Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
AFCON: Shabiki atembea kilomita 10,000 kushabikia mechi ya soka
Muuguzi mmoja raia wa Zimbabwe ametembea kutoka Cape hadi Cairo kushabikia michuano ya Kombe la Afrika.
Alvin "Aluvah" Zhakata alitarajia kushuhudia mechi ya ufunguzi ya kombe la taifa bingwa Afrika nchini Egypt Juni 21, baada ya timu ya taifa ya Zimbabwe kufuzu kushiriki mashindano hayo.
Lakini alikosa mechi hiyo kwasababu safari yake ya kihistoria ilichukua muda mrefu kuliko jinsi alivyotarajia.
Hata hivyo aliwashukuru watu wote waliofuatilia safari hiyo katika mtandao wake wa Twitter, ambako amepata umaarufu mkubwa- na kuelezea kuwa kamati ya shirikisho la soka barani Afrika linalosimamia wa michezo hiyo imempatia tiketi ya kuhudhuria mechi ya finali ya siku ya Ijumaa kati ya Algeria na Senegal.
'Afrika sio rafiki kwa Waafrika'
Mtu huyo wa miaka 32 aliyefika mji mkuu wa Misri, Cairo wiki iliyopita baada ya kutembea kilomita 10,000 kwa siku 44, wakati mwingine akiomba madereva wa mabasi na malori wamsaidie kufupisha safari yake ameelezea kuwa hana la kujutia kuhusu safari hiyo licha ya uchovu aliyopata.
Pia anasema kuwa amejifunza mengi kuhusu tabia yake na Afrika.
"Nilikua nikidhani mimi sio mvumilivu - lakini nimegundua kuwa naweza kuwa mvumilivu kupita kiasi," aliimbia BBC.
Kitu kingine alichogundua katika safari hiyo ni kuwa "Afrika sio rafiki kwa Waafrika"- linapokuja suala la mipaka na hati ya usafiri.
Watu wengi waliozuru taifa hilo kutoka Ulaya na Marekani walipewa umuhimu zaidi, alisema.
"Ada ya visa inayotozwa na baadhi ya mataifa ya Afrika ni ghali kuliko ada ya visa anayotozwa mtu anayesafiri Ulaya - na mtu huchukua muda mrefu zaidi.
"Naamini tunahitaji kuwa na Afrika ambayo haina mipaka."
Alianza safari yake tarehe 27 mwezi Mei kupitia Afrika Kusini, Zimbabwe, Zambia,Tanzania, Kenya, Ethiopia, Sudan na Misri.
'Tulitaka kuandikisha historia'
Alianza safari hiyo akiwa na rafiki yake Botha Msila, mwanasoka wa Afrika Kusini, ambaye anaishi karibu na Cape Town.
"Tulitaka kuandikisha historia kuwa watu wa kwanza kutembea kutoka Cape hadi Cairo kuwa kutumia barabara ili kuhudhuria mihcuano hiyo," Zhakata alisema.
Muuguzi huyo wa kujitegemea ambaye anaishi mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, amekuwa akiwasiliana na Msila tangu alipojuana nae katika fainali ya michuano ya Cosafa Cup nchini Afrika Kusini miaka miwili iliyopita.
Alimwambia jinsi ilivyosafiri peke yake mwaka 2016 kwa kutumia barabara kutoka Harare hadi Kigali kushabikia Warriors katika michuano ya Afrika nchini Rwanda.
Baada ya hapo walichangisha nauli y a kurudi kutoka kwa wasamaria wema kwa kutumia hashtag ya #CapeToCairo kujionea maendeleao ya bara letu.
Lakini wawili hao walitengana baada ya Msila kurejea alipofika mpaka wa Kenya-Ethiopia kwasababu hakuwa na uwezo wa kupata visa.
Ethiopia hupokea maombi ya visa kupitia mtandao kwa wasafiri wanaotumia barabara.
Japo alikuwa na pesa taslimu walihitaji kulipa ada hiyo kupitia mfumo wa kielektroniki anawlifanikiwa kufanya hivyo.
Lakini ombi lao lilicheleweshwa kwa siku tano zaidi.
"Kwa bahati mbaya mitambo yao ilikumbwa na hitilafu kwasababu huduma ya intaneti ilikuwa imezimwa kote nchini ili kuzuia wizi wa mitihani," alielezea Zhakata.
Msila, ambaye anafahamika kwa safari zake nchini Afrika Kusini kushabikia timu ya taifa ya Bafana Bafana na klabu yake ya Bloemfontein Celtic, hakuwa na budi kusitisha safari yake ya Cairo na kurejea mjini Nairobi Kenya.
Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini lilimuokoa kwa kumlipia tiketi ya ndege kutoka Nairobi hadi Cairo.