Mama Mzazi wa Mwandishi Erick Kabendera amwangukia Rais Magufuli

Mama mzazi wa mwandishi wa habari Erick Kabendera, bi Verdiana Mjwahuzi (81) amemuomba Rais John Magufuli kumsamehe mwanaye.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo, Bi Verdiana amesema mwanae Kabendera ni nguzo muhimu ya ustawi wa familia yake.

Erick Kabendera alikamatwa mwezi Julai 2019 na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, kukwepa kodi na kuongoza kikundi cha uhalifu. Mashtaka ambayo mawakili wake wameyakana.

Tayari mawakili wake wamefungua majadiliano na mkurugenzi wa mashtaka wa serikali (DPP) kukiri makosa na kuomba msamaha.

Wakati Kabendera anakamatwa, tayari afya ya mama yake ilikuwa dhoofu. Leo hii Bi Verdiana amewaambia waandishi wa habari kwamba afya yake ameendelea kudhoofika hasa kwasababu ameshindwa kupata matibabu anayoyahitaji na si kwa wakati unaotakiwa.

"Mheshimiwa Rais na yeye ni mtoto kama walivyo watoto wengine hata kama ni mkubwa. Ni mzazi na analea watoto. Namwomba anionee huruma. Angalia maisha yalivyo magumu, dawa sipati. Naomba Rais anisaidie kama anavyosaidia wazazi wake," amesema Bi Verdiana.

Kabendera ni mtoto wa saba kuzaliwa kati ya watoto nane wa Bi Verdiana.

Amesema pamoja na kuwa mdogo kati ya wanae, Kabendera ni mtoto ambaye mara tu anaposikia mama yake anaumwa hukimbia mara moja aidha kumpatia matibabu au kwenda kumuona nyumbani kwake.

"Huyu mtoto ni Mungu amenizawadia, ni tunu kwangu. Akisikia mama anaumwa anakimbia haraka. Sasa hizo dawa sizipati tena, macho yalikuwa yanauma na moja halioni tena na hili linaloona naona vitu vyeusi," alisema Bi Verdiana

Amemuelezea mwanae kwamba hana hulka ya kusema watu vibaya, asiyependa anasa na mchapa kazi. Bi Verdiana ana amini kwamba mashtaka dhidi ya Kabendera yanatokana na kazi zake za uandishi wa habari.

Unaweza kusoma pia:

"Siwezi kumsifia mwanangu, wanaume wengi wakitoka kazini wanakwenda kulewa lakini Eric anafanya kazi zake hapa nyumbani hadi saa saba usiku na wakati mwingine hadi saa nane . Mambo yote aliyopata ni kwa sababu ya kufanya kazi," amesema Bi Verdiana huku akibubujikwa machozi.

Bi Verdiana pia ameeleza masikitiko yake ya kushindwa kwenda kumsalimia mwanae aliyeko rumande.

"Kule Segerea (gerezani) siwezi kwenda kwa sababu kuna msongamano wa watu, mahakamani kuna ngazi. Lakini mara ya mwisho nilijitahidi nikaenda nilipomuona mwanangu sikulia, nilijikaza lakini chozi moja lilinitoka. Sikujua kama ni yeye, amekonda na ana nywele nyingi kama mwehu. Ni mweusi lakini amezidi kuwa mweusi," alisema Bi Verdiana kwa uhuzuni

Kabendera ni mwandishi wa habari za kichunguzi ambaye amefanya kazi na vyombo vingi vya habari vya ndani na nje ya nchi

Watu wengi wameguswa na kesi ya Kabendera wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu ambao wameielezea kama muendelezo wa uminywaji wa uhuru wa habari na haki ya watu kujieleza nchini

Wiki iliyopita wakili wa Kabendera aliuhoji upande wa mashitaka juu ya kuchelewa kujibiwa kwa barua ya Kabendera iliyokwenda ofisi ya DPP kuomba kuanza kwa majadiliano ya kukiri makosa na kuomba msamaha.

Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega aliutaka upande wa utetezi kwenda ofisi ya DPP kujua mchakato umefikia wapi

Kesi yake imeahirishwa mara kadhaa kwa sababu mbalimbali. Imepangwa kusikilizwa tena tarehe 18 Desemba 2018.