Je ni kwanini Rwanda inapiga marufuku raia wake kusomea DRC?

Rwanda imeanza kutoa masomo maalumu kwa wanafunzi raia wa Rwanda waliokuwa wanasoma katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Mpango huu ni mkakati maalum wa kuwataharisha wanafunzi hao kuendelea na masomo yao nchini Rwanda .

Rwanda unatumia mfumo wa kiingereza jambo ambao ni tofauti na mfumo wa Kifaransa unaotumiwa nchini Kongo.

Hatua hii imeanza mara baada ya Rwanda kupiga marufuku kwa wanafunzi wake kurudi kusoma DRC kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Unaweza pia kusoma:

Uamuzi huo umepokelewa na hisia tofauti miongoni mwa wazazi ambao wanaishi mji wa Rubavu mpakani mwa mji wa Goma kwa kuwa na hofu ya gharama na kuchanganya lugha.

Mwandishi wa BBC Yve Bucyana alizungumza na mmoja wa walimu, bwana James Kamugisha ambaye yuko kwenye mpango wa kuwatayarisha wanafunzi waliokuwa wanasoma DRC kujiunga na shule za Rwanda mwakani.

''Tunawapa mafunzo ya kiingereza, haya ni mafunzo ya nguvu yanayotolewa kwa muda mfupi kwa sababu tunawatayarisha kusoma pamoja na wanafunzi wengine katika shule za hapa Rwanda kama unavyojua mfumo wetu ni wa kiingereza''

Aidha muitikio unaonekana kuwa bado mdogo kulingana na namba ya wanahudhuria darasani ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi zaidi 400 waliokuwa wanasomea mjini Goma na ambao wanahusika na mpango wa Rwanda kuwakataza kurudi Goma.

Honore Munezero ni miongoni mwa wale wachache wanaohudhuria masomo haya maalum:

''Mwanzoni ilikuwa ngumu kwangu kufikiria kwamba nitabadilisha mfumo wa kifaransa tuliokuwa tunatumia shuleni Goma.

Lakini kwa siku chache nikiwa hapa kiingereza nimeanza kukimudu sawa sawa''

Hata hivyo baadhi ya wazazi waliamua kubakiza watoto wao nchini Congo huku wengine wakiwa bado wanatafakari la kufanya.

Unaweza pia kusoma:

Kinachowakera wazazi ni kwamba raia wa DRC wanaoishi mjini Rubavu wao wameendelea kuruhusiwa kwenda kusomea Congo na kuzua wasiwasi kuwa ugonjwa wa Ebola huenda ni kisingizio.

Naibu mkuu wa wilaya ya Rubavu anayehusika na elimu Ishimwe Pascifique amekuwa na haya ya kusema:

''Hakuna uonevu . Kila mtu ana uhuru wa kuchagua anapotaka kusomea.

Mnyarwanda anayetaka kusomea nchini Congo atakwenda na kuishi Congo,siyo kwenda na kurudi kila siku.

Atakayeamua kubaki nchini Congo kwa ajili ya masomo hatutamrudisha kwa nguvu''.