Tanzania: Je, majeruhi wa ajali ya Morogoro watarudi katika hali yao ya awali?

Majeruhi 13 wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro nchini Tanzania kufuatia kulipuka kwa gari la mafuta, wanaendelea na matibabu katika hospital ya Taifa Muhimbili na wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha maumbo na viungo vyao.

Jumla ya majeruhi 47 walipokelewa katika hospitali hiyo ya taifa kutoka Morogoro, ambapo kati yao 34 walifariki dunia na kufanya idadi ya waliokufa kutokana na ajali hiyo kuwa 102.

Daktari Bingwa wa Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Edwin Mrema amezungumza na BBC na kueleza kuwa ni lazima majeruhi wote kufanyiwa upasuaji kwa sababu wameungua sehemu kubwa za miili yao.

" Sehemu kubwa inamaanisha ngozi yote imeshapotea na haiwezi kurudi tena na moto uliopo ndani unaendelea ndani zaidi hivyo usipofanya chochote basi madhara zaidi yatatokea na katika mazingira yetu utaruhusu vijidudu vingine viingie ndani.

Moto ambao uko wazi ambao umeingia ndani ya mwili ukiwa wazi basi ukiacha utaingia ndani zaidi hivyo ni muhimu wafanyiwe upasuaji na kufunika sehemu iliyo wazi.

Kazi yetu katika upasuaji ni kurudisha kazi ya kiungo kilichopotea, ngozi imepotea basi hiyo ngozi inapaswa kurudishwa".

Kazi ya Ngozi

Ngozi ina kazi nyingi ikiwa ni pamoja na kurekebisha joto la mwili kupoa, kukiwa na baridi basi ngozi inasaidia kumlinda mtu kujikinga na baridi na ngozi ni urembo katika mwili wa mwanadamu.

Lakini je, upasuaji wa kurekebisha viungo utafanywaje?

Majeruhi wa ajali ya moto, ngozi za miili yao zimeungua kwa takribani asilimia 80 au 85.

Upo upasuaji ambao wataalamu wanaweza kutumia misuli endapo kufunika kama mfupa uko wazi, lakini kwa wale ambao wameungua ngozi ambao ndio wengi katika majeruhi hao, wao watazibwa ngozi zao kwa kutumia sehemu kama ya paja.

"Tutarudisha ngozi hiyo kutoka kwenye sehemu kama mapaja kwa sababu kuna sehemu kubwa ambayo tutaweza kupata ngozi na watapona vizuri tu na kurudi katika hali yao ya kawaida".

Daktari Mrema aliongeza kusema kuwa upasuaji huo mpaka ufanyike, unahitaji muda wa kama wiki mbili au tatu ikitegemea unene wa sehemu iliyoungua.

"Ile ngozi imekufa hivyo lazima itoke kwa dawa na kila siku tunasafisha kwa usafi kabisa.

Wiki mbili mpaka tatu , inategemea ule unene wa kuungua au athari ya moto imeenda chini kiasi gani?"