Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Abiria 176 wafariki baada ya ndege ya Ukraine kuanguka Iran
Ndege ya Ukraine aina ya Boeing-737 iliyokuwa na abiria zaidi ya 170 imeanguka Iran, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.
Watoa huduma wa msalaba mwekundu wa Iran wanasema kuwa hakuna dalili yeyote kama kuna mtu aliyepona katika ajali hiyo.
Ndege namba PS752 hiyo inayomilikiwa na shirika la kimataifa la ndege la Ukraine ilianguka muda mfupi baada ya kuanza safari katika uwanja wa ndege wa Imam Khomeini mjini Tehran.
Ubalozi wa Tehran imesema kuwa injini ya ndege iliharibika na hakuna uhusiano wowote wa kigaidi.
"Kwa mujibu wa taarifa za awali, ndege hiyo ilianguka kwa sababu ya itilafu za kiufundi.Kwa sasa suala la ndege hiyo kuhusishwa na ugaidi limeondoka," ubalozi ulisema katika mtandao wa wizara ya mambo ya nje wa Ukraine.
Abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo ni raia 82 wa Wairan, 63 wa Canada, 11 wa Ukraine pamoja na wafanyakazi, Waswidi 10, raia wanne wa Afghanistan, watatu wa Uingereza na watatu wa Ujerumani, Waziri wa mambo ya nje Vadym Prystaiko alibainisha.
Ripoti za awali zinadai kuwa ndege hiyo ilikuwa safarini kuelekea mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
Serikali ya Ukraine imesema kuwa inafanya uchunguzi kujua chanzo cha ajali hiyo.
Ziara ya Rais Volodymyr Zelensky kuelekea Oman ilisitishwa na amerejea mjini Kyiv, taarifa zinasema.
"Pole zangu nyingi kwa ndugu na jamaa wa abiria wote waliokuwa katika ndege hiyo pamoja na wafanyakazi wa ndege hiyo,".
Haijabainika ikiwa ajali hiyo ina uhusiano wowote na mzozo wa Iran-na Marekani.
Abiria wapatao 168 na wafanyakazi 9 wa ndege hiyo wamedhibitishwa kuepo kwenye ndege hiyo, Waziri mkuu Oleksiy Honcharuk alisema.
Shirika la ndege la kimataifa la Ukraine limesitisha safari zake zote za ndege za Tehran.
Ndege iliyopata ajali ilifanyiwa matengenezo siku ya jumatatu.
Kikosi ya uokoaji kimetumwa katika eneo la tukio licha ya kwamba wahudumu wa Msalaba mwekundu kuvitaarifu vyombo vya habari kuwa haiwezekani kuwa kuna mtu yeyote angeweza kupona katika ajali hiyo.
Kikosi cha uokoaji kimepata moja ya kisanduku cheusi cha ndege hiyo, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti.
Ukraine imetuma ndege maalum kwa ajili ya kurejesha miili ya waliokufa katika ajali hiyo kwa kutegemea maamuzi ya Iran, amesema bwana Zelensky.
Kitengo cha usafiri wa anga kimeiambia BBC kuwa ndege hiyo iliyopata ajali ilitengenezwa mwaka 2016 na hivyo ni ndege mpya kabisa.
"Hakukuwa na itilafu yeyote kubwa ambayo ingeweza kusababisha matokeo hayo kwa kabla haijaanza safari labda kama kuna kitu kilitokea angani."
"Kwa kuangalia tu pande zote ni kuwa ndege hiyo ilikuwa iko kwenye hali nzuri na haikuwa na haikuwa na matatizo yoyote ya kiufundi hivyo ni ngumu kusema kuwa sababu hiyo ndio ilisababisha kuanguka ."
Bwana Curtis alisema kuwa mamlaka ya Iran,Marekani na Ufaransa zinahusika na uchunguzi zaidi , lakini hawajaweka wazi ni namna gani watafanya kazi kwa pamoja.
Kwa sasa Marekani iko na mvutano mkubwa na Iran, hivyo haijulikani ni namna gani pia wataweza kufanya uchunguzi huo.
"Wataanza kwa kutoa taarifa ya kile kilichotokea katika ndege hiyo...kuangalia kama ni masuala ya itilafu za kiufundi za ndege au kulikuwa uvujaji wa mafuta ambao ulipelekea kufikia hali hiyo, aliasema.
"Na hatuwezi kuondoa uwezekano wa kuwa kulikuwa kuna kitu nje ambacho kilipelekea ndege kuanguka au kuna mambo mengine yanaweza kuhusika pia."
Kuna maelfu ya ndege za Boeing 737-800 ambazo zinafanya shughuli zake duniani kote na zimemaliza safari zaidi ya milioni kumi.
Ndege hizo zimekutana ajali 10, ikiwemo ajali hii pia.
Na hakuna abiria hata mmoja aliyekufa, alisema bwana Curtis.
Hii ni mara ya kwanza kwa shirika la ndege la kimataifa la Ukraine kukutana na ajali kubwa kiasi hiki.