Isabel dos Santos: Benki ya EuroBic yakata uhusiano na bilionea wa Angola

Chanzo cha picha, Getty Images
Benki ya Portugal Eurobic imetangaza kwamba itasitisha uhusiano wake na mwanamke tajiri barani Afrika , Isabel dos Santos.
Hatua hiyo inafuatia uchunguzi uliofanywa na BBC na washirika wake ambapo walifichua mambo yanayozua maswali mengi yaliotekelezwa na bilionea huyo.
Bi Dos Santos anasema kwamba madai hayo dhidi yake ni ya uongo. Mipango yake ya kibiashara ilishirikisha kampuni ya mafuta ya Angola Sonangol na kampuni kubwa ya huduma za simu nchini humo.
Pia unaweza kusoma:
Benki hiyo imesema kwamba bodi ya wakurugenzi imeamua katika mkutano siku ya Jumatatu kufutilia mbali uhusiano wa kibiashara iliokuwa nao na kampuni zinazohusiana na hisa za Isabel dos Santos mbali na watu anaohusiana nao kwa karibu, ikiongezea itachunguza uhamisho wa makumi ya mamilioni ya madola yanayohusiana na Isabel.
Bilionea huyo ambaye ni mwana wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Jose dos Santos anamiliki asilimia 42.5 za hisa za EuroBic kupitia kampuni mbili, na kumfanya kuwa mwanahisa mkuu wa benki hiyo , ripoti zimesema.
Wakati babake alipostaafu kama rais 2017, alifutwa kazi kama mwenyekiti wa kampuni ya mafuta nchini Angola miezi miwili baadaye.
Stakhabadhi zilizofichuliwa mapema wiki hii zinasema kwamba wakati alipoondoka Sonangol, bi Dos Santos aliidhinisha malipo ya $.58m.
Bi Dos Santos alivyopata utajiri
Baadhi ya fedha hizo ziliifilisi akaunti ya Sonangol katika benki hiyo ya EuroBic , kulingana na gazeti la The New York Times.
Siku ya Jumapili ,stakhabadhi zilizofichuliwa na BBC na washirika wake zilionyesha jinsi alivyopatiwa mikataba ya fedha nyingi inayohusiana na ardhi, mafuta, almasi na mawasiliano wakati babake alipokuwa mamlakani.
Stakhabadhi hizo zilionyesha jinsi mwanamke huyo tajiri barani Afrika alivyojipatia mali yake inayodaiwa kuwa na thamani ya $2b kupitia madai ya kuipora nchi yake mbali na kufanya ufisadi.
Jenerali wa mashtaka nchini humo alisema siku ya Jumatatu anataka bi dos Santos kurudi Angola ili kujibu madai hayo na kuahidi kutumia kila njia kumrudisha nyumbani.
Bi dos Santos anasema kwamba madai dhidi yake ni ya uongo na kwamba yanashinikizwa kisiasa na serikali ya Angola.
Tayari anachunguzwa na mamlaka ya Angola kwa ufisadi na kwamba mali yake nchini humo imekamatwa. Awali alikuwa amesema kwamba hakutaka kurudi Angola kwasababu alikuwa akihofia usalama wake.

Isabel dos Santos ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Mwana mkuu wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Jose Eduardo Dos Santos
- Ni mke wa mfanyabiashara wa Congo Sindika Dokolo
- Alihudumu katika shule ya upili ya wasichana ya mabweni nchini England.
- Alisomea uhandisi wa umeme katika chuo kikuu cha Kings College mjini London.
- Akiwa na miaka 24 alikuwa akimiliki hisa katika mgahawa wa Miami Beach uliopo mjini Luanda
- Aliinuka na kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika
- Alichaguliwa kuongoza shirika kuu la mafuta nchini Angola la Sonangol 2016 na kufutwa kazi 2017.
- Ana hisa za asilimia sita katika mafuta ya Ureno na kampuni ya gesi ya Galp ambayo ina thamani ya $830m
- Anamiliki 42.5% ya benki ya Portugal ya Eurobic bank
- Ana asilimia 25% ya hisa katika kampuni ya simu ya Unitelnchini Angola
- Pia ana 42.5% ya hisa katika benki ya Angola kwa jina Banco BIC












