Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Deepika Padukone na Ranveer Singh: India yasherehekea harusi ya Bollywood
Nyota wa Bollywood Deepika Padukone na Ranveer Singh wamefunga pingu za maisha katika hoteli moja ya kifahari nchini Italia.
Majina ya wachumba hao yalitanda katika mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter huku mashabiki wengi wakiwatakia heri njema.
Waigizaji hao wamehusika katika filamu tatu pamoja, zikiwemo zilizopata umaarufu mkubwa Bajirao Mastani na Padmaavat.
Jarida la Forbes linaripoti kuwa wanandoa hao wamepata faida ya $21m katika kipato cha pamoja mwaka jana.
Harusi ilifanyika Jumatano, siku iliyo kumbukumbu ya walipoigiza filamu yao ya kwanza pamoja mnamo 2013 - Goliyon Ki Rasleela Ram-Leela.
Licha ya kwamba waandishi hawakualikwa kwenye harusi hiyo, picha za sherehe za kabla ya harusi zilifichuka katika majarida ya burudani na magazeti.
Watu wamekuwa wakizitafuta picha hizo pakubwa ambazo huenda zimesambazwa na wageni waliohudhuria sherehe katika mitandao yao ya kijamii - inaarifiwa wapenzi hao waliwapiga marufuku wageni waalikwa kuweka chochote kuhusu harusi hiyo katika mitandao.
Uvumi kuhusu kuchumbiana kwa waigizaji hao nyota ulianza kusambaa miaka 6 iliyopita, lakini hawakulithibitisha hilo wazi mpaka mapema mwaka huu.