Jaguar kusalia rumande akisubiri uamuzi kuhusu ombi lake la dhamana

Chanzo cha picha, JAGUAR/FACEBOOK
Mbunge wa Kenya aliyekamatwa kwa kutoa maneno ya chuki dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni atabaki rumande kwa siku ya pili wakati dhamana yake ikishughulikiwa.
Polisi walimfikisha Charles Njagua Kanyi maarufu Jaguar mahakamani hii leo lakini hakusomewa mashtaka.Kwa mujibu wa Mahakama, uchunguzi unafanyika kuhusu madai ya kupanga kuvamia mali za watu na kuwashambulia raia wa kigeni walio nchini Kenya.
Muendesha mashtaka ameitaka mahakama kuendelea kumshikilia mshukiwa kwa majuma mawili wakati wakimalizia uchunguzi wao.
Mahakama itatoa uamuzi kuhusu ombi la dhamana ya Jaguar kesho.
Bwana Kanyi alikamatwa jana kwa madai kuwa alitoa kauli za kichochezi dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni katika soko kuu la Gikomba nchini Kenya.
alipokuwa akizungumza kuhusu kuwepo kwa ushindani wa kibiashara na wageni usio na usawa, alisema: ''Wakenya ni sharti wafanye biashara zao bila kushindana na watu kutoka mataifa mengine. Raia wa Pakistan wametawala biashara za kuuza magari nchini humu, Watanzania na Waganda wanatawala katika masoko yetu. Tunasema imetosha iwapo hawatarajeshwa nyumbani katika saa 24 tutawashika na kuwapiga na hatuogopi mtu yeyote'', alinukuliwa akisema.

Chanzo cha picha, JAGUAR /FACEBOOK
Kauli hiyo iliibua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii.Hisia tofauti zimeibuka kufuatia matamshi aliyotoa mbunge wa Kenya dhidi ya wachuuzi wa kigeni wanaoendehsa biashara nchini Kenya.
Katika kanda ya video iliosambazwa nchini Kenya na katika nchi jirani Tanzania, mbunge huyo Charles Njagua Kanyi, alisema hawatokubali watu wa nje waje kuendesha biashara nchini.
"...Ukiangalia soko zetu, Watanzania na Waganda wamechukua biashara zetu, sasa sisi tumesema enough is enough".
Jaguar ni nani?
Charles Njagua Kanyi al maarufu Jaguar ni mwanamuziki, mwanasiasa na mjasiliamali na inaaminiwa kuwa mmoja wa wasanii tajiri nchini Kenya na katika eneo la Afrika Mashariki
Alizaliwa katika familia ya maskini katika familia ya watoto watatu. Jaguar alisomea katika shule ya msingi mjini Nairobi na akiwa na umri wa miaka 11 alifiwa na mama yake ambaye wakati huo alikuwa ndiye mlezi wake pekee.
Alilazimika kufanya kazi za vibarua ili kujikimu kimaisha na moja ya kazi alizozifanya ilikuwa ni kazi ya ukondakta wa mabasi ya abiria, maarufu daladala au matatu, na kwa msaada wa marafiki aliweza kumaliza shule.
Maisha ya kimuziki:
Rekodi Jaguar ya kwanza ilifanyika namo mwaka 2004 na baadae akajiunga na kampuni ya muziki ya Afrika mashariki Ogopa Deejays mnamo mwaka 2005 ambapo na miziki mmoja baada ya mwingine miongoni mwake "kigeugeu." Uliovuma sana na kupokea tuzo nyingi.

Chanzo cha picha, JAGUAR /FACEBOOK
Katika kazi yake ya Muziki Jaguar ameweza kupata tuzo mbali mbali.
Mnamo mwaka 2013 Jaguar alianza kurekodi katika Studio kuu Switch Studios iliyoanzishwa na mmoja wa wazalishaji wa muziki wake wa muda mrefu, Philip Makanda zamani akiwa katika Ogopa Deejays.
Miongoni mwa nyimbo nyingine zilizompatia umaarufu ni Kioo na One centimeter, na kufanya ushirikiano wa kimziki( Kolabo) na wasanii maarufu wa muziki badarani Afrika kama Iyanya kutoka Nigeria, na Mafikizolo kutoka Afrika Kusini katika singo "Going Nowhere"












