Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni kwanini Kagame akaamua kumuachia Victoire Ingabire?
Rais Paul Kagame wa Rwanda ametangaza kwamba hakushinikizwa na mtu yeyote kutoa msamaha na kumwachilia huru mwanasiasa wa upinzani Bi Victoire Ingabire.
Akihotubia bunge baada ya wabunge waliochaguliwa hivi karibuni kuapishwa rasmi, rais Kagame amesema msamaha aliotoa ndiyo njia aliyochagua ya kutatua matatizo na kujenga taifa hilo.
Rais Kagame amewaonya walioachiliwa huru kutuliza misimamo yao la sivyo wajikute tena gerezani.
Akihutubia bunge jipya mara tu baada ya kuapisha wabunge waliochaguliwa hivi karibuni, Rais Paul Kagame amegusia swala la msamaha aliotoa kwa wafungwa zaidi ya 2000 walioachiliwa huru mwishoni mwa wiki iliyopita.
Miongoni mwao mwanasiasa wa upinzani Victoire Ingabire na msanii Kizito Mihigo waliokuwa gerezani kwa hatia ya makosa ya uhaini.
Kiongozi huyo mkuu wa Rwanda amemuonya yeyote atakayeendelea kuwa na msimamo mkali kuwa atarudishwa gerezani.
"Hawa watu tuliowaachilia huru wakiwemo wale wanaofahamika nje kama nyota wa kisiasa, walipotoka nje walianza kupiga kelele eti 'mimi sikuomba msamaha, mimi siwezi 'na pengine kusema kwamba waliachiliwa huru kutokana na shinikizo la kimataifa.
Shinikizo? shinikizo hapa? haiwezikani kabisa! Ukiendelea na msimamo huo unaweza kujikuta umerudi gerezani. Kama ni ushahidi wa kukuonyesha kwamba hatukushinikizwa na yeyote, unaweza kujikuta umerudi gerezani au nje ya nchi ambako utakuwa hauna kazi''.
Rais Kagame amesisitiza kwamba kutoa msamaha ndiyo njia pekee anayoweza kutumia katika kumaliza matatizo yaliyosibu taifa lake na namna ya kulijenga taifa hilo.
Victoire Ingabire alipotoka gerezani alimshukuru rais Kagame kwa msamaha wake lakini akasisitiza kuwa hakuomba msamaha kwa kuwa hakufanya kosa lolote.
''Ni huruma tuliyo nayo lakini huruma inayolenga kutatua matatizo. Tungetoa msamaha unadhani ni watu wangapi ambao bado wangelikuwa gerezani?
Maelfu ya watu wangelikuwa bado gerezani. Lakini kwa sababu tunataka kujenga taifa letu tumeamua hao wahalifu kuwavut , kuwashawishi ili na wao waweze kutoa angalau mchango kidogo wa kujenga taifa. Hii Rwanda mnayoiona ilikotoka ni mbali...tulipata somo la kuhimili matatizo'' ameongeza rais Kagame.
Mbali na hayo, Rais Kagame amelitaka bunge jipya kubuni mkakati wa kushughulikia ipasavyo mafisadi kuliko ilivyokuwa.
Rwanda ni miongoni mwa nchi zinazoaminika kuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi.
Wabunge kwa mara nyingine wamechagua Bi Donatile Mukabalisa kutoka chama cha Liberali kuwa spika wa bunge.
Victoire Ingabire ni nani?
Bi Ingabire alirudi kutoka jela nchini Uholanzi 2010 ili kushiriki katika uchaguzi wa urais.
Alikamatwa na kuzuiliwa kuwania urais na amekuwa akihudumia kifungo jela tangu wakati huo.
Bi Ingabire , ambaye ni mwanachama wa kabila la Hutu, alikuwa akihoji ni kwa nini makumbusho ya mauaji ya halaiki nchini Rwanda ya 1994 hayakuhusisha watu wa kabila la Hutu.
Wengi wa watu 800,000 waliouawa walikuwa watu wa Kabila la Tutsi lakini Wahutu wenye msimamo wa kadri pia waliuawa na Wahutu wenye msimamo mkali.
Chama cha Rwanda Patriotic Front cha Rais Kagame kinachotawaliwa na Watutsi wengi kilimaliza mauaji hayo.