Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ajali ya Kenya ferry yazua gumzo la bahari ina 'wenyewe'
- Author, Faith Sudi
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Kenya ina matumaini wapigambizi wa Afrika Kusini watafanikiwa kuopoa miili ya watu wawili waliozama baharini siku tisa zilizopita.
Mwanamke na binti yake wa miaka minne walizama katika kivuko cha Likoni chenye shughuli nyingi baada ya gari lao kuanguka baharini.
Msemaji wa serikali Cyrus Oguna amethibitisha kuwa wapigambizi hao wa Afrika Kusini watawasili nchini kwa makundi mawili na wataanza kazi ya kutafuta miili hiyo siku ya Jumanne.
Video ya ajali hiyo iliyonaswa wakati wa tukio imekua ikisambazwa katika mitandao ya kijamii.
Tangu siku hiyo kumekuwa na shughuli za uokoaji ambazo zimejumuisha maafisa kutoka vitengo vya Kenya Navy, Kenya Ferry, na wapiga mbizi wa kibinafsi.
Lakini wananchi wamekua wakielekeza hasira zao kwa jeshi la wanamaji la Kenya- kwa kukosa vifaa maalum vya kazi.
Bahari ina wenyewe?
Saa chache baada ya ajali hiyo mkuu wa shirika la Ferry Bakari Gowa aliiambia BBC kwamba kutokana na shughli ambazo huendelea katika eneo hilo, masaa 3 pekee ndiyo yanaweza kutumiwa kutafuta miili ya waathiriwa.
''Hatujachukua muda mrefu, shughuli hii haiwezi kufanyika muda wa usiku pia kwa sababu operesheni ya feri haiwezi kufanyika jioni na asubuhi wakati watu wanatumia kivuko hicho''.
Kufikia sasa, miili ya waathiriwa bado haijapatikana.
Lakini katika mitandao ya kijamii kumezuka swala la "Bahari ina wenyewe". Ni kauli ambayo inazungumziwa sana na wenyeji wa pwani ambao wanadai kwamba janga kama hili linapotokea, sala maalum inapaswa kufanywa ambayo inahusisha kuchinjwa kwa mnyama na kisha damu yake kumwagwa kwenye eneo la tukio ili kusababisha miili ya waathiriwa kujitokeza.
Changawa Gharama ni mkaazi wa Fumbini kilifi na anaamini kwamba kuna njia moja tu ya miili hiyo kupatikana kwa urahisi.
"Zamani , mtu alipopotea,watu walikusanyika na kutafuta ng'ombe mweusi mwenye paji nyeupe, wakamchinja katika eneo alilozama kisha wakamwaga damu kwenye bahari... " Anaeleza Gharama.
''Si ushirikina, ni mila yetu ambayo hatuwezi kuiwacha... Ni kama kumuomba Mungu ili kile ambacho unatafuta ukipate kwa urahisi.''
"Bahari ina wenyewe... Kila bahari lazima iwe na vichumbakazi. Na vichumbakazi ndiyo wenyewe. Lazima tambiko hiyo ifanywe, lazima uwapatie damu kwa kuchinja mnyama ili miili hiyo ipatikane"
Abdul Bar Juma ni Baharia mkongwe kutoka jijini Mombasa.
"Juu ya bahari, maji huwa yanaonekana yametulia lakini chini huwa yanasonga. Kwa hivyo yakisonga hawawezi kuwa wako pale Likoni. Kwa hivyo hayo mambo ya 'ooh inapaswa tuchinje ng'ombe, kufanywe nini...' Hayo ni mambo ya kishirikina.
Katika mila za kiafrika, watu wengi huamini kwamba wakati janga linapotokea kuna hitaji la kuyafurahisha miungu ili kuzuia majanga mengine kutokea.
Kuridhisha miungu hutegemea na imani ya mtu. Mara kwa mara panapotokea ajali inayogharimu maisha ya watu wengi, mbalimbali hukusanyika mahali pale na kufanya maombi kwa imani kwamba yatazuia janga kama lile kutokea tena siku za usoni.
Mfano wakati lori la mafuta lipolipuka baada ya kupoteza mwelekeo na kugongana na gari zingine katika mji wa Naivasha nchini Kenya mwaka wa 2016 na kusababisha ajali ya watu zaidi ya 30.
Wakristo kutoka matabaka mbalimbali walikusanyika katika eneo hilo siku chache baada ya ajali hiyo kutokea na kufanya maombi katika eneo hilo ili kuzuia janga hilo kujirudia.
Kulingana na wataalamu wa Kihistoria, kuna wakati ambapo matambiko yanafanya kazi na kuna wakati ambayo hayafanyi kazi.
"Kuzama kwa hili gari na mengineyo ambayo yamewahi kuzama kunaweza kuambatanishwa na mila na itikadi pamoja na hoyo imani ya kuabudu mizimu. Lakini sidhani kwamba kwa sasa hivi taaluma ya kisayansi na kiteknolojia ina nafasi ya mambo kama hayo. Kuna uwezekano kwamba teknolojia yetu ndiyo imekuwa hafifu ndiyo maana miili kwa muda huu mrefu hazijaweza kupatikana."
"Kisingizio kwamba labda kushindwa kwa serikali au kushindwa kwa watu kuweza kutafuta na kupata hilo gari pamoja na miili ya watu wawili ni kisingizio ambacho baadae tutaanza kukiingiza katika itikadi, mila na desturi za kiasili ili tupate visababu vya kuonyesha ni kwa nini hatujatekeleza wajibu wa kisasa; kwamba tunahitaji kuwa na wataalamu, tunahitaji kuwa na watu wenye ujuzi wa kupiga mbizi na zaidi tunahitaji kuwa na vyombo ambavyo vinaweza kufika mahala ambapo kuna lile gari na miili na vikaweza kuvutwa kuja juu." Anasisitiza Profesa.
Imetimia siku tisa na bado mwili wa Mariam Kaghenda na mwanawe haijapatikana. Watu wengi hasa wakaazi wa pwani wanaamini kuwa limesababishwa na kutozingatia itikadi ya kafara,sawia na wao kuna wengine ambao wana imani kwamba miili hiyo itapatikana kutumiateknolojia lakini bado gumzo la kutolewa kafara linaendelea.