Kanisa katoliki linapinga chanjo ya saratani inayopangwa kutolewa kwa wasichana wadogo Kenya

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili

Shirika la madaktari wa Kanisa Katoliki nchini Kenya (KCDA), linapinga mpango wa kuwapa chanjo dhidi ya virusi vya HPV viinayosababisha saratani ya shingo ya uzazi kwa watoto wasichana wa miaka 10.

Hatua yao inakuja wakati ambapo Wizara ya Afya nchini humo inajiandaa kufanya kampeini ya chanjo hiyo katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Madaktari hao wanasema hatua ya kupinga chanjo hiyo inazingatia ''utafiti'' ambao unaashiria kuwa chanjo ya HPV ni hatari kwa binadamu.

"Chanjo hiyo sio salama kwa mtu yeyote sio watoto pekee. Walioitengeneza hawasemi madhara yake wakati yapo wazi kabisa na ibainike wazi kuwa sio usemi wangu ," Mwenyekiti wa KCDA, Dkt Stephen Karanja, ameiambia BBC.

"Hawa watoto sharti walindwe na kila mtu ikiwa ni pamoja na serikali kuhakikisha wanadumisha maadili mema katika jamii." aliongeza

Wataalamu wa ngazi ya juu wanasema madai hayo ''Hayana msingi wowote''

Daktari bingwa wa wanawake katika Hospitali Kuu ya Kenyatta Dkt Alfred Mokomba katika tafiti zake zilizopita amesema chanjo hiyo ni salama na inaweza kutumiwa kwa watoto.

Wizara ya Afya itawapatia bila malipo dozi mbili ya chango ya HPV wasichana wa miaka 10 katika hospitali za umma 9,000, za kibinafsi na zile za kidini kote nchini.

Shirika la Afya Duniani linapendekeza wasichana wapewe chanjo hiyo na wanawake kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu mara moja kwa mwaka ili kuwapunguzia hatari ya kupata maradhi ya saratani.

  • Linasema chanjo dhidi ya saratani ni imara zaidi ikipewa wasichana wa kati ya miaka 9 na 14.
  • Kuna aina karibu 100 ya virusi vya HPV, na 14 kati ya hizo husababisha saratani.
  • Aina mbili ya HPV (16 na 18) husababisha 70% ya saratani ya shingo ya uzazi.

Siku ya Jumanne maafisa wakuu wa wizara ya Afya nchini Kenya walikutana na washirika wao kujadiliana kuhusu hali ya saratani nchini na kujiandaa kwa mpango wa chanjo ya kitaifa dhidi ya ugonjwa huyo.

"Kupata chanjo ya HPV ni njia bora zaidi ya kujikinga na saratani ya shingo ya uzazi na ni salama. Mimi pia ni baba wa watoto wa wasichana na wote wamepata chanjo. Kwa kuwapa chanjo watoto wetu wasichana tunawakinga na ugonjwa huo maisha. Watakuwa vizuri, nakufikia malengo yao maishani," alisema mwakilishi wa WHO nchini Kenya Dr Rudi Eggers.

Wizara ya Afya inalenga kupunguza visa vya saratani ya shingo ya uzazi - ambaye ni ya pili baada ya saratani ya matiti nchini Kenya, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la kimataifa la utafiti wa saratani.

Ugonjwa huo unaua karibu wanawake saba nchini Kenya kila siku na karibu 3,000 kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu kutoka wizara ya Afya.

Kuna karibu visa vipya 40,000 vya saratani ya shingo ya uzazi vinavyoropotiwa duniani kila mwaka. Duniani ni ugonjwa wa nne unaowaathiri zaidi wanawake

"Inasikitisha kuwa tunapoteza wanawake saba kila siku kutokana na ugonjwa ambao unaweza kupingwa kupitia chanjo. IUkijikinga dhidi ya maambukizi ya HPV unaweza kujiepusha na saratani ya shingo ya uzazi," alisema mkuu wa chanjo katika wizara ya Afya, Dkt Collins Tabu, katika mkutano wa washika dau wa afya nchini Kenya uliofanyika siku ya Jumanne.

Gharama ya matibabu

Alisema chanjo hiyo ambayo pia ni mbinu ya kinga ni ya gharama nafuu ikilinganishwa na matibabu ya saratani.

"Tunachokifahamu kufikia sasa ni kuwa chanjo hiyo inatoa kinga ya hadi 90% dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi. Tafiti mbili zilizofanywa na KNH zinaonesha kuwa chanjo ya HPV ni bora zaidi katika kukabiliana na aina ya 16 na 18 ya virusi vya HPV- ambavyo vinasadikiwa kusababisha saratani ya shingo ya uzazi," Dkt Mokomba aliliambia Gazeti la Nation.

Kwa mujibu wa madaktari wa Kanisa Katoliki, wanasema virusi hivyo kama magonjwa ya zinaa, huwaathiri watu "walio na mienendo ya kufanya ngono kiholela".

Sasa wanatoa wito kwa serikali kuhakikisha wazazi wanahamasishwa ili wawezi "kuwalinda watoto wao wasiathiriwe na maovu yanayoendelea katika jamii.

Hivi karibuni wagonjwa na wahudumu wa ugonjwa wa saratani waliandamana jijini Nairobi kuishinikiza serikali kuondoa gharama kubwa za matibabu kwa ugonjwa huo.

Wagonjwa na wauguzi walioandamana pia walimtaka rais Uhuru Kenyatta atangaze saratani kuwa ni janga la kitaifa.

Walisema iwapo hatua hiyo itaidhinishwa basi rasilmali nyingi zitaelekezwa katika kutoa matibabu ya nafuu na yanayowafikia wote nchini pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu na kuweka vifaa hospitalini katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Hofu dhidi ya chanjo

Chanjo zimesaidia kuokoa maisha mamilioni ya watu duniani kote katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, zimekuwa ni hakikisho kwa makuzi salama ya watoto na afya bora kwa watu wazima.

Hata hivyo, wataalamu wamebaini hali ya ongezeko la kukataa kutumia chanjo katika baadhi ya maeneo duniani.

Shirirka la Afya Dunia (WHO) lipo katika tahadhari kubwa ya hali hiyo kiasi cha kuorodhesha ongezeko hilo kama moja ya mambo 10 yanayohatarisha afya ya ulimwengu kwa mwaka 2019.

Hofu dhidi ya chanjo, kwa mfano nchini Marekani ilisababisha mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa ukambi ay surua mika 25 iliopita.

Wakati Kenya inawalenga watoto wasichana kupata chanjo dhidi ya HPV, nchi kama Australia pia inawalenga wavulana katika juhudi ya kutokomeza kabisa virusi hivyo vinavyosababisha saratani.

Kwa sababau virusi vya HPV husambazwa kupitia ngono, kuwapa chanjo wavulana kutapunguza kuenea kwa virusi hivyo vinavyohusishwa na na 5% ya maradhi ya saratani.

Tafita kadhaa nchini Australia zinzonesha kuwa chanjo ya HPV inatoa ulinzi imara dhidi ya saratani.

Uchunguzi wa saratani ya shingo ya uzazi nchini Australia inalenga kutokomeza ugonjwa huo kufikia mwaka 2035.

Gharama na upatikanaji wa chanjo hiyo hata hivyo bado ni changamoto kubwa nchini Keny.

Sio watu wengi wanaoweza kumudu gharama ya kufanyiwa uchunguzi wa mapema wa virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya shingo ya uzazi.

Gharama ya utibu saratani ya aina hiyo ni kati ya dolla 1,720 hadi $7,590 ikiwa mgonjwa hatafanyiwa upasuaji nchini Kenya.

Na endapo matibabu yatahusisha upasuaji basi gharama hiyo itapanda kwa kati ya dolla 6,720 hadi dolla 12,500 kwa mujibu wa shirika la kudhibiti saratani nchini Kenya .