Maswali kuhusu Qasem Soleimani yajibiwa: Je kuuawa kwake kutazua vurugu dunia nzima?

Marekani ilimuua kamanda wa ngazi ya juu wa kikosi maalum cha Iran, Qasem Soleimani katika mashambulio ya angani nchini Iraq siku ya Ijumaa.

Soleimani alikuwa kiongozi wa oparesheni za kigeni za Iran, mashariki ya kati, na mauaji yake yameibua uhasama mkali kati ya Washington na Tehran.

BBC inajibu maswali yote kuhusu athari ya mauaji yake kupitia uchambuzi wa kina.

Kuna uwezekano wa kuzuka kwa Vita Vikuu vya tatu vyaa Dunia ? - Lewis Alcott

Japo baadhi ya wachambuzi wanasema mauaji ya Soleimani ni ishara kwamba Marekani "imetangaza vita"dhidi ya Iran, ni vyema kutopuuza au kutopatia umuhimu tukio hili.

Hatua hii haitasababisha vita vikuu vya tatu vya dunia. Washirika wakuu ambao wanaweza kushiriki katika mzozo kama huo, kwa mfano Urusi na China, sio wahusika wakuu katika sarakasi hii.

Lakini hatua hii huenda ikawa mwanzo mpya katika mzozo wa mashariki ya kati na jukumu la Washington katika mzozo huo.

Iran inatarajiwa kulipiza kisasi, hali ambayo itasababisha mzunguko wa matukio ya kujibu mashabulio kati ya mataifa hayo mawili na huenda ikawa mzozo kamili.

Mashambulizi ya Iran huenda yakawa dhidi ya kambi za kijeshi zinazolinda maslahi ya Marekani katika eneo hilo lakini pia huenda yakalenga ngome zinazoshirikiana na Marekani ambazo Iran inahisi ni muhimu kwake katika mapambano hayo.

Ni haki kumuua mtu chini ya sheria ya kimataifa? - Eamonn Donaghy

Marekani inaweza kujitetea kuwa Soleimani alihusika katika mashambulio ya uchokozi dhidi ya vikosi vyake nchini Iraq.

Vikosi hivyo viko nchini humo kupitia ombi la serikali ya sasa ya Iraq.

Soleimani alikuwa mtu ambaye Washington iliamini aliwaua wafanyikazi wengi wa Marekani.

Kando na hilo kikosi cha Quds ambacho alikuwa akikiongoza kilichukuliwa na Marekani kama shirika la kigaidi.

Kwa hivyo mauaji yake huenda yakaambatana na kauli ya Marekani.

Lakini mtaalamu wa sheria ya kimataifa, kutoka chuo cha mafuzo ya sheria cha Notre Dame, Prof Mary Ellen O'Connell, anasema hatua hiyo itakuwa na athari za kisheria:

"Kujilinda sio sababu ya kuua kisheria. Hakuna kitu kama hicho. Kipengee cha sheria ya Umoja wa Mataifa, kinasema kujilinda ni haki ya kujibu mashambulio kutoka kwa mtu aliyejihami muda huo," alisema.

"Matumizi wa ndege isiyokuwa na rubani kumuua jenerali wa jeshi la Iran Qasem Soleimani mjini Baghdad ilikuwa sio kujibu mashambulizi ya kujihami dhidi ya Marekani. Iran haijashambulia ardhi ya Marekani," alisema.

"Kutokana na hoja hizi, Marekani imetekeleza sio tu mauaji ya kiholela bali pia , imetekeleza hatua inayokiuka sheria nchini Iraq."

Maoni ya Umoja wa Mataifa ni yapi kuhusu mauaji haya? - Sara

Mbali na kuwa mwakilishi wa mataifa yote duniani, ni vigumu kubaini maoni ya Umoja wa Mataifa, kwasababu kiuhalisia hakuna kitu kama hicho.

Kwa mfano mtu, anaweza kutegemea maoni ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa?

Maoni hayo huenda yakatofautiana hali ambayo inaweza kutokana na mataifa wanachama kutoafikiana kuhusu suala fulani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea hofu yake kuhusiana na ongezeko la hali ya taharuki katika eneo la mashariki ya kati.

"Huu ni wakati ambao viongozi wanastahili kuwa na uvumilivu. Ulimwengu hautaki kushuhudia vita vingine katika eneo la Ghuba," Msemaji wake, Farhan Haq,alisema katika taarifa.

Je kuna hatari ya Iran kujibu kupitia silaha ya nyukilia? Ina uwezo wa kutumia nyukila? - Harry Rickman

La hasha. Iran haina programu ya silaha za nyuklia, japo ina vigezo ambavyo vinaweza kuchangia ubunifu wa progamu kama hiyo-na jinsi ya kuwa na moja wapo.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa haihitaji bomu la nyuklia. Lakini je usumbufu wa Washington dhidi yake unaweza kuishawishi kufutilia mbali mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wake wa nyuklia iliyofikia na jamii ya kimataifa? Hilo linawezekana.

Jenerali Soleimani alikuwa anafanya nini Iraq? Serikali ya Iraq inasemanini kuhusu hilo? - Tom

Haijabainika jenerali Soleimani alikuwa na shughuli gani nchini Iraq. Lakini Iran inasaida makundi mashuhuri ya wasi wa kishia nchini humo na mwanamume aliyeuliwa pamoja naye, Abu Mahdi al-Muhandis - alikuwa kiongozi wa Kataib Hezbollah (kundi ambalo linadaiwa kutekeleza shambulio la roketi la hivi karibuni dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani) na naibu wa kamanda wa muungano wa waasi unaoungwa mkono na Iran nchini Iraq.

Serikali ya Iraq imejipata katika hali ngumu kujibu swali hilo, hususan baada ya shambulio hilo kufanyika katika ardhi yake.

Iaq ni mshirika wa Iran na Marekani. Vikosi vya Marekani viko nchini Iraq katka mapambano dhidi ya makundi ya Islamic State (IS).

Jukumu la Marekani na Iran ni lipi Iraq? - Kakinga Moses

Iran ni mshirika wakaribu wa serikali ya Iraq inayoongozwa na Washia. Pia ni mhusika mkuu katika taifa hilo kupitia shughuli zake za kibinafsi na makundi ya waasi waliotajwa hapo juu.

Marekani ina wanajeshi 5,000 troops nchini Iraq, wanaotoa mafunzo kwa wanajeshi wa Iraq na kutoa ushauri kwa nchi hiyo kumaliza na makundi ya kigaidi kama vile IS, yaliyosalia nchini humo.

Kimsingi pande hizi mbili - Marekani na Iran- zimekuwa zikiviziana nchini Iraq.

Swali kuu ni je wakati utawadia ambapo mzozo utaibuka na kufanya kuendelea kuwepo kwa Marekani nchini humo kuwa kukumbwa na kizungumkuti?