Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Orodha mpya ya mabilionea Afrika yamshirikisha Dangote , Mo Dewji na Isabel dos Santos
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
Mfanyabiashara Mohammed Dewji kutoka Tanzania ametajwa kuwa miongoni mwa mabilioni 20 wa Afrika katika ripoti ya jarida la Forbes la mwaka 2020.
Hatahivyo utajiri wa bilionea wa Tanzania Mo umedaiwa kupungua hadi dola bilioni 1.6.
Katika ripoti hiyo mfanyabiashara tajiri nchini Nigeria Aliko Dangote ameorodheshwa kwa mara ya tisa mfululizo, kuwa mtu tajiri zaidi barani Afrika .
Dangote mwenye umri wa miaka 62 ambaye anafanya biashara ya Simiti, Sukari na unga wa ngano ana utajiri wa dola Bilioni 10.1.
Pia unaweza kusoma:
Dangote anafuatiwa na mfanyabiashara wa Misri Nassef Sawaris ambaye aliongeza utajiri wake kutoka dola bilioni 6.3 hadi dola bilioni nane.
Mfanyabiashara huyo anamiliki asilimia 5.7 ya hisa za kamapuni ya viatu ya Adidas . Ongezeko la hisa za Adidas liliomuongezea dola bilioni moja nukta tano katika akaunti yake.
Bilionea aliyeorodheshwa katika nafasi ya tatu ni raia wa Nigeria Mike Adenuga ambaye utajiri wake unatokana na sekta ya mawasiliano na mafuta. Kampuni yake ya mawasiliano ya simu Globacom ndio ya tatu kwa ukubwa nchini Nigeria ikiwa na wateja milioni 43.
Alijipatia utajiri wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 26 akiuza kanda za viatu na vinywaji.
Bilionea aliyeorodheshwa wa nne barani Afrika ni mfanyabiashara wa almasi na raia wa Afrika Kusini Nicky Oppenheimer.
Nicky ambaye ni mrithi wa mali ya familia yake ya Oppenheimer ana utajiri wa dola bilioni 7.7.
Familia yake imekuwa ikihusika na uuzaji wa almasi.
Isabel dos Santos mwenye utajiri wa dola bilioni 2.2 amedaiwa kujipatia utajiri wake wakati babake alipokuwa rais ambapo alijipatia hisa katika makampuni mengi ya Angola pamoja na benki.
Mwanamke huyo ambaye ametajwa kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika amesema kwamba anamiliki hisa kutoka kampuni zilizopo Ureno, ikiwemo Telecom na runinga ya nyaya.
Msemaji wa Isabel aliambia jarida la Forbes kwamba ni mfanyabiashara huru .
Watu matajiri zaidi duniani
Katika orodha ya watu wanne matajiri zaidi duniani, Bernard Arnault amempiku Jeff Bezos na kuwa mtu tajiri zaidi duniani akiwa na mali yenye thamani ya dola billioni 116.5.
Bernard ndiye mmiliki wa kmapuni ya mitindo ya Louis Vuitton na Sephora akiwa na idadi ya mitindo chapa.
Jeff Bezos anayemiliki mali yenye thamani ya dola bilioni 115.6 alitangazwa kuwa mtu wa pili kwa utajiri zaidi duniani. Bezoz ambaye anatalakiana na mkewe baada ya kuishi pamoja kwa miaka 25 katika ndoa ametangaza kwamba atahamisha asilimia 4 ya hisa zake za Amazon kwa mtalaka wake.
Watatu katika usanjari huo ni Bill Gates mwenye mali yenye thamani dola bilioni 110.6. Yeye na mkewe Melinda wanasimamia wakfu wa Bill na Melinda Gates , ukiwa ndio wakfu mkubwa wa kibinafsi duniani.
Wakfu huo hufanya kazi kuimarisha hali ya afya duniani mbali na kutoa fursa sawa kwa walimwengu.
Tajiri wa nne ni Warren Buffett mwenye mali yenye thamani ya dola bilioni 90.6b. Akijulikana kwa jina maarufu kama Oracle Omaha , Buffet ni mmojwapo wa wawekezaji waliopata ufanisi mkubwa zaidi duniani.
Akiwa mwana wa mbunge wa zamani wa Marekani alinunua hisa akiwa na umri wa miaka 11 na kulipa kodi akiwa na umri wa miaka 13.
Orodha ya mabilionea 20 na utajiri wao barani Afrika:
- Aliko Dangote $10.1 B
- Nassef Sawiris $8 B
- Mike Adenuga $7.7 B
- Nicky Oppenheimer $7.7 B
- Johann Rupert $6.5 B
- Issad Rebrab $4.4 B
- Mohamed Mansour $3.3 B
- Abdulsamad Rabiu $3.1 B
- Naguib Sawiris $3 B
- Patrice Motsepe $2.6 B
- Koos Bekker $2.5 B
- Yasseen Mansour $2.3 B
- Isabel dos Santos $2.2 B
- Youssef Mansour $1.9 B
- Aziz Akhannouch $1.7 B
- Mohammed Dewji $1.6 B
- Othman Benjelloun $1.4 B
- Michiel Le Roux $1.3 B
- Strive Masiyiwa $1.1 B
- Folorunsho Alakija $1 B