Chanjo ni nini, zinafanya kazi vipi na kwa nini baadhi wana mashaka nazo?

CHANJO

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanjo zimesaidia kuokoa maisha mamilioni ya watu duniani kote katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, zimekuwa ni hakikisho kwa makuzi salama ya watoto na afya bora kwa watu wazima.

Hata hivyo, wataalamu wamebaini hali ya ongezeko la kukataa kutumia chanjo katika baadhi ya maeneo duniani.

Shirirka la Afya Dunia (WHO) lipo katika tahadhari kubwa ya hali hiyo kiasi cha kuorodhesha ongezeko hilo kama moja ya mambo 10 yanayohatarisha afya ya ulimwengu kwa mwaka 2019.

Chanjo

Chanzo cha picha, BBC Sport

Chanjo ziligundulika vipi?

Kabla ya uwepo wa chanjo, dunia ilikuwa si sehemu salama sana, na mamilioni ya watu walikuwa wakipoteza maisha kila mwaka kwa magonjwa ambayo sasa yanaweza kudhibitika.

Wachina ndio walikuwa watu wa mwanzo kugundua sampuli ya chanjo katika karne ya 10, kwa kuwaweka karibu na sehemu za makovu za watu ambao wameathirika na magonjwa mbalimabli ili kuwajengea kinga ya mwili.

Karne nane mbele, daktari Mwingereza Edward Jenner alibaini namna gani wakamua maziwa walipata ndui ya ng'ombe ambayo haikuwa hatarishi, lakini ilikuwa nadra kwao kupata ndui ya binadamu ambayo ni hatari.

Ndui (ya binadamu) ilikuwa ni ugonjwa hatari zaidi wa kuambukiza, ambao uliua mpaka 30% ya wale ambao waliuugua.

Wale ambao walipona aghlabu walibaki na makovu mengi ama kupofuka.

Mwaka 1796 Jenner alifanya majaribio akimtumia mvulana wa miaka minane, James Phipps.

Daktari huyo alimpaka mtoto huyo majimaji kutoka kwenye kidonda cha ndui ya ng'ombe, na baada ya muda mfupi akaonesha dalili za maambukizi.

Baada ya kupona kabisa ugonjwa huo, daktari Jenner alimuwekea majimaji kutoka kwenye kidonda cha ndui (ya binadamu), lakini hakupata maambukizi.

Ndui ya ng'ombe ilimjengea chanjo dhidi ya ndui ya biadamu.

Mwaka 1798, matokeo ya majaribio hayo yalichapishwa na neno la Kingereza la vaccine (chanjo) - likabuniwa kutokana na neno la Kilatini la vacca - ambalo tafsiri yake kwa kiswahili ni ng'ombe.

Yapi mafanikio ya chanjo?

Chanjo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti maafa yaliyokuwa yakisababishwa na magonjwa na magonjwa mbalimbali katika kipindi cha miaka 100 iliyopita.

Takribani wati milioni 2.6 walikuwa wakipoteza maisha kila mwaka kutokana na surua kabla ya chanjo ya kwanza ya ugonjwa huo kuanza kutumika kwenye miaka ya 60.

Chanjo zimewezesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na surua kwa asilimia 80 baina ya mwaka 2000 mpaka 2017, linabainisha Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

MMR

Ni miongo michache iliyopita ambao watu walikuwa wakigubikwa na hofu ya kupooza mwili ama kifo, kutokana na ugonjwa polio.

Leo hii, ugonjwa wa polio umebaki kidogo sana kuangamizwa kabisa duniani.

POLIO

Kwa nini baadhi ya watu wanapinga chanjo?

Mashaka juu ya chanjo yamekuwepo toka siku za mwanzo za ugunduzi wa chanjo zenyewe.

Kitambo, watu walikuwa wakisita kutokana na sababu za kidini, walikuwa wakiamini kuwa chanjo zilikuwa chafu ama najisi, ama walihisi kuwa walikuwa wakiingiliwa uhuru wao wa kufanya maamuzi kwa kulazimishwa chanjo.

Katika miaka ya 1800 kulishamiri kwa makundi ya kupinga chanjo nchini Uingereza, makundi ambayo yalikuwa yakipigia chapuo njia mbada za kudhibiti magonjwa, ikiwemo kutengwa kwa wagonjwa.

Miaka ya 1870, kundi la kwanza la kupinga chanjo lilianza nchini Marekani, baada ya kutembelewa na mwanaharakati wa Kiingereza, William Tebb.

Moja ya watu muhimu katika miaka ya hivi karibuni katika harakati dhidi ya chanjo ni bwana Andrew Wakefield.

Mwaka 1998, daktari huyo ambaye maskani yake ni jiji la London alichapisha ripoti ya uongo akihusianisha chanjo ya MMR na magonjwa ya tumbo na usonji.

MMR ni chanjo tatu kwa moja ambayo hupewa watoto kuwakinga na magonjwa matatu ya surua, matumbwitumbwi na rubella.

Japo chapisho lake lilikataliwa na Wakefield akafutiwa leseni ya udaktari nchini Uingereza, idadi ya watoto waliopatiwa chanjo hiyo ilishuka baada ya madai yake.

Mwaka 2004, idadi ya watoto 100,000 walipungua katika wale waliotarajiwa kupokea chanjo hiyo nchini Uingereza -hali ambayo ilipelekea ongezeko la surua nchini humo.

mtoto mwenye surua

Chanzo cha picha, Science Photo Library

Suala la chanjo linafanywa kuwa la kisiasa pia katika siku za hivi karibuni.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia Matteo Salvini anayaunga mkono makundi yanayopinga chanjo nchini humo.

Rais wa Marekani Donald Trump, bila ya kuwa na ushahidi wowote, anahusisha chanjo na ulemavu wa utindio wa ubongo, lakini hivi karibuni amewataka wazazi kupeleka watotot zao wakapate chanjo.

Utafiti wa kimataifa juu ya fikra za watu kuhusu chanjo umebainisha kuwa japo watu wengi hawana shida na chanjo, Ulaya kuna wengi ambao hawaamini sana katika chanjo, hususani katika nchi ya Ufaransa.

Ipi hatari ya kuzipa kisogo chanjo?

Pale ambapo idadi kubwa ya watu wanapopokea chanjo, inasaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa, na kwa namna nyengine husaidia kuwalinda wale ambao hawana kinga ama hawawezi kupata chanjo.

Hali hiyo hufahamika kama kinga ya pamoja, na pale inapovunjika, basi hatari yake huwa kubwa kwa watu wengi zaidi.

Wastani wa watu ambao inabidi wapatiwe chanjo ili kutengeneza kinga ya pamoja inatofautiana kulingana na ugonjwa, mathalani kwa surua ni zaidi ya asilimia 90 na polio ni zaidi asilimia 80.

Mwaka jana, jamii yenye msimamo mkali ya Kiyahudi katika eneo la Brooklyn, Marekani ilisambaza vipeperushi ambavyo vilikuwa vikihusisha chanjo na usonji.

Jamii hiyo hiyo ipo kwenye mlipuko mkubwa wa surua nchini Marekani ambao haujawahi kuripotiwa kwa miongo kadhaa.

surua

Chanzo cha picha, AFP

Daktari kinara wa chanjo wa England alitoa onyo mwaka jana kuwa watu wengi nchini humo wanadanganyika na taarifa za kupotosha juu ya chanjo zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Watafiti nchini Marekani wamebaini kuwa Urusi imekuwa ikituma taarifa za uongo kuhusu chanjo mtandaoni ili kuchanganya fikra za watu.

Wastani wa watoto ambao wanapokea chanjo zinazopendekezwa umebaki kuwa asilimia 85 kwa miaka kadhaa iliyopita, kwa mujibu wa WHO.

Shirika hilo linasema chanjo hudhibiti vifo kati ya milioni mbili mpaka tatu kila mwaka duniani.

Changamoto kubwa ya kutoa chanjo, na kuwa na viwango vidogo vya kinga zipo kwenye nchi ambazo zimegubikwa na matatizo ya kiusalama na mifumo mibovu ya utoaji wa huduma za afya zikiwemo Afghanistan, Angola na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

WHO pia imeeleza kuwa kujisahau ni moja ya changamoto kwenye nchi zilizoendelea - kwa lugha nyepesi, watu wamesahau ni athari za namna gani ambazo magonjwa yanaweza kusababisha kwenye jamii zao.