Sukari si lazima katika kikombe cha chai

Woman drinking tea

Chanzo cha picha, Getty Images

'Usihadaike na rangi, tamu ya chai sukari,' ni msemo maarufu wa Waswahili, lakini sasa wanasayansi wanautoa kasoro.

Iwe ni kifungua au kiamsha kinywa asubuhi ama wakati wa kufuturu, waweza kupata kikombe cha chai kisichokuwa na sukari na usikose uhondo.

Watafiti wanasema si lazima chai ijazwe sukari ili mtu aifurahie.

Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa wanywaji wa chai wanaweza kufurahia vikombe vyao bila sukari - na hilo limefanikiwa baada ya kubadili tabia taratibu kwa muda mrefu.

Wanasayansi pia wanasema si lazima kupunguza taratibu, hata kuacha kwa mkupuo pia ni suala linalowezekana.

Hata hivyo wanasayansi waliofanya utafiti huo wanasema wanahitaji ushiriki mkubwa zaidi wa watu ili kuyapa nguvu zaidi matokeo yao.

Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha London na Chuo Kikuu cha Leeds vyote vya ncini Uingereza wamechakata taarifa kutoka kwa wanaume 64 wanaopendelea kunywa chai kwa sukari nyingi.

Cup of tea

Chanzo cha picha, Getty Images

Washiriki wa utafiti huo waligawanywa katika makundi mawili, wale ambao waliacha kido kidogo na wale walioacha ghafla.

Matokeo ya utafiti yakaonesha kuwa hata ukiacha kutumia sukari, bado waweza kufurahia chai yako.

42% ya walioacha taratibu wameacha moja kwa moja kutumia sukari, wakati 36% ilikuwa ni ya wale ambao wameacha ghafla.

Timu hiyo ya watafiti imehitimisha kuwa: "Kupunguza sukari kwenye chai wala haiathiri utamu wake, na hilo linaashiria kuwa mabadiliko ya tabia kwa muda mreu juu ya jambo hilo yanawezekana."

Watafiti hao pia wameongeza kuwa njia zo za kujizuia zinaweza kutumiwa katika kupunguza matumizi ya sukari kwenye vinywaji vingine pia.

Matokeo ya utafiti huo yalifanyiwa kazi mwezi Aprili jijini Glasgow, Uskochi katika Mkutano wa Wataalamu wa Bara Ulaya dhidi ya unene wa kupitiliza.