Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu matukio haya yatakavyoelekeza mwaka 2020
Mwaka 2020 upo nasi rasmi, huu ni mwaka ambao katika 'ratiba' yake utakuwa na matukio makubwa ambayo yatakuwa sehemu ya historia na kukumbukwa kwa miaka mingi ijayo.
Matukio hayo yatakuwa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki na dunia nzima. Yatakuwa matukio ya nyanja zote kuanzia siasa mpaka michezo.
Je, Nkurunzinza kuachia madaraka?
Tarehe 20 Mei 2020 ni siku ambayo Warundi watakuwa wanapiga kura ya kumchagua raisi wao.
Hata hivyo kuna jambo ambalo linasubiriwa kwa hamu, nalo ni kuona endapo Pierre Nkurunziza atagombea urais ama la.
Toka mwaka 2015, Burundi imekumbwa na machafuko ya kisiasa ambayo yamegharimu maisha ya mamia ya watu na maelfu wengine kwenda ukimbizini.
Chanzo cha machafuko ilikuwa ni tafauti za tafsiri ya katiba na hatimaye Nkurunziza kuongeza muhula wa tatu madarakani.
Mwaka 2018, Burundi ikafanya kura ya maoni ambayo ilibadili katiba na kurefusha mihula ya urais madarakani kutoka miaka mitano hadi saba.
Hatua hiyo ikatafsiriwa na wengi kuwa ni maandalizi ya bw Nkurunziza kusalia madarakani baada ya 2020.
Vyama vya upinzani na makundi ya wanaharakati vimekuwa vikishambuliwa na kumekuwa na mazingira ya woga nchini humo.
Vyombo vya habari vya ndani na nje vimekumbana na mkono wa dola. Mashirika ya habari ya kimataifa kama BBC na VOA yamepigwa marufuku nchini humo.
Je uchaguzi utakuwa huru na wa haki? Je, Nkurunziza ataondoka madarakani? Maswali hayo mawili yatapata majibu yake kufikia Mei, 2020.
Magufuli tano tena?
Ni mwaka wa uchaguzi nchini Tanzania, muhula wa kwanza wa rais John Pombe Magufuli unafikia tamati mwezi Oktoba 2020.
Kwa utamaduni wa chama tawala Tanzania cha CCM, rais anayemaliza muhula wa kwanza hupitishwa bila kupingwa kwenda kugombea muhula wa pili na wa mwisho wa urais wa nchi.
Hivyo, inategemewa rais Magufuli kupita bila kupingwa ndani ya CCM.
Ijapokuwa kuna fununu kuwa baadhi ya makada waandamizi wa chama hicho ambao wanapanga kumpinga Magufuli katika kuwania awamu ya pili ya urais ndani ya CCM.
Jina la waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Tanzania, Bernard Membe limekuwa likitajwa katika fununu hizo, mwaka huu mbivu na mbichi juu ya fununu ama mipango hiyo zitafahamika.
Kwa upande wa upinzani mambo kwao yamezidi kuwa magumu.
Baadhi ya wabunge wa upinzani na madiwani wamevihama vyama vyao na kuelekea CCM katika kile kilichoitwa kuunga mkono juhudi za maendeleo za rais Magufuli.
Hata mgombea kinara wa upinzani katika uchaguzi wa 2015, Edward Lowassa pia amerejea CCM.
Vigogo kadhaa wa upinzani wanakabiliwa na kesi mahakamani.
Malalamiko makubwa ya upinzani ni kuminywa kwa demokrasia nchini humo. Mikutano ya hadhara ya kisiasa imepigwa marufuku isipokuwa kwa mwakilishi (mbunge/diwani) wa eneo husika.
Mwishoni mwa mwaka jana, ulifanyika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini humo. Vyama vikuu vya upinzani vilisusia uchaguzi huo vikilia kuchezewa rafu. Mwishowe 'CCM ikashinda kwa kishindo'.
Toka kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania 1995, hakuna mgombea wa upinzani ambaye amewahi kumuangusha mgombea wa kiti cha urais wa CCM.
Kwa upande wa visiwa vya Zanzibar, rais Ali Mohammed Shein anamaliza miaka 10 yake madarakani na mwaka huu visiwa hivyo vitapata rais mpya.
Abiy Ahmed kupimwa kwenye debe
Toka kuingia madarakani kwa Abiy Ahmed kama waziri mkuu wa Ethiopia mwezi Aprili 2018, mambo yamebadilika kwa kasi nchini humo.
Ethiopia ambayo ilikuwa na jina baya la kuminywa kwa demokrasia, maandamano ya upinzani wa jamii ya Waoromo na mgogoro wa mpaka baina yake na Eritrea yote hayo yakapatiwa ufumbuzi.
Wafungwa wa kisiasa wakaachiwa, maandamano yakaisha, na baraza la mawaziri likapata uwakilishi mkubwa wa wanawake.
Yote hayo yamefanywa na waziri mkuu kijana Ahmed ambaye kwa sasa ana miaka 43.
Ahmed kwa kipindi hiko kifupi madarakani amepokea tuzo ya amani ya Nobel.
Mambo hayo yakitokea, si kila mtu ambaye alikuwa akiridhishwa na kinachoendelea, jaribio la mapinduzi dhidi ya Abiy lilifanyika na kushindikana, japo mkuu wa majeshi aliuawa.
Ethiopia itafanya uchaguzi mkuu mwezi Mei 2020 huku ikionekana kama umaarufu na ushawishi wa Ahmed ukifunika wa wapinzani wake.
Je, Ahmed anakubalika kiasi gani ndani ya Ethiopia? Uchaguzi huo utatoa jibu.
Brexit 'kutimia hatimaye'
Brexit, ni msamiati ambao umetawala siasa za Uingereza toka mwaka 2016.
Toka Waingereza kupiga kura ya kutaka kujitoa Jumuiya ya Ulaya (EU), siasa za nchi hiyo zimezungukwa na suala hilo ambalo limeishia kugeuka jinamizi la kisiasa.
Brexit imeondoka na mawaziri wakuu wawili wa nchi hiyo, wa kwanza David Cameroon ambaye aling'oka baada tu ya kura ya Brexit 2016.
Mwaka 2019, Theresa May ambaye alirithi madaraka kutoka kwa Cameroon naye alibwaga manyanga baada ya juhudi zake za kutaka kufanikisha Brexit kugonga mwamba.
Baada ya panda shuka za kisiasa, hatimaye Boris Johnson amemrithi Bi May. Mwezi Disemba 2019, chama cha Conservative chini ya Boris kilipata ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu ambao haujashuhudiwa kwa zaidi ya miaka 30.
Ushindi huo sasa unampa nguvu ya wingi ndani ya bunge Boris kufanikisha Brexit.
Tayari bunge limepitisha mpango wa Brexit wa Boris, na sasa Uingereza inategemewa kujitoa rasmi EU mwishoni mwa mwezi huu, yaani Januari 31, 2020.
Kesi dhidi ya Trump
Mwaka 2019, Donald Trump aliingia katika historia kwa kuwa raisi wa tatu wa Marekani kupigiwa kura ya kutumua madaraka yake vibaya.
Kura hiyo ya kutokuwa na imani na Trump ilipigwa katika Bunge la Kongresi. Trump anakabiliwa na tuhuma mbili ya kwanza kushawishi nchi ya nje kuingilia mambo ya ndani ya Marekani kwa kuitaka Ukraine kumchunguza mpinzani wake wa kisiasa Joe Bide. Tuhuma ya pili ni kuzuia Kongresi kufanya uchunguzi dhidi yake.
Kura hiyo ilipigwa ndani ya Kongresi ambayo ina wingi wa wabunge wa chama pinzani cha Democrats. Sasa mashtaka hayo yanatarajiwa kupelekwa katika bunge la Seneti. c
Kesi hiyo inatazamiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka huu. Endapo Maseneta watakubaliana na hoja za wenzao wa Kongresi na kupiga kura ya wingi dhidi ya Trump basi atang'oka madarakani.
Hata hivyo, hilo halitazamiwi kutokea kwa kuwa chama cha Trump cha Republican kina wawakilishi wengi kwenye bunge la Seneti.
Uchaguzi mkuu wa Marekani
Trump anategemewa kuruka kihunzi cha kesi yake kwenye Bunge la Seneti, na ikiwa kama inavyotegemewa basi mwezi Novemba 2020 atakutana na kihunzi cha uchaguzi mkuu.
Miaka yake minne madarakani ya kwanza inafikia kikomo mwaka huu, na upinzani dhidi yake ni mkubwa.
Bado chama cha Democrat hakijapata mgombea wake, lakini hasimu wa Trumo Joe Biden, ambaye alikuwa makau wa rais wa Barrack Obama ndiye kinara kwenye mbio za ndani za chama.
Si rahisi kutabiri matokeo kwa siasa za Marekani, lolote linaweza kutokea, ushindi wa Trump dhidi ya Hillary Clinton 2016 ulishangaza wengi. Hivyo hata mwaka huu pia yanaweza kuja 'maajabu'.
Marais watatu kabla ya Trump, Obama, George W Bush na Bill Clinton wote waliweza kutetea nafasi yao kwa mihula miwili.
Liverpool kuvunja uteja wa miaka 30?
Kwenye ulimwengu wa kandanda, mwaka 2020 unaweza kushuhudia kitu ambacho maraya mwisho kuonekana ilikuwa miaka 30 iliyopita.
Japo wenyewe hawasemi, ama yawezekana hawataki kunukuliwa wakisema, miaka 30 ya kushindwa kuchukua taji la Ligi ya Primia kwa Liverpool hatimaye inaelekea kufika kikomo.
Hawawezi kusema hadharani, ama kuonesha furaha yao kwa sasa, kwa kuwa katika miaka hiyo 30 kumekuwa na vipindi ambavyo walikaribia kunyakua kombe lakini likawaponyoka.
Lakini yaonekana mwaka huu hadithi ni tofauti, ubora wa kikosi ni wa hali ya juu, yawezekana ikawa sahihi kusema kikosi hiki cha sasa ndiyo bora zaidi kuliko vyote katika miongo mitatu iliyopita.
Nuru ya ushindi iling'ara zaidi kwa vijana hao wanaonolewa na Mjerumani Jurgen Klopp baada ya kuichapa Leicester City inayoshika nafasi ya pili kwa goli 4-0 siku ya Boxing Day.
Tofauti ya alama baina ya Liverpool na Leicester ni alama 13. Na Liverpool wana mchezo mmoja mkononi, endapo wataushinda pengo litakua alama 15.
Bingwa mtetezi Mancester City wapo nyuma ya vinara Liverpool kwa alama 14 kwa sasa na endapo Liverpool akishinda kiporo chake itakuwa alama 17.
Ili ubingwa uwaponyoke msimu huu, basi watalazimika kufungwa michezo mitano kati ya 19 ijayo, huku wapinzani wao wa karibu, Man City na Leicester washinde michezo yao yote. Hakika hizo zitakuwa hesabu ngumu kutimia.
Kwa namna yeyote ile, Liverpool ni bingwa mteule wa ligi ya Primia msimu wa 2019/2020.
Mara yao ya mwisho kuchua taji hilo ilikuwa ni miaka 30 kamili iliyopita, msimu wa 1989/1990.
Euro 2020 - Nani kuwa mfalme wa Ulaya?
Kwa mara ya kwanza mashindano ya timu za taifa za kandanda za Ulaya yatafanyika katika nchi 12 tofauti.
Mechi ya ufunguzi itapigwa Roma kati ya Italia na Uturuki huku fainali ikipigwa Wembley, Uingereza.
Mfumo huo unatumika kama alama ya kusherehekea miaka 60 mashindano hayo.
Mwaka 2016, timu ya taifa ya Ureno ambayo haikupigiwa chapuo na wengi iliwaacha mahabiki midomo wazi kwa kunyakua kombe hilo.
Inaelekea haya ndiyo yatakuwa nashindano ya mwisho ya Euro kwa Cristiano Ronaldo mwenye miaka 34, swali ni kuwa ataweza kuiongoza timu yake kutetea ubingwa.
Ushindani utakuwa mkubwa, timu nne zilizocheza nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 Croatia, Uingereza, Ubelgiji na Ufaransa zote zinatoka Ulaya.
Olimpiki - Kenya tegemeo la Afrika Mashariki
Haya ndiyo mashindano makubwa zaidi ya michezo ulimwenguni, na mwakani yatafanyika nchini Japani baina ya Juni na Agosti.
Kwa Afrika Mashariki, Kenya ndio imekuwa ikiwakilisha vyema huku Uganda wakijitokeza mara moja moja.
Tanzania imekuwa msindikizaji, mara ya mwisho kushinda medali ilikuwa miaka 40 kamili iliyopita mwaka 1980. Suleiman Nyambui na Filbert Bayi wakishinda medali za fedha.
Kenya hata hivyo imekuwa ikizoa medali kila baada ya miaka minne hususani kwenye eneo la riadha.
Mwaka 2016, jijini Rio Brazil Kenya ilinyakua jumla ya medali 13, kati ya hizo sita zikiwa za dhahabu. Mwaka 2012 jijini London Kenya iliibuka na medali 11, mbili zikiwa za dhahabu.
Na mwaka huu pia, kapu la Kenya la medali linategemewa kuendelea kunona.
Bingwa asiye mpinzani Eliud Kipchoge anapigiwa upatu kuitetea medali yake ya dhahabu katika mbio za marathon aliyoishinda jijini Rio 2016.