Magufuli amteua Doto Biteko kuwa waziri mpya Tanzania, amhamisha Anjellah Kairuki

Magufuli

Chanzo cha picha, IKULU, Tanzania

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amempandisha cheo Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko kuwa waziri mpya wa madini.

Rais amechukua hatua hiyo baada ya kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri Jumanne ambapo alifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi za Serikali.

Aliyekuwa Waziri wa Madini Anjellah Kairuki ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji ambao ni wadhifa mpya.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza uteuzi huo, alisema Dkt Magufuli aliamua kumteua Waziri anayeshughulikia masuala ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza msukumo na kuimarisha usimamizi wa masuala ya uwekezaji.

Hivi majuzi, Rais Magufuli aliamrisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kihamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wizara ya madini, ambayo awali ilikuwa na manaibu waziri wawili, sasa itakuwa na naibu waziri mmoja ambaye atakuwa Dkt Stanslaus Nyongo.

Bw Biteko ni nani hasa?

Doto Mashaka Biteko alizaliwa mwaka 1978 na amekuwa mbunge wa jimbo la Bukombe katika mkoa wa Geita kaskazini magharibi mwa Tanzania kuanzia mwaka 2015.

Alisomea shule ya msingi ya Nyaruyeye na kisha akajiunga na shule ya sekondari ya Sengerema na baadaye Chuo cha kiufundi cha Butimba.

Alisomea stashahada yake katika CHuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Morogoro na baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha St Augustine ambapo alisomea shahada ya ualimu.

Alihitimu na shahada ya pili (uzamili) kutoka chuo kikuu hicho cha St Augustine mwaka 2013.

Aidha, alipata cheti cha usimamizi (menejimenti) katika Chuo Kikuu cha Renmin cha China.

Alianza siasa mapema na chuoni mwaka 2007 alikuwa mwanachama wa kamati tendaji ya Chama cha Mapinduzi katika SAUT.

Alichaguliwa mbunge mwaka 2015 na akawa mwenyekiti wa kamati ya kawi na madini, wadhifa ambao aliushikilia hadi mwaka 2018.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM jijini Dar Es salaam kikiendelea Desemba mwaka 2018

Chanzo cha picha, IKULU, Tanzania

Maelezo ya picha, Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM jijini Dar Es salaam kikiendelea Desemba mwaka 2018

Wakuu wengine walioteuliwa ni:

  • Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Nyamuhanga alikuwa Katibu Mkuu Ujenzi, na anachukua nafasi ya Mhandisi Mussa Iyombe ambaye amestaafu.
  • Dkt. Zainabu Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia afya). Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Chaula alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (afya).
  • Mhandisi Elius Mwakalinga kuwa Katibu Mkuu Ujenzi. Kabla ya uteuzi huo, Mwakalinga alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na anachukua nafasi ya Mhandisi Nyamuhanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu TAMISEMI.
  • Bi Dorothy Mwaluko kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji). Kabla ya Uteuzi huo Bi. Mwaluko alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
  • Dkt Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya). Kabla ya uteuzi huo Dkt. Gwajima alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
  • Dkt. Francis K. Michael kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Francis K. Michael alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
  • Dkt. Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Ulisubisya alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (akishughulikia afya). Kituo cha kazi cha Dkt. Ulisubisya kitatangazwa baadaye.
  • Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera. Kabla ya Uteuzi huo Prof. Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Athumani Diwani Msuya ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Viongozi hao wataapishwa Jumatano saa tatu na nusu asubuhi katika ikulu ya Dar es Salaam.

Rais Magufuli pia ameifuta nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa Bi. Immaculate Ngwalle ambaye amestaafu.

Aidha, amefanya uamuzi wa kufungua Ubalozi Mpya wa Tanzania nchini Cuba. Balozi wa Tanzania nchini Cuba atateuliwa baadaye.