Wanawake Iran wacheza muziki kumuunga mkono binti aliyekamatwa

Baadhi ya wanawake huko Iran wametuma picha za video katika mtandao zinazowaonyesha wakicheza, ili kumuunga mkono binti aliyekamatwa na polisi.

Maedeh Hojabri amekusanya maelfu ya wafuasi wa mtandao wa Instagram kwa picha za video zinazo mwonyesha akicheza muziki wa Iran na muziki wa pop.

Siku ya ijumaa, Televisheni ya taifa ilirusha video ya Hojabri akiomba radhi.

Watumiaji wa mtandao walianza kusambaza picha za video na jumbe mbali mbali ili kumuunga mkono binti huyo anayependa kucheza na walitumia hashtags mbali mbali kama vile "Kucheza sio uhalifu"

Serikali ya Iran ina sheria kali zinazotoa mwongozo kwa wanawake juu ya mavazi na kupinga kabisa mwanamke kucheza muziki na mwanaume hadharani labda iwe mbele ya mwanafamilia.

Lakini picha za video za Hojabri zinamwonyesha binti huyo akicheza nyumbani bila kitambaa cha kusitiri kichwa au Hijab.

Hata hivyo inasemekana kuwa aliyekamatwa si yeye peke yake kwani kuna wachezaji kadhaa ambao pia wamekamatwa wiki za hivi karibuni.

Mmiliki mmoja wa Blog aliandika "ukimwambia mtu yoyote yule duniani kuwa wasichana wa miaka 17 na 18 wana tiwa mbaroni kwa kucheza muziki, furaha na uzuri wao kwa mashitaka ya kueneza uhuni wakati wabakaji wa watoto wako huru watacheka! Kwa sababu hawataamini"

Mmoja wa watumiaji wa mtandao wa Twitter ameandika: "Nacheza muziki ili waone na wajue kwamba hawawezi kuchukua furaha na matumaini yetu kwa kuwatia mbaroni vijana na mabinti kama Maedeh"

Hii si mara ya kwanza kwa wachezaji wa muziki kutiwa mbaroni huko Iran, kwani mapema mwaka huu kiongozi mmoja wa mji wa Mashhad alitiwa mbaroni baada ya picha za video kuonekana zikionyesha wanawake na wanaume wengi wakicheza muziki katika moja ya duka kubwa wakati watu sita walitiwa mbaroni kwa kucheza muziki wa Zumba Mwezi wa nane.

Mwaka 2014 vijana waki Iran sita walio rusha katika mtandao video yao wakicheza wimbo wa mwanamuziki pharell Happy katika mitaa na paa za nyumba huko Tehran walihukumiwa jela mwaka mmoja na fimbo 91.