Ni kwa nini inachukua muda kuitikia mikasa kama wa MV Nyerere

Chanzo cha picha, MSEMAJI WA SERIKALI TANZANIA
Hadi sasa jumla ya miili ya watu 224 imeopolewa na watu wengine 41 wakiokolewa wakiwa hai katika ajali hiyo ya kivuko cha MV Nyerere.
Serikali ya Tanzania imesema itaunda tume ya uchunguzi itakayohusisha wataalamu na vyombo vya dola kuchunguza kwa kina chanzo cha ajali hiyo na tayari maafisa kadhaa wa serikali wamekamatwa kufuatia tukio hilo.
Wakati huo huo Rais wa Tanzania John Magufuli ametengua uteuzi wa mkurugenzi wa bodi ya mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) na kuivunja bodi hiyo.

Watu wanatoa maoni gani?
"Sio kutoa pole ya 500,000 tu haitoshi serikali walipe fidia kwa ndugu wa marehemu maana kuna watu walikuwa wanawategemewa na hakuna fidia ilinganayo na maisha ya watu tunaeza ita kifuta jasho," mchangiaji mmoja aliandika kwenye mtandao Facebook
Pia kunao wanaona haja ya Kuwepo kwa vyombo vya kushika doria wakati wa kusafiri ili ikiwepo ajali uokoaji unakuwa wa haraka.
Ni hatua gani zinastahili kufanywa kusaidia Manusura?
Akizungumza na BBC Mwenyekiti wa chama cha kutetea abiria Hassan Mchanjama anasema abiria wanaotumia feri wana haki sawa na za abiria yeyote ambaye anaweza kutumia usafiri kama wa barabara na wale waliopoteza maisha wanastahili kufidiwa.
Anasema kwa kuwa vyombo vya majini mara nyingi havina bima lakini chombo cha MV Nyerere kinamilikiwa na serikali kwa hivyo anayestahili kuwajibika zaidi ni hapa serikali yenyewe.

Chanzo cha picha, STEVE MSENGI
Ameongeza kusema kuwa kutokana na kuwa vyombo vya majini havina bima, serikali inastahili kuhakikisha kuwepo mfuko maalum wa kuwafidia abiria wanaopata madhara kama hayo, kuweza kufidiwa kwa kuwa mara unapata watu hawa wengi ni tegemeo kwenye familia, kwa hivyo bila ya kufanya hivyo umaskini utaendelea.

Chanzo cha picha, STEVE MSENGI
Pongezi kwa wavuvi waliowaokoa watu
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw John Mongella aliwapongeza wavuvi katika kijiji cha Bwisya, Kisiwani Ukata, Wilaya ya Ukerewe kwa jitiha zao katika kuwaokoa baadhi ya watu wajikuta kwenye ajali ya MV Nyerere.
Akizungumza wakati wa mazishi siku ya Jumapili Mongella alisema wavuvi waliwaokoa watu 40 mchana wa siku ambayo ajali ilitokea.
Feri hiyo iliyokuwa safarini kutoka Bogolora kwenda Ukara ilipindika Alhamisi mwendo wa saa saba na dakika nane.
Taarifa ilifikia ofisi ya mkuu wa mkoa mwendo wa saa nane na dakika kumi kwa mujibu wa Bw Mongella, "Wavuvi walitoa mashua zao na kubadilishana kwa zamu na wakati timu kutoka mwanza ilipowasili mwendo wa saa kumi na dakika 45, wavuvi kutoka kijiji walikuwa tayati wamewaokoa watu 40," alisema Mongella wakati akiwashukuru.

Pongezi sawa na hizo pia zilitoka kwake Waziri wa uchukuzi mhandisi Isack Kamwelwe. "Wakati niliwasili niliwakuta wavuvi wakishiriki katika shughuli ya uokoaji. Wamefanya kazi nzuri na serikali inawapongeza sana kwa hilo," alisema
Mambo gani unastahili kuzingatia unaposafiri kwa feri?
· Panga kuondoka mapema ili upate kuwasili wakati ingali bado mchana
· Zuia kusafiri wakati bahari au ziwa ni chafu au wakati hali ya hewa ni mbaya
· Kama unaabiri chombo ambacho unahisi kimebeba watu wengi kupita kiasi, shuka mara moja
· Mara unapo abiri, fahamu kuhusu sehemu zilizo katibu nawe. Hakikisha kuwa maeneo ya kutokea au kutorokea yako salama na pia hakikisha kuwa yako wazi.
· Hakikisha jaketi za uokozi ziko kwenye chombo, ziko wapi hasa na unaweza kuzikifikia wakati wa dharura?
· Vyombo vya kutangaza viko sawa kuweza kutangaza wakati kuna dharura?
· Wahudumu wa chombo wanaweza kuwasiliana na abiria kwa haraka?
· Kama unaamini kuwa sehemu fulani ya chomno haipo sawa, shuka mara moja na fanya mipango tofauti ya kusafiri.












