Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waandamana kupinga kamera za ngono zinazowanasa wanawake kisiri Korea Kusini
Maelfu ya wanawake walikusanyika kwenye mji mkuu wa Korea Kusini Seoul jana Jumamosi, wakitaka hatua kuchukuliwa dhidi ya wale wanaowarekodi wakitumia kamera za siri, yakiwa ndiyo maandamano makubwa zaidi kuwai kufanywa na wanawake nchini humo.
Wahusika hurekodi video au hupiga picha wakitumia kamera zilizofichwa maeneo ya umma.
Licha ya usambazaji wa picha za ngono kuwa haramu nchini Korea Kusini, video na picha hizo husambazwa pakubwa mitandaoni.
Waandalizi wanasema wanawake wanaishi kwa hofu kila mara kuwawatarekodiwa au kupigwa picha bila kujua.
Wakibeba mabango wanawake walioandamana ni vijana wa takriban miaka 20 wanaoonekana kuwa waathiriwa wakubwa wa kamera hizo fiche.
Wanawake hao walifunika nyuso zao kulingana na walivyoshauriwa na waandalizi wa maandamano hayo.
Walioandamana wanasema karibu wanawake 55,000 walishiriki licha ya polisi kusema kuwa walikuwa takriban 20,000.
Korea Kusini imekumbwa na wakati mgumu kukabiliana na kuongezeka kwa uhalifu miaka ya hivi karibuni.
Idadi ya visa vinavyotokana na kamera fiche viliongezeka kutoka 1,100 mwaka 2010 hadi zaidi ya 6,500 mwaka 2017.
Tangu mwaka 2004 Korea Kusini iliagiza kuwa kamera za simu zitengenezwe kwa njia fulani ambapo zitatoa sauti ya juu wakati zinapiga picha au zinarekodi video kuwatahadharisha watu.
Lakini sauti hizo zinaweza kuzimwa na wahusika pia hutundika kamera kwenye ukuta, mifuko, viatu na hata chooni.
Rais Moon Jae-in anasema uhalifu huo umekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Wiki iliyopita aliliambia baraza la mawaziri kuwa wahusika wanastahili kuchukuliwa hatua kali kuliko madhara wanayoyasababisha.