Omar al Bashir kupelekwa mahakama ya ICC

Baraza la mpito limekubali kumkabidhi rais wa zamani Omar al Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya ICC.

Omar al Bashir alikuwa akitafutwa kutokana na makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu.

Mwezi Desemba kiongozi huyo wa zamani aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi mwezi Aprili, alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na kituo cha marekebisho ya tabia kwa makosa ya rushwa.

Chini ya sheria za sudan, watu wa umri wa zaidi ya miaka 70 hawatumikii kifungo gerezani. Bashir sasa ana miaka 76

Kiongozi huyo wa zamani aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi mwaka 1989 na kutawala kwa mkono wa chuma.

Waendesha mashtaka wa mahakama ya ICC waliomba ashtakiwe kwa makosa ya mauaji katika jimbo la Darfur.

Unaweza pia kusoma:

Waendesha mashtaka Sudan pia walimshtaki kwa makosa ya kuwaua waandamanaji wakati wa maandamano yaliyosababisha kuondolewa kwake madarakani.

Umoja wa mataifa umesema kuwa watu karibu 300,000 waliuawa na wengine milioni 2.5 walikimbia makazi yao.

''Haki haiwezi kufikiwa ikiwa hatutatibu majeraha,'' alisema msemaji wa serikali.

''Tulikubali kuwa kila anayetafutwa atafikishwa mbele ya ICC. Ninasema hili kwa uwazi kabisa,'' alisema Mohammed Hassan Eltaish.

Tuhuma dhidi ya Omar al-Bashir

Mauaji ya kimbari

Kuwaua watu wa jamii ya Fur, Masalit na Zaghawa

Kuwasababishia mafadhaiko makubwa ya kimwili na kiakili

Kuwaweka katika hali ngumu kwa kuwaharibia makaazi yao

Uhalifu dhidi ya binadamu

Mauaji

Kumpoteza mtu

Kuwahamisha watu kwa nguvu

Ubakaji

Mateso

Uhalifu wa kivita

Kushambulia raia katika jimbo la Darfur

Kuiba mali katika miji na vijiji

Kuzaliwa kwake

Omar al Bashir alizaliwa mwaka 1944 katika familia ya wakulima kaskazini mwa Sudan, ambayo pia ni sehemu ya ukoo wa ufalme wa Misri.

Ni mwanachama wa Al-Bedairyya Al-Dahmashyya, kutoka kabila la Bedouin.

Alijiunga na jeshi la Misri akiwa kijana mdogo na kupanda ngazi ya uongozi wa jeshi hilo, katika vita dhidi ya Israel mwaka 1973.

Ni mambo machache sana yanajulikana kuhusu maisha ya kibinafsi ya kiongozi huyo wa zamani wa Sudan.

Hana watoto na alipofikisha miaka ya 50 alioa mke wa pili.

Alimuoa mjane wa Ibrahim Shams al-Din, anayetajwa kuwa shujaa wa kaskazini - kama mfano kwa wengine, alisema

Mapigano ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe yaliwafanya wengi wa wandani wake wa karibu kuwaoa wajane ambao waume wao waliuawa vitani.