Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Janet Jackson: Kuwa mama kumenipa furaha isiyo na kifani
Janet Jackson ameweka wazi namna alivyokuwa akihangaika kuipata furaha yake, anasema alikata tamaa kirahisi lakini alifurahi sana baada ya kuwa mama.
Katika barua yake kwa jarida la Essence, mwanamuziki huyo wa miondoko ya pop amesema alikuwa akikabiliwa na msongo ''mkubwa'' wa mawazo maisha yake yote.
Mwanamama huyu mwenye miaka 52 alimshukuru Mungu na mtoto wake wa kiume kwa kumsaidia kuipata amani.
''Furaha yangu ni kumbeba mtoto wangu mikononi na kumsikia akilia ,au tukitazamana.
''Nikimbusu, au nikimuimbia taratibu wakati wa kumbembeleza ili alale ni furaha''.
''Furaha iko kwenye kumshukuru Mungu.Furaha ni kusema 'Asante Mungu, kwa ajili ya maisha yangu, nguvu zangu na uwezo wangu wa kukua kwenye upendo.
Jackson ni mmoja kati ya waimbaji wenye mafanikio katika historia ya chati za muziki za Marekani, akiwa na nyimbo 27 ambazo zilikua miongoni mwa nyimbo 10 bora na nyingine 10 zilizokamata namba moja zikiwemo nyimbo kama Nasty,That's The Way Love Goes na Again.
Alizungumzia namna alivyokuwa akipambana na msongo wa mawazo wakati huo alikuwa anaandaa albamu ya mwaka 1997 , The Velvet Rope, ambayo iliandikwa akiwa katika hali ya kuchoka kihisia
''Kuna wakati nilijiona sina matumaini sina msaada''.
Katika kitabu chake alichokichapa mwaka 2011, True You, nyota huyo alisema alihisi kutojiamini tangu akiwa mtoto-alipokuwa akifanya kazi katika Televisheni, akiwa na miaka 10.
''Kabla ya kazi ya kutengeneza kipindi kuanza, niliambiwa vitu viwili, '' aliandika.'' Nilikuwa mnene na nilitaka kupunguza mwili na kwa sababu nilikua ninaelekea kupevuka kimwili, niliyabana matiti yangu.
''Hali ya kutojiamini huanza tangu utotoni, kujisikia mnyonge.Inaweza kufanana na hali ya kushindwa kufikia viwango vya juu, na pia kunakuwa na masuala ya ubaguzi na jinsia''.