Rashida Tlaib: Mwana wa wahamiaji kutoka Palestina kuweka historia Marekani

Rashida Tlaib binti wa mhamiaji wa Kipalestina anatarajia kuwa mwanamke wa kwanza wa Kiislamu kuinga katika bunge la Congress nchini Marekani.

Mwana mama huyu ambaye aliwahi pia kuwa mwakilishi kutoka jimbo la Michigan ameshinda uchaguzi wa awali kupitia chama cha Democrats katika mji wa Detroit.

Bila ya kuwa na mpinzani kutoka chama kikuuu cha upinzani cha Republican ama mgombea mwengine yeyote aliyewania kiti hiko dhidi yake amejihakikishia kiti hicho katika Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Novemba.

Picha za video katika mitandao ya kijamii zinamuonesha Rashida akiwa katika hali ya kuguswa akiielezea familia yake nyingine iliyo katika eneo la ukingo wa Magharibi, ambao walikuwa wakifuatiulia mafanikio yake hayo katika Televisheni.

Rashida Tlaib ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanasiasa pia alizaliwa mwaka 1976, amekuwa mwanamke wa kwanza wa Kimarekani muislamu kulitumikia baraza la kutunga sheria la huko Michigan.

Ameweka rekodi pia ya kuwa mmoja ya wanawake wengi walioteuliwa mwaka huu baada ya uchaguzi wa jana kuwania nafasi za uwakilishi katika uchaguzi wa mwezi Novemba.

Baada ya uchaguzi wa jana katika majimbo manne nchini Marekani, kwa sasa kuna wanawake 11 wanaowania nafasi ya ugavana na viti 185 katika Baraza la Wawakilishi.