Je, Israa al-Ghomgham atakuwa mwanaharakati wa kwanza mwanamke kuhukumiwa kifo Saudia?

Mwendesha mashtaka wa serikali ya Saudi Arabia ameripotiwa kutaka adhabu ya kifo kwa wanaharakati watano, akiwemo mwanaharakati wa haki za wanawake Israa al-Ghomgham.

Shirika la Human Rights limesema kwamba hivi karibuni lilienda kwenye mahakama ya ugaidi kusikiliza kesi zinazohusisha wale waliofanya maandamano kupinga eneo la Qatif.

Bi.Ghomgham anaaminika kuwa mwanamke wa kwanza kuhukumiwa hukumu ya kifo.

Human right watch imetahadharisha kuwa hatua hiyo itaonyesha mfano mbaya kwa wafungwa wengine wanaharakati .

Watetezi wa haki za binadamu pamoja na wanaharakati wanawake wapatao 13 wamefungwa tangu mwezi mei wakituhumiwa kufanya shughuli zinazohatarisha usalama wa taifa hilo.

Baadhi waliachiwa huru lakini wengine bado wameshikiliwa na vyombo vya usalama bila kujua hatima yao.

Human Rights Watch imesema bi. Ghomgham alikuwa mwanaharakati aliyefahamika katika kushiriki kuandaa maandamano makubwa yaliyofanyika Qatif mwaka 2011.

Wajumbe wa jamii ya Washia walikusanyika barabarani kulalamikia ubaguzi wanaoupata kutoka katika serikali ya Sunni-led.

Bi. Ghomgham na mume wake waliripotiwa kukamatwa mwezi desemba mwaka 2015 na kufungwa katika jela za Dammam's al-Mabahith tangu wakati huo mpaka sasa.

Mwendesha mashtaka amemshtumu Bi. Ghomgham na wanaharakati wengine watano kwa makosa ya kufanya maandamano katika mji wa Qatif,kuwahamasisha watu kuandamana,kuandaa kauli mbiu za kuipinga serikali,kupiga picha za video za maandamano na kuzituma kwenye mitandao ya kijamii pamoja na kutoa msaada kwa waasi,,maelezo hayo ni kwa mujibu wa Human rights watch.

Mwendesha mashtaka ameripotiwa kutaka wapewe adhabu ya kifo kulingana na sheria za kiislamu na chini ya maamuzi atakayofanya hakimu kuhusu kesi hiyo na adhabu itakayo tolewa.

Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu ya Saudi kutoka barani ulaya yamezitaka mamlaka kuondoa adhabu hiyo kwa Bi. Ghomgham.

Aidha serikali ya Saudi Arabia haijasema chochote kuhusu kesi anayoikabili bi. Ghomgham.

Ingawa mahakama hiyo tayari ilishawahukumu kifungo cha maisha wanaharakati kadhaa wa Shia baada ya kuwakamata ,kitu ambacho makundi ya haki ya binadamu yanaona hukumu hizo zinatolewa kutokana na msukumo wa kisiasa.

Maafisa wanasema watu hao walikuwa wana hatia kwa makosa ya ugaidi ikiwa pamoja na kupigana na vyombo vya usalama.