Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanza: Kibao kipya cha nyota Rayvanny na Diamond Platnumz chafungiwa na Basata
Kibao kipya kiitwacho, Mwanza, kilichotolewa na wasanii mashuhuri Tanzania Rayvanny na Diamond Platnumz kimepigwa marufuku na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Novemba 12 Katibu Mtendaji wa Basata Godfrey Mngereza, sababu kuu ya kufungiwa wimbo huo ni ukiukwaji mkubwa wa maadili ya Kitanzania kwa "kutumia maneno yanayohamasisha ngono."
Basata pia imeonya vyombo vya habari, na watu binafsi kutoutumia, kuucheza ama kuusambaza wimbo huo kwa namna yoyote ile.
"Baraza linatoa onyo kali kwa msanii Rayvanny, Diamond Platnumz pamoja na uongozi wa Wasafi Limited kufuata sheria, kanuni na taratibu wakati wa kuandaa kazi za sanaa. Aidha Baraza limesikitishwa na kitendo hiki ambacho kimefanywa kwa makusudi," imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mngereza.
Wimbo huo wa Mwanza ulitolewa rasmi jana na tayari ulishavutia maelfu ya watazamaji kwenye mitandao ya kijamii. Wasanii hao wametakiwa kufuta kibao hiko katika kurasa zote ambazo walisambaza.
Basata wamekuwa mstari wa mbele nchini Tanzania kufungia nyimbo ambazo wamekuwa wakidai zinaenda kinyume na maadili. Katika miaka ya hivi karibuni, nyimbo ambazo zimeonekana zikiukosoa utawala wa Rais John Magufuli pia zimekuwa zikichukuliwa hatua kali nchini Tanzania.
Mwezi Juni mwaka huu, Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu alitangaza mpango wake wa kulishtaki baraza hilo baada ya kuufungia wimbo wake.
Basata ilitangaza kufungiwa kwa wimbo mpya wa Sugu unaoitwa 219 kwa madai kuwa una ujumbe wenye uchochezi. Mpaka sasa bado Sugu hajawasilisha suala hilo mahakamani.
Diamond si mgeni wa kufungiwa nyimbo zake na Basata, mwezi Februari vibao vyake viwili Hallelujah (uliomshirikisha Morgan Heritage ) na Waka Waka (uliomshirikisha Rick Ross) vilifungiwa.
Wakati huo Diamond alikuwa katika fungu moja na wasanii wengine 10 ambao walichukuliwa hatua hizo na Basata.
Nyimbo mbili za Ney wa Mitego, jina lake halisi Emmanuel Elibariki - Pale kati Patamu na Maku Makuz - pia zimefungiwa.
Mwanamuziki Roma Mkatoliki ambaye jina lake halisi ni Abernego Damiani naye amefungiwa wimbo wa Kibamia.
Wimbo wa Amani Hamisi maarufu kama Manifango wa Hainaga Ushemeji pia umefungiwa, sawa na I am Sorry JK wake Nikki Mbishi ambaye jina lake halisi ni Nicas John Mchuche.
Nyimbo nyingine ni Tema mate tumchape (Hamad Ali maarufu Madee), Uzuri Wako (Juma Mussa Mpolopoto maarufu Jux), Nampa Papa (Gift Stanford maarufu Gigy Money) na Nampaga (Barnaba Elias maarufu Barnaba).