Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kiongozi wa CUF Julius Mtatiro matatani kwa madai ya kumkashifu Rais
Mmoja wa viongozi wa juu wa chama cha upinzani nchini Tanzania CUF Julius Mtatiro alikamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa muda nchini Tanzania kwa tuhuma za kudaiwa kutuma ujumbe kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Ujumbe huo wake unadaiwa kumkashifu Rais Magufuli.
Hatua hii inakuja kufuatia utekelezaji wa sharia mpya ya kimitandao nchini humo,ambayo imekuwa ikipingwa na baadhi ya wanaharakati kwamba inabana uhuru wa kujieleza.Viongozi na wanasheria wa chama hicho wamekuwa wakiendelea na jitihada za kuhakikisha anapata dhamana.
Mtatiro aliandika swali kwenye ukurasa wake wa facebook akiuliza ''Rais kitu gani bwana?'' jambo ambalo lilimsababishia kuingia matatani
Kauli yake mtandaoni inadaiwa kuwa imemkashifu Rais Magufuli.
Maafisa wa polisi walienda kufanya ukaguzi nyumbani kwa Mtatiro kuchukua kifaa alichokitumia kuandikia na kuweja ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii.
Julius Mtatiro aliweka ujumbe huo akimuunga mkono kijana mmoja kutoka Mwanza, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, Justine Emmanuel ambaye ndiye awali aliyeuliza swali hilo kwenye ukurasa wake kisha akakamatwa siku tatu zilizopita.
Msemaji wa CUF, Mbarara Maharagambe amesema ''Tunafanya utaratibu wa kushughulikia dhamana yake kwa kuwa dhamana iko wazi''.
Haikuwa wazi swali hilo lilikuwa na maana gani kwa kuwa halikuwa na maelezo zaidi.
Sheria za Tanzania zinaeleza kuwa matamshi au maandiko ya namna hiyo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani
Ikiwa atakutwa na hatia, Mtatiro atakabiliwa na kifungo cha mpaka miezi sita gerezani.
Wanaharakati wa masuala ya haki za binaadamu wamekuwa wakikosoa mamlaka kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza.
Lakini serikali imesema uhuru usio na mipaka unaweza kusababisha uvunjwaji wa amani.