Benki ya Dunia yawezesha kujengwa kwa kiwanda cha kisasa cha tembo Kenya

Wateja wakipimiwa pombe ya mnazi
    • Author, John Nene
    • Nafasi, BBC Swahili

Habari njema kwa wa watu wa Pwani nchini Kenya. Waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi katika kaunti ya Kilifi Luciana Sanzua ametangaza ujenzi wa kiwanda cha pombe ya mnazi utaanza baadae mwaka huu eneo la Mtwapa.

``Tayari mbegu maalum iliyoboreshwa kwa kazi hii tumeileta kutoka India, iko katika kituo chetu cha mafunzo ya ukulima (Agriculture Training Centre) huko Mtwapa,'' anasema Sanzua.

``Mnazi wa sasa unatoa nazi 150 lakini mbegu ambazo tumeleta zitatoa nazi 500 kwa msimu, na kabla tuanze kuzipanda lazima mbegu hizo zipitie utafiti kwa sababu ni ngeni kwetu. Ikionekana haina magonjwa ama wadudu wakutuletea madhara kazi inaanza ya upanzi wa miche hiyo.''

Sanzua anasema kaunti ya Kilifi inashirikiana na Benki ya Dunia (World Bank) na muungano wa wakulima kwa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachogharimu dola 600,000.

Waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi katika kaunti ya Kilifi Luciana Sanzua

``Kupitia kiwanda hicho,'' anasema Sanzua,''tutaweza kuongeza ubora wa kileo cha mnazi. Kwa siku moja kitaingiza kama dola milioni 15 na kwa mwezi dola milioni 450. Hapo hapo tutapata ethanol inayoweza kutumika kwa mambo kadhaa, sukari, sukari guru na asali.''

Kulingana na Sanzua, jina la kinywaji hicho halitabadilika kwa sababu wanataka kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa jina la Mnazi. La kufurahisha zaidi kwa mradi huo ni ajira kwa vijana wa kaunti ya Kilifi na Pwani kwa jumla.

Pombe hiyo ambayo hugemwa, pia hufahamika kwa jina la tembo.

``Ajira kote nchini Kenya imekua ni donda sugu. Afya ya watoto wetu kwa miaka mingi imedhoofika kwa matumizi ya mihadarati lakini kiwanda hiki kitawapa kazi vijana hao. Tuna wasomi Kilifi lakini shahada zao zimekua hazina faida kwa sababu ya ukosefu wa kazi, nao pia watafaidika,'' anasema Sanzua.

Kwa miaka mingi, pombe hii ya mnazi imekua na umaarufu wake pwani ya Kenya kwani mbali na kuburudisha baadhi yao pamoja na watalii ni kitega uchumi kwa wengi wao.

Pombe ya mnazi ikipimwa kwenye bilauri

Mama Gahaha Mwinyi ni miongoni mwa wauzaji wa kinywaji hicho sehemu ya Mbudzi Mitamboni kaunti ya Kilifi.

``Nimeuza pombe ya mnazi kwa zaidi ya miaka 20,'' anatueleza mama huyo,''mtoto wangu mmoja sasa yuko Chuo Kikuu na mwingine sekondari, wote nawasomesha kwa sababu ya hii biashara yangu.Mimi sinywi lakini nimefaidika sana.''

Wagemaji nao wanafaidika mno kwa uuzaji wa pombe hii ya mnazi, na ujenzi wa kiwanda hicho utakua ni baraka kubwa kwao kwa sababu watafaidika zaidi.

``Mimi nimesomesha watoto wangu wote kutokana na kazi ya ugemaji,'' anaeleza Mzee Vue Taura ambaye anasema kiwanda hicho kitaleta faida kubwa kwao ingawaje kwa umri wake sasa hawezi kazi hiyo ya ugemaji.

Wanaume wakipata kinywaji

``Ni kazi ambayo ina athari zake,'' anasema Taura,'' kuna siku niliteleza nikaanguka hadi chini nikiwa juu ya mti wa mnazi. Sikuumia sana hata hivyo.''

Mwanawe Taura, Francis Vue, anakubaliana na asemayo baba yake kuhusu manufaa ya ugemaji kwa familia yao na kinywaji cha mnazi.

``Kama si kazi hii ya baba hatungesoma lakini sasa tuko sawa, na kiwanda kikianzishwa kaunti ya Kilifi itabadilika. Vijana wengi watapata kazi,'' anasema Francis Vue.