Waziri Augustine Mahiga "Misingi ya haki za kibinadamu hazifananishwi na misimamo ya kitamaduni"

Tanzania imekuwa ikifanya mazungumzo na baadhi ya mataifa ya Ulaya ambayo kwa siku za hivi karibuni yamekuwa yakiionyeshea kidole nchi hiyo kuwa inakiuka haki za binadamu.
Akizungumza na BBC Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki Augustine Mahiga amesema mazungumzo yamekuwa mazuri, na kusisitiza kutofautiana huko kwa mitazamo na baadhi ya mataifa hayo kuhusiana na suala la haki za binadamu kulitokana na utofauti wa tafsiri ya misingi ya haki za binadamu.
Waziri Mahiga amekiri kuwepo kwa kutoelewana katika suala hilo na ameeleza kwamba sasa wameelewa.
"Mara nyingi watu wanapozungumzia suala la haki za binadamu wanapiga picha kwa mara moja bila kutazama mazingira yote, bila kutazama limetokana na nini na limetokea wapi na kwa nini suala hilo limezungumzwa?
Hapa katikati kumekuwa na masuala mbalimbali ambayo hayakufafanuliwa vizuri, misingi ya haki za kibinadamu huwezi kuchanganya na utamaduni wa nchi, huwezi kuchanganya na sheria za nchi na kuchanganya na misimamo ya kidini na Imani za watu."
Waziri huyo ameongeza kwa kusema kwamba serikali imefanya mazungumzo na nchi kama Norway na wameelewa bila kutishia chochote na hata kusema kitu chochote hadharani.
Aidha katibu mkuu wa Denmark amekuja pia ili kujadili suala hilo.
Chanzo cha Tanzania kutoeleweka na baadhi ya mataifa

Chanzo cha picha, MAKONDA INSTAGRAM
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda aliunda kamati maalum ya watu 17 ili kuhakikisha kuwa watu wanaofanya biashara chafu za ngono wanachukuliwa hatua za kisheria.
Makonda alizionya na kutoa angalizo kwa mashirika ya haki za binadamu kuwa Tanzania ina tamaduni zake na ushoga ni kesi ya jinai kwa mujibu wa kifungu cha 154 ambacho kinasema mtu yeyote ambaye anamuingilia mtu yeyote kinyume cha maumbile au, anamuingilia mnyama kimwili au anamruhusu mwanaume kumuingilia yeye mwanaume au mwanamke kinyume cha maumbile, atakuwa ametenda kosa, na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha na wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka thelathini .
Serikali ya Tanzania imejitenga na kampeni ya kuwakamata na kushtaki mashoga inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliyotolewa Jumapili, Novemba 4 inadai kampeni hiyo ni mawazo binafsi ya Makonda na si msimamo rasmi wa serikali.
"Serikali ya Tanzania ingependa kufafanua kwamba hayo ni mawazo yake (Makonda) na si msimamo wa Serikali."
Katika taarifa hiyo, serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa ambayo imeisaini na kuiridhia.












