tayari watu wanaogopa kuja hapa," ameiambia BBC.

Anataka serikali kuhakikisha kanuni za usafi zinafuatwa ili wateja kuwa salama.

Ni maoni yanayoungwa mkono na Mohammed Khamis mjini Zanzibar, ambaye anasema msikiti wa eneo lake haujachukua hatua stahiki kulinda watu.

"Nilikuta ndoo yenye maji pasi na sabuni. Msikiti wenyewe haunyunyiziwi dawa kabla na baada ya sala," ameiambia BBC.

Na hatimae ameacha kwenda msikitini na kufanya ibada nyumbani ili kujilinda.

"Si mimi tu, hata baadhi ya jamaa zangu katika maeneo mengine wameamua kufanya hivyo kujilinda. Maelekezo kutoka ofisi ya Mufti yapo wazi, tatizo ni katika utekelezaji wake huku chini, nah apo ndipo hatari ilipo," amesema.

Na kutokana na vifo vya wabunge watatu chini ya wiki mbili, chama kikuu cha upinzani Chadema ambacho kimekuwa kikitoa wito wa kuahirishwa kwa vikao vya bunge kwa muda, kimepiga marufuku wabunge wake kushiriki vikao hivyo na kuwataka wajitenge angalau kwa kipindi cha wiki mbili.

Mamlaka haijahusisha vifo hivyo na virusi vya corona lakini hatua hiyo inaakisi kutoaminiana kuhusu namna nchi hiyoi inavyokabiliana na janga la corona.