Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania: Watu 60 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kulipuka
Watu 60 wamethibitishwa kufariki na wengine zaidi ya 65 kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kulipuka katika eneo la Msamvu mjini Morogoro, Mashariki mwa Tanzania.
Polisi wanasema watu hao walikuwa wakichota mafuta baada ya lori hilo kupinduka katika bara bara kuu mapema Jumamosi wakati ajali hiyo ilipotokea.
Bado chanzo cha ajali hiyo hakijathibitishwa lakini kuna hofu huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.
"Hali ni mbaya sana. Watu wengi wamefariki, hata wale waliokuwa hawateki mafuta kwasababu eneo hili ni lina shughuli nyingi," alisema Daniel Ngogo, aliliyenukuliwa na Shirika la Habari la.
Kamanda wa Polisi wa Morogoro Wilbroad Mtafungwa amenukuliwa na Gazeti la Mwananchi akithibitisha tukio hilo.
Inahofiwa kuna miili mingine ambayo imebanwa chini ya lori hilo baada ya moto kulipuka.
Walioshuhudia ajali hiyo wanasema waendesha piki piki ndio walioathirika zaidi na mkasa huo.
Picha zilizo chapishwa katika mitando ya kijamii zinaonesha miili kadhaa ya watu iliyoteketea kupita kiasi ikiwa imetapakaa katika eneo la tukio.
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amenukuliwa katika taarifa kutoka kwa Ikulu akielezea masikitiko yake kuhusu mkasa huo.
''Nimesikitika sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliofariki katika ajali hii, natoa pole kwa wale wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za marehemu wote'' ilisema taarifa hiyo.
Mmoja wa manusura wa mkasa huo alisikika akisimulia kilichojiri.
"Hapa nilikuta watu wanang'ang'ania mafuta na watu walikuwa bizee kuchota mafuta na hawaelewi haya ni mafuta au maji. Katika huo mshangao sasa mimi nasikia moto umelipuka. Moto ulipozuka tukaanza kukimbiana, kila mmoja anajiokoa kivyake vyake, kufikia hapo nimeanguka chini nikaanza kutambaa kwa magoti nikufanikiwa kuondoka ." alisema manusura huyo
Baadhi ya watu wanatumia mitandao ya kijamii kuelezea masikitiko yao na kuwapa pole Watanzania haswa wakaazi wa Morogoro waliohusika katika ajali hiyo.
Mji wa Morogoro ni moja ya njia kuu za malori yanayobeba shehena ya mizigo na mafuta kutoka bandari ya Dar es Salaam.
Bado haijafahamika lori hilo lilikuwa linamilikiwa na kampuni gani ya usafirishaji na iwapo lilikuwa linaenda nje ya Tanzania ama la.
Matukio yaliopita ya ajali ya lori ya mafuta kulipuka
2009: Kenya iliwahi kukabiliwa na mkasa kama huu ambapo watu zaidi ya 100walifarikibaada ya lori la mafuta lililopata ajali kulipuka katika barabara ku wakati watu walikuwa wakijaribu kuchota mafuta.
2015: Karibu watu 70 walifariki huko mashariki mwa Nigeria baada ya lori la kubeba mafuta kushika moto.
2018: Takriban watu 50 walifariki baada ya trela ya kusafirisha mafuta kugongana na gari ndogo katika barabara kuu magharibi kwa Jamhuri ya Demokrsi ya Congo.