MV Nyerere: Tunayoyafahamu kufikia sasa kuhusu mkasa wa kuzama kwa kivuko wilaya ya Ukerewe, Mwanza, Tanzania

Kivuko kilichopewa jina MV Nyerere kilizama Alhamisi adhuhuri kikitokea bandari ya Bugolora katika kisiwa cha Ukerewe kuelekea katika kisiwa cha Ukara
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli amesema watu 131 wamethibitishwa kufariki kufikia sasa na watu waliookolewa ni 40, huku shughuli za uokoaji zikiendelea.
Ameagiza kuundwa kwa tume ya uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo na kusema kuwa wote waliochangia kusababisha ajali hiyo watachukuliwa hatua kali.
Rais pia ametangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa kuanzia Ijumaa ambapo pia ameamrisha kuwa bendera ya taifa ipepee nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia Jumamosi.
Tunafahamu nini kufikia sasa?
Rais Magufuli asema dereva aliyepaswa kuendesha MV Nyerere hakuwepo

Sasa imebainika kwamba nahodha wa kivuko cha MV Nyerere kilichozama Alhamisi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 130 hakuwepo katika feri hiyo wakati ilipozama.
Akihutubia taifa siku ya Ijumaa jioni rais wa Jamhuri ya Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa ana habari kwamba nahodha huyo alimwachia zamu ya kuendesha chombo hicho mtu ambaye hakuwa amepata mafunzo ya kazi hiyo.
Akizungumza moja kwa moja kupitia runinga, rais Magufuli amesema kuwa nahodha huyo tayari amekamatwa na polisi .
Aidha rais Magufuli ameagiza wale wote wanaohusika na operesheni za kivuko hicho kukamatwa ili kuhojiwa.
Waliofariki ni wangapi?
Idadi rasmi ya waliothibitishwa kufariki ni 131, kwa mujibu wa tangazo la Rais Dkt John Magufuli ambaye alilihutubiwa taifa kupitia runinga Ijumaa jioni. Baadaye taarifa kutoka ikulu ilitolewa ikithibitisha idadi hiyo. Waliookolewa wakiwa hai ni 40.
Alhamisi, miili iliyokuwa imeopolewa kutoka baharini ilikuwa 44, na watu 37 walikuwa wameokolewa wakiwa hai.
Pantoni ilikuwa imewabeba abiria wangapi?
Kuna taarifa za kukinzana kuhusu idadi hasa ya abiria waliokuwa kwenye feri hiyo. Taarifa za kwanza zilidokeza kwamba huenda ilikuwa imebeba hadi watu 400.
Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Kanali Lucas Maghembe alikuwa mwenyewe ametaja idadi hiyo mwanzoni alipokuwa anahojiwa na wanahabari baada ya tukio.

Kanali Maghembe alisema wakati huo kwamba wanakadiria watu walioweza kuogelea au kujiokoa walikuwa kama mia moja hivi.
Meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria kati ya 100 na 120 lakini mkuu huyo wa wilaya anasema ni vigumu kubaini hasa idadi ya abiria waliokuwemo.
Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Zitto Kabwe ametoa wito kwa serikali nchini Tanzania kutoa taarifa rasmi kuhusu idadi ya watu waliokuwa kwenye MV Nyerere ilipozama.

Chanzo cha picha, Steve Msengi
Bw Kabwe, ambaye ni mbunge wa Kigoma-Ujiji amesema ukosefu wa habari kuhusu idadi kamili ni dalili za ubaya wa sheria mpya ya takwimu nchini humo.
"Baadhi ya Watu wanasema kivuko kilikuwa na abiria kati ya 150 na 500. Ni muhimu Serikali itoe Taarifa rasmi ya idadi ya abiria waliokuwamo ili kuondoa sintofahamu ama Serikali iahidi kutoshtaki raia yeyote shuhuda kutoa makadirio ya Watu ili kuimarisha juhudi za uokoaji," amesema.
Kwa nini abiria wakawa wengi Alhamisi?
Alhamisi huwa ni siku ya gulio katika kisiwa cha Ukaya, yaani soko la wazi, na inaarifiwa watu wengi walikuwa wakisafiri na mizigo na bidhaa zao.
Hii ilichangia meli hiyo ambayo kawaida inafaa kuwabeba watu 100 hivi kuwabeba watu wengi kupita kiasi. Ni kawaida kwa kivuko hicho kuwabeba watu wengi Alhamisi.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, kivuko hicho cha Mv Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu.
Julai mwaka huu kilikuwa kimefungwa injini mpya baada ya ile ya awali kuanza kupata hitilafu. Gazeti hilo linasema MV Nyerere imekuwa ikihudumu eneo la Ukerewe tangu 2004.

Ajali ilitokea vipi?
Kanali Lucas Maghembe anasema mwendo wa saba unusu mchana, meli hiyo ilipokaribia kufika ufuoni, nahodha alipoanza kupunguza kasi ya meli, watu walikimbia upande mmoja wakitaka kuwa wa kwanza kuondoka kwenye meli hiyo.
Hilo lilisababisha uzito kuegemea upande mmoja na meli ikaanza kuinama na mwishowe kupinduka.
Iligeuka kabisa na kitako chake kikaangalia upande wa juu. Baadhi ya watu waliogelea na wengine kuokolewa kwa mitumbwi.
Uchunguzi hata hivyo unaendelea kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.
Miongoni mwa waliofariki ni nahodha na wafanyakazi watatu wasaidizi. Ni mhudumu mmoja aliyenusurika akiwa hali mahututi na alilazwa hospitalini.
Kanali Maghembe amesema iwapo itabainika kwamba kuna waliosababisha ajali hiyo, labda kwa kufanya hujuma, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana, akizungumza na gazeti la Mwananchi, alisema kivuko hicho kilizama wakati kikielekea katika Kisiwa cha Ukara.
Anasema kivuko hicho kiliondoka Bugolora saa 6 mchana na ilipofika saa nane kamili adhuhuri ndipo kikapinduka.
Kwa nini juhudi za uokoaji zikasitishwa Alhamisi usiku?

Chanzo cha picha, Reuters
Maafisa wa uokoaji walisitisha juhudi za uokoaji zaidi kutokana na giza mwendo wa saa mbili usiku. Kanali Maghembe anasema pia watu waliokuwa wakisaidia uokoaji kwa kutumia mitumbwi walikuwa wamechoka.
Juhudi rasmi za uokoaji zilianza mwendo wa saa kumi alasiri baada ya wataalamu wa uokoaji kuwasili kutoka Mwanza.
Kufikia wakati wa kusitishwa kwa juhudi za uokoaji, miili 44 ilikuwa imeopolewa, na watu 37 walikuwa wameokolewa wakiwa salama. 32 walilazwa hospitalini na saba walikuwa salama walikwenda nyumbani.
Kanali Maghembe anasema waokoaji walikuwa wanafanya uokoaji walikuwa pia wameingia ndani ya meli na kuchunguza wakabaini hakukuwa na dalili za watu kupatikana wakiwa hai. Giza lilikuwa linatatiza.
Magufuli amesema chochote?
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli alikuwa hajatoa tamko la moja kwa moja kuhusu mkasa huo Alhamisi lakini Ijumaa alilihutubia taifa kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo alitangaza siku nne za maombolezo.
Rais Magufuli ameagiza pia kuundwa kwa tume ya uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo na akaagiza pia wote waliohusika katika kusababisha ajali hiyo wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
"Taarifa za awali zimeonesha dhahiri kuwa kivuko cha MV Nyerere kilikuwa na idadi kubwa ya watu na mizigo kupita uwezo wake, kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi wa chanzo cha ajali hii, tunatarajia kuwa ataupeleka mahakamani," amesema.
Dkt Magufuli amemtuma Waziri wake Mkuu Kassim Majaliwa kwenda eneo la mkasa.
Awali ujumbe wake ulikuwa ni, kupitia Msemaji wa serikali ya Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Gerson Msigwa, aliyekuwa ametoa salamu za rambirambi kwa walioathiriwa na mkasa huo.
"Rais anatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na ajali. Rais anaomba Watanzania kuwa watulivu wakati juhudi za uokoaji zinaendelea na baadaye Serikali itaweza kutoa taarifa cha nini kitakachoendelea," alisema alipopiga simu Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)

Chanzo cha picha, Steve Msengi
Bw Msigwa pia alituma salamu za rambirambi kwa waathiriwa kwa niaba ya serikali Alhamisi jioni.
Aliandika kwenye Twitter: "Kwa niaba ya Serikali natoa pole kwa waliopoteza ndugu na jamaa katika ajali iliyohusisha kuzama pantoni ya MV Nyerere inayomilikiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) inayotoa huduma zake katika visiwa vya Ukerewe na Ukara."
"Serikali kupitia Temesa itaendelea kutoa taarifa zaidi wakati huu juhudi zikielekezwa kwanza katika shughuli za uokoaji na huduma nyingine za kibinadamu."
Baadaye Ijumaa, Bw Msigwa alipakia kwenye Twitter nukuu kutoka kwa Rais Magufuli aliyesema ameshtushwa sana na ajali hiyo.
"Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na ajali ya MV Nyerere, nawapa pole wote waliopoteza jamaa zao na nawaombea wote walionusurika kupona haraka, kwa wakati huu nawaomba tutulie wakati juhudi za uokoaji zinaendelea," amesema.

Chanzo cha picha, MSEMAJI WA SERIKALI TANZANIA
Kenyatta, Kagame na Odinga: Waliotuma salamu za rambirambi kutoka kanda hii
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli na Watanzania kwa jumla kutokana na mkasa huo.
Amesema Wakenya wako pamoja na "ndugu zao" Watanzania kipindi hiki kigumu.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, ametuma salamu za rambirambi kwa walioathiriwa na mkasa wa feri nchini Tanzania.
Amesema anaombolewa na Watanzania kipindi hiki kigumu na kumuomba Mungu awape nguvu wote walioathiriwa, pamoja na raia wote wa Tanzania.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Rais wa Rwanda Paul Kagame pia ametuma salamu za rambirambi kwa jamaa na wapendwa wa waathiriwa wa mkasa huo wa kuzama kwa kivuko Mwanza.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 3













